Wananchi Makambako wakubali mradi wa umwagiliaji, wadai uhakika wa umiliki ardhi

Njombe. Baada ya miezi ya hofu na sintofahamu kuhusu hatima ya ardhi yao, hatimaye wananchi wa mitaa ya Kihanga, Idofi, Kikula na Kipagamo katika Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe wamekubali utekelezaji wa mradi wa kilimo cha umwagiliaji katika eneo la Balali lenye ukubwa wa takribani ekari 1,300.

Hata hivyo, pamoja na kuunga mkono mradi huo, wananchi hao wameiomba Serikali kuhakikisha wanamilikishwa rasmi maeneo yao kwa kupatiwa hati miliki kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo, ili kulinda maslahi yao ya ardhi.

Wananchi hao wametoa kauli hiyo Aprili 7, 2026, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Makambako ukiongozwa na Mbunge wa Makambako ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo.

Awali, baadhi ya wananchi walikuwa na hofu kuwa utekelezaji wa mradi huo ungeweza kusababisha kupoteza maeneo yao ya ardhi.

Hata hivyo, baada ya kupatiwa elimu kuhusu namna mradi utakavyotekelezwa, wengi wao wamekubali kuupokea wakiamini utasaidia kuongeza tija katika kilimo.

Mmoja wa wananchi wa eneo hilo, Afrikanus Kipungu, amesema wanapokea mradi huo kwa matumaini, lakini wanahitaji uhakika wa kisheria kuhusu umiliki wa ardhi yao.

“Kama wanachokisema kinatoka moyoni tunashukuru, lakini ni vizuri wakaanza kutupatia hati miliki za maeneo yetu kabla ya mradi kuanza. Watu wanabadilika, leo unaweza kuambiwa jambo, kesho likawa tofauti,” alisema Kipungu.

Kwa upande wake, Faraja Ngunda amesema wananchi wanahitaji kufahamu namna watakavyonufaika na mradi huo ili kuepuka hali ya baadhi yao kuwa wahanga wa maendeleo.

Baadhi ya wananchi wa halmashauri ya mji wa Makambako wakiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Idofi halmashauri ya mji wa Makambako mkoani Njombe.

“Shauku ya kila mwananchi ni kuona mradi huu unamnufaisha. Inawezekana ukaja, lakini mimi nikabaki muhanga, nikapoteza eneo langu bila kunufaika,” alisema Ngunda.

Akizungumza katika mkutano huo, Meneja wa Umwagiliaji Mkoa wa Njombe, Machage Mwema amewahakikishia wananchi kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha kila anayemiliki ardhi katika eneo hilo anapatiwa hati miliki ili kulinda maeneo yao dhidi ya uvamizi.

Amesema hatua hiyo inalenga kuzuia migogoro ya ardhi inayoweza kujitokeza mara baada ya kuanzishwa kwa miundombinu ya umwagiliaji.

“Baada ya kuweka miundombinu ya umwagiliaji, maeneo hayo huwa na thamani kubwa na watu huanza kuyatamani. Ndiyo maana tunataka kuhakikisha kila mwenye eneo anamiliki kihalali kwa hati miliki,” alisema Mwema.

Ameongeza kuwa mradi huo utakuwa na miundombinu mbalimbali, ikiwemo mabwawa ya kuhifadhi maji kwa ajili ya kilimo, mabwawa ya samaki, chumba cha baridi kwa ajili ya kuhifadhi mboga mboga pamoja na soko la kuuza mazao ya wakulima.

Akizungumza kwenye hadhara hiyo, Chongolo amesema mradi huo ni muhimu katika kuimarisha kilimo cha umwagiliaji na kuongeza kipato cha wananchi wa eneo hilo.

Amesisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuwa wazi kwa wananchi kuhusu miradi ya maendeleo ili kuondoa hofu na kujenga uaminifu.

“Unapokuwa kiongozi lazima useme ukweli kwa wananchi wako kuhusu miradi inayokuja. Hatuwezi kuficha jambo lolote,” amesema Chongolo.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha uongozi wake hataruhusu mwananchi yeyote kupokonywa ardhi yake kinyume cha sheria.

Meneja Umwagiliaji Mkoa wa Njombe, Machage Mwema akizungumza na wananchi kuhusu mradi kilimo cha umwagiliaji unaotarajia kuanza hivi karibuni hulo halmashauri ya mji wa Makambako mkoani Njombe.

“Mimi ni mbunge wenu kwa miaka mitano. Kama kuna mtu atanyang’anywa eneo lake, aje kuniambia, kwa sababu hapo nitakuwa nimefanya kosa,” amesema Chongolo.

Mradi huo unatarajiwa kusaidia wakulima wa Makambako kuondokana na utegemezi wa mvua pekee na hivyo kuongeza uzalishaji wa mazao pamoja na kuimarisha uchumi wa wananchi wa eneo hilo.