Morogoro. Tabasamu na matumaini mapya vimeanza kuonekana kwa baadhi ya wazazi na walimu katika Shule ya Msingi Mkwatani, wilayani Kilosa mkoani Morogoro, baada ya Taasisi ya Multi Dome Relief Center kukabidhi vitimwendo vitano kwa watoto wenye ulemavu pamoja na mashine ya fotokopi kwa ajili ya kusaidia shughuli za kielimu shuleni hapo.
Msaada huo wenye thamani ya zaidi ya Sh5.3 milioni umetolewa Aprili 7, 2026, ukiwa na lengo la kupunguza changamoto wanazokumbana nazo watoto wenye ulemavu na kuboresha mazingira ya ujifunzaji kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Kwa wazazi wengi, msaada huo unaonekana kuwa mwanzo wa mabadiliko katika maisha ya watoto wao ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za usafiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kielimu.
Mzazi wa mwanafunzi katika shule hiyo, Dhaifa Nyakunga, amesema mashine ya fotokopi itasaidia kupunguza mzigo wa gharama ambazo wazazi walikuwa wakichangia kwa ajili ya uchapishaji wa mitihani.
“Mashine hii itawarahisishia walimu kuandaa mitihani na kupunguza gharama kwa wazazi. Tunaamini sasa wazazi wengi watashiriki zaidi katika vikao vya shule na maendeleo ya watoto wao,” amesema Nyakunga.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Mkwatani, Shabaan Kilumbi, ambaye amesema kabla ya kupatikana kwa mashine hiyo baadhi ya wazazi walikuwa wakikwepa vikao vya shule kutokana na michango ya mitihani.
“Changamoto ya gharama za kudurufu mitihani ilikuwa kubwa. Wazazi wengine waliona mzigo mkubwa, lakini sasa tunatarajia hali hiyo itapungua na ushiriki wao utaongezeka,” amesema Kilumbi.
Kwa upande wa wazazi waliopokea vitimwendo, msaada huo umeonekana kuwa suluhisho la changamoto walizokuwa wakikumbana nazo katika kuwahudumia watoto wao.
Mkazi wa Chamwino, Dyness Cephar (26), ambaye ana mtoto mwenye ulemavu wa viungo, amesema kwa muda mrefu alikuwa analazimika kumbeba mtoto wake mgongoni kila alipohitaji kumpeleka sehemu mbalimbali.
“Nilikuwa napata shida sana kumbeba mtoto wangu mgongoni kila ninapotoka naye. Sasa baada ya kupata hiki kitimwendo, nitakuwa na uwezo wa kumpeleka sehemu mbalimbali kwa urahisi. Hata suala la kuanza shule linawezekana kwa sababu ana umri wa miaka saba,” amesema Dyness.
Naye Winfrida Franchis (35), mkazi wa Misongeni Bigwa, amesema msaada huo utamwezesha mtoto wake kuanza kuzoea mazingira ya kijamii na kucheza na watoto wengine.
“Hii baiskeli itanisaidia kumtoa mtoto nje acheze na wenzake. Kabla ya hapo nilikuwa namweka ndani kwa sababu sikuweza kumbeba kila wakati,” amesema Winfrida.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mkwatani, Tatu Muhomba, amesema mashine ya fotokopi imekuja wakati muafaka kwani itarahisisha maandalizi ya mitihani na kupunguza gharama kwa wazazi.
“Tulikuwa tunachangisha hadi Sh200 kwa kila mwanafunzi zaidi ya 400 kwa ajili ya mitihani, lakini sasa mzigo huo umepungua. Pia walimu walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kudurufu mitihani,” amesema Muhomba.
Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Multi Dome Relief Center Morogoro, Fauzi Al Bagarah (Mwenye Kazu) akizungumza jambo na wazazi na walimu wa shule ya msingi Mkwatani baada ya taasisi hiyo kukabidhi msaada wa mashine ya fotokopi yenye thamani ya sh3.5milioni wilaya ya kukosa mkoa wa Morogoro. Picha na Juma Mtanda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Multi Dome Relief Center, Fauzi Al Baraggar, amesema taasisi hiyo inaendelea kushirikiana na Serikali kusaidia makundi yenye mahitaji maalumu, wakiwemo watoto yatima, wazee na wajane.
Amesema tangu Januari mwaka huu taasisi hiyo imetoa vitimwendo vitano vyenye thamani ya Sh1.7 milioni na mashine moja ya fotokopi yenye thamani ya Sh3.5 milioni, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha ustawi wa jamii.
“Lengo letu ni kushirikiana na Serikali kuboresha huduma za kijamii na kuinua elimu hasa katika maeneo ya vijijini,” amesema Baraggar.
Aidha, amewataka wazazi kuacha kuwafungia watoto wenye ulemavu ndani ya nyumba, akisema hatua hiyo huwanyima fursa ya kushirikiana na wenzao na kuchelewesha maendeleo yao.
“Watoto hawa wanahitaji kushiriki katika jamii kama watoto wengine. Kuwafungia ndani kunawafanya waogope watu na kushindwa kujiamini,” amesema.