Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameongoza Watanzania kumuenzi aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume, kwa kushiriki dua maalumu na kuweka shada la maua katika kaburi lake.
Sheikh Karume, mwanamapinduzi aliyeuawa Aprili 7, 1972, ni zaidi ya nusu karne sasa hayupo duniani, lakini matendo yake na mema aliyoyafanya kwa ajili ya taifa yanamfanya aendelee kukumbukwa.
Kiongozi huyo alijitoa muhanga kwa ajili ya taifa lake la Zanzibar (lilivyokuwa wakati huo) kabla ya kujiunga na Tanganyika takribani miaka 60 iliyopita.
Rais Samia na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, wametoa ujumbe wao juu ya siku hii ya kumbukizi ya kifo cha Hayati Karume.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akishiriki Dua maalum ya kumuombea aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Hayati Abeid Amani Karume ikiwa ni miaka 54 tangu kuuawa kwake. Dua hiyo maalum imefanyika Afisi Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kisiwandui, Zanzibar Aprili 7, 2026.
Leo Aprili 7, 2026, ni siku ya kukumbukwa kwake ambapo Rais Samia ameshiriki dua maalumu akiambatana na viongozi wenzake kutoka Zanzibar na Bara.
Kukumbukwa kwake leo kunatimu miaka 54 ya kifo chake, ambapo Rais Samia amewawakilisha Watanzania kuweka shada la maua katika kaburi lake katika Ofisi Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui, Zanzibar.
Viongozi mbalimbali wameshiriki, akiwemo Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba na Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
Awali, kabla ya matukio hayo mawili kuhitimisha kilele cha kumbukumbu ya kiongozi huyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania, Alhad Mussa Salum, amesema Karume amewanufaisha watu wa Zanzibar na Tanzania Bara.
Amemtaja Karume kama kiongozi aliyejenga ujasiri na uthubutu katika utendaji wa mambo kwa kuweka misingi ya utu na ubinadamu.
Amesema kiongozi huyo ameweka misingi ya umoja na mshikamano baina ya Tanzania na Zanzibar ambao hauvunjika kamwe.
“Ujasiri ambao leo tunausema Wazanzibar wanao katika uthubutu wa mambo na umakini ni kwa sababu ya Karume.
“Alikuwa kiongozi aliyejiamini na aliyetuunganisha katika umoja wa kitaifa, jambo ambalo Mtume Muhammad alituelekeza. Mtu kama huyu kumuombea dua tuna haki na kila sababu ya kufanya hivyo,” amesema.
Alhaj Salum amesema suala la kumuombea dua Karume si la leo, ni zaidi ya miaka 50 sasa wanamuombea.
Amebainisha kuwa ipo kila sababu ya kuamini kwamba Karume anakwenda peponi hata kama alifanya kosa gani kwa namna wanavyomuombea dua.
Ujumbe wa Samia, Dk Mwinyi
Katika ujumbe wake aliouweka kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, Rais Samia amesema: “Naungana na Watanzania wote kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Muasisi wa Muungano.”
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiweka Shada la Maua katika Kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Hayati Abeid Amani Karume mara baada ya Dua iliyofanyika katika Afisi Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui Zanzibar leo Aprili 7, 2026, katika Siku ya Kumbukumbu ya (Karume Day).
“Tutaendelea kumkumbuka na kumuenzi Mzee wetu Karume kwa uzalendo, ujasiri, uthubutu na mchango wake mkubwa katika kudumisha amani, umoja, mshikamano na maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Heri ya Kumbukizi ya Siku ya Karume!”
Naye Rais Mwinyi kwenye akaunti zake za kijamii ameandika: “Leo tunaadhimisha Siku ya Kumbukizi ya Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar na kiongozi shupavu aliyelijenga taifa letu.”
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiweka Shada la Maua katika Kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Hayati Abeid Amani Karume mara baada ya Dua iliyofanyika katika Afisi Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui Zanzibar leo Aprili 7, 2026, katika Siku ya Kumbukumbu ya (Karume Day).
“Tunaendelea kuuenzi mchango wake kwa kudumisha amani, mshikamano na kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya maendeleo ya Zanzibar na taifa kwa ujumla. Mwenyezi Mungu amrehemu Hayati Sheikh Abeid Amani Karume na kumpa pepo ya milele.”
