Dar es Salaam. Hujafa, hujaumbika. Ndivyo unaweza kuelezea safari ya maisha ya kijana Abdallah Khalid aliyeshindwa kufikia ndoto zake za kuwa udaktari bingwa wa mifupa kutokana na ulemavu wa miguu.
Hata hivyo, licha ya changamoto hizo, Khalid hakukata tamaa na sasa anaanza safari mpya ya kuisaka kesho yake kwa kuuza mayai maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam bila kujali ulemavu wake.
Ni wazi kila mtu anapoanza safari ya maisha, kuanzia elimu, huwa na ndoto zake, lakini changamoto mbalimbali za kimaisha ndizo hubadili mtazamo na mwelekeo wa anapofikiria.
Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Khalid, kijana na mkazi wa Kigamboni anayejishughulisha na biashara ya kuuza mayai ya kuchemsha kwa kuyatembeza mtaani kwenye viunga vya jiji hilo.
Hata hivyo, kwa muonekano, huwezi kudhania kama Khalid anaweza kumaliza kuuza hata trei moja ya mayai kutokana na changamoto ya ulemavu wa viungo aliyonayo.
Abdallah Halidi, akiwa anarejea nyumbani kwake baada ya kutoka kununua mayai yanapouzwa kwa bei ya jumla jirani na anakoishi Gezaulole Juu, Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Kijana huyo hutembea kwa kutumia mikono ambayo huivalisha malapa aina ya ‘yeboyebo’ ili asiumie wakati anapotambaa. Pia, miguu yake iliyojikunja ndiyo hutumia kama mikono kubeba mayai na vitu vingine.
Pamoja na ulemavu wake huo, Khalid mwenye miaka 24, amekuwa akienda kununua bidhaa hizo akiwa peke yake hadi kuyaandaa tayari kwa ajili ya biashara ili apate riziki.
Katika simulizi hii na Mwananchi, anaeleza kuwa kwa siku huuza trei mbili hadi tatu kama biashara imeenda vizuri, na anashukuru ni kazi ambayo imemuwezesha kuendesha maisha yake kama kulipa kodi ya nyumba huko Gezaulole Juu, Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Biashara hiyo, mbali na kuuza Kigamboni, huwa akienda hadi feri upande wa Wilaya ya Ilala na wakati mwingine hufika hadi Kariakoo jijini hapa kwa ajili ya kutafuta wateja ili kusogeza maisha mbele.
Khalid alizaliwa miaka 24 iliyopita huko Kasulu Mjini, Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, akiwa na changamoto ya ulemavu huo wa kupinda kwa miguu.
Anasema wazo la kufanya biashara hiyo lilikuja mwaka 2021, ikiwa ni mwaka mmoja tangu aliposhindwa kuendelea na shule katika Shule ya Kabanga Mazoezi iliyopo Kasulu baada ya kuumwa miguu kwa muda mrefu.
Kijana Abdallah Halidi, akiwa anakoka moto kwa ajili ya kuchemsha mayai nyumbani kwake Gezaulole Juu, Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda kuyauza.
Katika mahojiano maalumu, anaeleza kuwa wakati huo alipokuwa ameingia darasa la saba, wazazi wake hawakuwa na uwezo wa kumpeleka hospitali, bali waliishia kumpa dawa za kupunguza maumivu.
Anafafanua kuwa hali hiyo aliendelea nayo hadi kushindwa kufanya mtihani wa Taifa wa kumaliza elimu ya msingi, na ikawa ndiyo mwisho wake wa kuendelea na shule tofauti na ilivyokuwa malengo yake.
Anasema baada ya kukaa nyumbani takribani mwaka mmoja, alijiuliza atakaa hivyo hadi lini ilhali anapumua kama walivyo wengine, ndipo akapata wazo la kuanzisha biashara ya mayai ya kuchemsha huko Kasulu.
Anasema licha ya kuianza biashara hiyo kwa changamoto, ikiwemo kutouza hata trei moja, hakukata tamaa kwani alijipa matumaini kadri siku zilivyokuwa zikisogea.
“Baadaye niliwasiliana na baadhi ya marafiki zangu waliokuwa Dar es Salaam, nikauliza hali ya biashara, nikaambiwa kuna mzunguko wa watu wengi, nikamuomba mmoja wao anitafutie chumba,” anasema.
“Nashukuru Mungu, uamuzi wangu haukuwa mbaya kwa kuwa wakati nikiwa Kasulu nilikuwa nikiuza trei moja, lakini baada ya kuja Dar es Salaam walau namaliza trei mbili hadi tatu,” anasema Khalid.
Kuhusu ratiba yake, anasema huamka saa 12 asubuhi kufuata mayai yanapouzwa kwa bei ya jumla na anaporudi huyaosha kisha kuyachemsha kwa takribani nusu saa, na baada ya hapo huyapanga kwenye trei kwenda mtaani sokoni.
