Dar es Salaam. Hatua ya Rais wa Cameroon, Paul Biya, amemteua mwanawe Franck Emmanuel Biya kuwa makamu wake, jambo ambalo limeibua mjadala kuhusu mipaka ya uongozi wa kifamilia na athari zake kwa uwajibikaji wa umma katika mifumo ya kisiasa barani Afrika.
Hatua hiyo imekuja kufuatia mabadiliko ya katiba yaliyorejesha nafasi ya Makamu wa Rais katika mifumo ya utawala wa taifa hilo, huku nafasi hiyo ikipewa mamlaka makubwa, ikiwemo kurithi moja kwa moja uongozi wa nchi endapo Rais hatakuwepo madarakani kwa sababu mbalimbali.
Katika muktadha huo, mjadala umejikita siyo tu kwa mtu aliyeteuliwa, bali taswira ya familia ndani ya dola na namna inavyoathiri imani ya umma kwa taasisi za uongozi.
Kufuatia taarifa zilizoripotiwa kutoka nchini humo Aprili 6, 2026, Rais Biya amemteua mtoto wake huyo kuwa makamu wake, hatua inayohofiwa kuwa mkakati wa kumrithisha kiti cha urais atakapoachia wadhifa huo.
Wachambuzi wa siasa na wanasheria wanaona tukio hilo linafungua ukurasa mpana wa mjadala unaogusa mgongano wa kimaadili kati ya uaminifu binafsi wa kiongozi kwa watu wake wa karibu na wajibu wa kulinda misingi ya uwajibikaji wa umma.
Wakati katiba za nchi nyingi hazizuii uteuzi wa aina hii, hoja kuu imeendelea kubaki kwenye namna jamii inavyopokea uamuzi huo na athari zake kwa dhana ya usawa katika upatikanaji wa viongozi, ambapo kila inapotokea uteuzi wa ndugu wa Rais, mijadala imekuwa ikishika kasi.
Wachambuzi wa kisiasa wameibua tafakuri iwapo uteuzi wa aina hii unajengwa juu ya uwezo na uzoefu au unafungua mianya ya mgongano wa masilahi na kudhoofisha uwajibikaji serikalini.
Uteuzi wa Biya kwa mtoto wake umeamsha fikra zaidi kutokana na viongozi wengine barani Afrika kutumia nafasi zao na kuwateua ndugu zao katika nafasi za juu na nyeti katika uongozi wa nchi, hatua ambazo zimekuwa zikizua mitazamo tofauti katika jamii.
Miongoni mwa mifano ya hivi karibuni ni Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara, aliyemteua mdogo wake, Tene Ouattara, kuwa Naibu Waziri Mkuu baada ya kushika nafasi ya Waziri wa Ulinzi.
Mbali na huyo, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amemteua mwanawe Muhoozi Kainerugaba kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na ndugu yake Salim Saleh kuwa mshauri mkuu wa Rais masuala ya ulinzi, nafasi za juu na nyeti zaidi kwa uongozi wa taifa hilo la Afrika Mashariki.
Aidha, kilichotokea Cameroon pia kimeonekana nchini Equatorial Guinea, ambako Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo alimteua mwanawe Teodorin Nguema kuwa Makamu wa Rais, hatua iliyotafsiriwa na baadhi ya wachambuzi kama sehemu ya maandalizi ya urithi wa madaraka.
Pamoja na tofauti za mazingira ya kisiasa katika nchi hizi, hoja inayojirudia ni namna uteuzi wa ndugu katika nafasi nyeti unavyogusa misingi ya uwajibikaji na uhalali wa kisiasa, hasa katika zama ambazo Afrika imekuwa na kilio kuhusu usimamizi wa rasilimali za umma, rushwa na uwajibikaji wa viongozi serikalini.
Mjadala wa uwajibikaji na maadili ya uongozi
Wachambuzi wa siasa wanasema kikatiba, marais wengi wana mamlaka ya kufanya uteuzi huo, lakini kimaadili hatua hizo zinadhoofisha imani ya umma kwa taasisi za dola, wakionya kuwa busara inahitajika katika kufanya maamuzi hayo.
Kwa upande mwingine, baadhi yao wanatetea uteuzi huo wakisema uaminifu, uzoefu na uwezo wa mteule ni vigezo muhimu vinavyopaswa kupewa kipaumbele, wakisisitiza kuwa ndugu wa Rais hakupaswi kuwa kikwazo cha mtu kulitumikia taifa lake.
Mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala bora, Profesa Mohamed Makame anasema suala la uteuzi halijafungwa na mahusiano ya mtu na anayeteua, bali limefungwa na sifa za mtu anayetakiwa kuteuliwa.
“Bila shaka kwa maisha yetu Afrika na nchi maskini tulizonazo, wengi huona kama kuteuliwa uongozi ni fursa ya kutoka kimaisha; jamii huangalia zaidi maslahi ya kiuchumi anayoyapata anayeteuliwa badala ya majukumu ya nafasi anayoteuliwa. Hiki ndicho chanzo cha malalamiko na ukosoaji unaosikika,” anasema.
Mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza), Profesa Makame anasema manung’uniko kuhusu upendeleo wa uongozi hayaishii kuangaliwa undugu wa wateuliwa na mteuaji, bali huenda hadi kwenye majimbo, makabila au vyama vya siasa, akisema yote huweza kutumiwa kukosoa kuwa mamlaka ya uteuzi inapendelea.
“Mimi naona jambo la msingi siyo uhusiano wa kiudugu kati ya mteuaji na mteuliwa, bali utendaji wa anayeteuliwa. Kuwalalamikia wanaoteuliwa kwa kuangalia udugu wao na Rais badala ya utendaji wao kutawanyima nafasi watu wenye sifa kuwa viongozi kisa ndugu yao amepata urais. Hata hivyo, busara inahitajika kwa wanaoteua; isiwe mtu akiwa Rais basi ndugu wote wapate teuzi kwenye uongozi,” anasisitiza.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Faraji Mangula anaona hatua hii inachochewa na hofu ya viongozi kupata misukosuko watakapoondoka madarakani, hivyo wanateua ndugu zao ili wawarithishe uongozi na kuwahakikishia usalama wao baadaye.
“Hii ni hatari kubwa kwenye eneo la uwajibikaji na maadili. Kiongozi akifanya makosa, inakuwa ni ngumu kwa Rais kumchukulia hatua kali za kinidhamu. Pia inajenga uwezekano kwa viongozi kukaa muda mrefu sana madarakani, na inathibitisha utamaduni unaojengeka barani Afrika ambapo marais wengi wakiingia madarakani huona wakitoka watapata misukosuko; hivyo wanang’ang’ania madarakani, na wanapotaka kutoka, wanataka kuweka watu wao kujihakikishia usalama,” anasema.
Kwa mtazamo wa kisheria, Wakili Onesmo Kyauke anasema kuteua ndugu siyo kosa kisheria iwapo sifa na vigezo vinazingatiwa, akieleza kuwa changamoto kubwa ipo katika mifumo ya uwajibikaji ambapo Rais sasa atawajibika kusimamia ndugu yake na siyo mteule wake pekee.
“Tatizo halipo kwenye udugu, bali kwenye uwajibikaji na mifumo ya udhibiti. Hoja kuu zinazochochea ukosoaji ni uwajibikaji unaoibua swali kuwa ndugu wa Rais akikosea, atachukuliwa hatua kama raia mwingine? Pale ambapo majibu ni ‘hapana’, basi tatizo halisi linaanzia hapo,” anasema.
Anasema hata kama mteule ana sifa, jamii inaweza kuona mfumo umefungwa kwa watu wachache, hali inayoweza kupunguza imani ya umma kwa taasisi za dola, akisisitiza kuwa mjadala huu utaendelea kuwepo kadri mifumo ya uongozi inavyojaribu kusawazisha uaminifu binafsi na uwajibikaji wa umma, hata kama sheria hazizuii uteuzi wa namna hiyo.
Kwa upande wake, Mangula anaona kuwa sheria zinapaswa kuweka masharti katika mifumo ya uteuzi ili kuwadhibiti marais kuweka watu wa familia zao katika nafasi nyeti serikalini, ili kulinda uwajibikaji wa kweli na imani ya jamii kwa mamlaka za dola. Anabainisha kuwa bila kufanya hivyo, kiongozi anaweza kutumia vibaya mamlaka yake kufanya teuzi za upendeleo kwa ndugu zake kwenye nafasi nyeti za uongozi wa nchi.
