Kamati yaeleza sababu kutupilia rufaa ya Mtaka TOC, watatu kuchuana urais 

WAKATI watu watatu wakipitishwa kuchuana kuwania urais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), kamisheni ya uchaguzi huo imeeleza sababu za kutupilia mbali rufaa ya Anthony Mtaka.

Mtaka alikuwa miongoni mwa wagombea urais kwenye uchaguzi huo utakaofanyika Jumapili ya Aprili 12, 2026 kwenye Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, Posta jijini Dar es Salaam. 

Katika mchujo wa awali, Mtaka sanjari na Rahim Kalyango aliyekuwa akigombea nafasi ya makamu mwenyekiti, walienguliwa kwa kigezo cha kukosa sifa.

Wagombea hao walikata rufaa ambayo kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya uchaguzi huo, Ibrahim Mkwawa, rufaa hiyo pia imetupiliwa mbali.

Akizungumza leo Aprili 7, 2026, Mkwawa amesema wagombea hao baada ya kukata rufaa waliitwa kusikilizwa.

“Rufaa zao pia zimetupiliwa mbali kwa kuwa wamekosa sifa za kugombea zilizoanishwa kwenye katiba ya TOC,” amesema Mkwawa.

Licha ya kutozisema sifa hizo, Mwanaspoti inafahamu moja ya sifa hizo ni kuwahi kuenguliwa kwenye chaguzi za chama kilicho chini ya TOC.

Mtaka aliwahi kuenguliwa katika uchaguzi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) alipokuwa akitetea kiti cha urais, sanjari na aliyekuwa makamu wake, William Kallaghe, ingawa Kallaghe aligombea kwenye muhula uliofuatia na kushinda.

Akizungumzia uchaguzi wa Aprili 12, 2026, Mkwawa amesema orodha ya mwisho iliyopitishwa ina wagombea watatu kwenye nafasi ya urais.

Wagombea hao ni Henry Tandau na Leonard Thadeo kutoka Tanzania Bara na Hassan Khairalla Tawakal wa Zanzibar.

Nafasi ya makamu wa rais ina mgombea mmoja, Nassra Juma Mohammed, huku kwenye ujumbe wagombea 20 wanachuana kuwania nafasi 10, tano kutoka Bara na zingine Zanzibar.

Amesema wagombea wote wanaruhusiwa kuendelea na kampeni kwa siku tano kuanzia Aprili 7 hadi Aprili 11, 2026 tayari kwa uchaguzi huo.

Mkwawa ameonya vitendo vya rushwa akisisitiza kwamba mgombea atakayebainika ataenguliwa kwenye kinyang’anyiro hicho.

“Sheria za uchaguzi zina kanuni zake, hivyo ni muhimu wagombea kufanya kampeni kwa kuzingatia sheria na kanuni hizo,” amesisitiza.

Wapiga kura 41 wanatarajiwa kupiga kura siku hiyo kupata uongozi mpya wa TOC kwa muhula mwingine.