Kuhusu changamoto, anasema huwa anakutana nazo zaidi kipindi cha jua kali au wakati wa mvua, ambapo huchukua muda mrefu kumaliza kuuza kwa sababu huchoka kutokana na hali ya hewa.
“Ikiwa kuna jua kali huwa nachoka sana na kulazimika kupumzika kila baada ya hatua chache, na mvua zikinyesha pia nashindwa kutoka. Kutokana na hilo, huwa narudi nyumbani hadi saa nne usiku, jambo ambalo si rafiki kwangu,” anasema.
Abdallah anasema yeye ni mtoto wa tatu kati ya watoto wanne wa mzee Khalid Juma na Mariam Hussein na ndoto yake ilikuwa ni kuwa daktari bingwa wa mifupa ili kuwasaidia wenye ulemavu wa viungo.
“Nilipenda niwe daktari wa mifupa ili niweze kuwatibu watoto wanaozaliwa na ulemavu au wanaopitia changamoto za ulemavu wa viungo, lakini ndiyo hivyo hali ya kifamilia niliyonayo sikuweza kufikia ndoto hizo,” anasema.
Baada ya ndoto zake za kuwa daktari kushindwa kutimia, Khalid kwa sasa anasema anacholenga ni kuwa mfanyabiashara mkubwa wa mayai kwa bei ya jumla na vinywaji, japokuwa tatizo ni mtaji.
Kuhusu elimu au uelewa juu ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri, Khalid anasema imemuwia vigumu kwa kuwa anajua lazima uwe na biashara ya uhakika itakayokuwezesha kurejesha mkopo unaochukua.
Kuhusu alivyoiona Dar es Salaam na namna alivyokuwa akiichukulia wakati akiwa Kasulu, anasema ni mkoa ambao unatakiwa kujituma kwa kuwa kupambana ndiyo kula kwako.
“Pamoja na yote hayo sijawahi kujutia kuja Dar es Salaam kwa kuwa kila ninapokwenda sijawahi kukata tamaa. Naamini nikiendelea kupambana kuna siku nitafika mbali na kuzitimiza ndoto zangu,” anasema Khalid.
Kuhusu mchango wake kwa familia, hasa kwa ndugu na wazazi wanapohitaji chochote hususani kifedha, Khalid anasema huwa hawamuombi na yote hayo anasema wanajua bado anajitafuta.
Hata hivyo, anasema anashukuru tangu alipoanza kuonekana kwenye mitandao ya kijamii, ameweza kufunguliwa kibanda kwa ajili ya kuuza mayai na vinywaji, hivyo anaamini sasa anaenda kufanya biashara yake katika sehemu ya kudumu.
Pamoja na hatua hiyo, anaomba wadau kujitokeza kumshika mkono zaidi, kwa kuwa ameanza na mayai trei 50 kwa sasa, na anatamani kufikisha hata trei 100, mtaji ambao unahitaji awe na takribani Sh700,000.
“Kwa upande wa vinywaji nimeanzishiwa vya Sh200,000, lakini natamani kufikisha hata Sh400,000. Nawaomba wadau wanisapoti na ninashukuru kwa kupata sehemu rasmi ya kufanyia biashara zangu,” anasema Khalid.
Abdallah anasema wasikate tamaa na badala yake wajitume kufanya kazi ambayo wanaona wanaweza kuifanya kulingana na hali zao badala ya kutegemea kuomba.
“Katika hili naomba nisisitize, ulemavu usiwe sababu ya kuishi kwa kuomba. Kikubwa Mungu kakujalia uhai ambao unaweza kufanya kazi. Hata hao unaowaomba ipo siku watakuchoka,” amesema.
Walichosema majirani zake
Mmoja wa majirani, Zulphine Musa, anasema Khalid anatoa somo kubwa kwa watu wenye ulemavu ambao wengine wanaona maisha yaliyobaki ni kuomba.
“Hata sisi mara ya kwanza tulipomuona anaandaa mayai na kwenda kuyatembeza tulimshangaa, lakini mwisho wa siku tukamzoea na kusema kumbe kila kitu kinawezekana bila kujali una ulemavu.
“Kwa ujumla kuna la kujifunza kwa watu wa aina yake, lakini hata kwa walio wazima kujishughulisha badala ya kutegemea kuishi kwa kuomba,” anasema Zulphine.
Naye Ally Sadick anasema Khalidi ni mtu mwenye jitihada na kujituma, na wanafurahi kuona waandishi wakifika hapo kuonyesha kile anachokifanya. Anaamini wenye uwezo wa kumsaidia wataweza kufanya hivyo.
Kwa msomaji yeyote atakayeguswa na makala hii, unaweza kumsaidia Khalidi kupitia namba 0697536417 au kuwasiliana na mwandishi wa makala hii kwa namba 0759062281.
