Unguja. Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi wamewaomba wananchi kuendelea kuenzi mchango uliotolewa na aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume kwa kuendeleza maono yake, kutenda haki bila ubaguzi kama alivyofanya yeye.
Wamesema hayo leo Jumanne, Aprili 7, 2026 siku ya kumbukizi ya kifo chake na waliposhiriki dua ya kumbukizi ya miaka 54 ya kifo cha Hayati Karume Makao Makuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Kisiwandui kwa viongozi na wananchi.
Karume aliuawa Aprili 7, 1972 kwa kupigwa risasi na mlinzi wake katika jengo la Makao Makuu ya Chama cha Afro Shiraz Kisiwandui Mjini Zanzibar ambapo kwasasa ndio Makao makuu CCM, na kaburi lake lipo nje Kaskazini mwa ofisi hizo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akishiriki Dua maalum ya kumuombea aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Hayati Abeid Amani Karume ikiwa ni miaka 54 tangu kuuawa kwake. Dua hiyo maalum imefanyika Afisi Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kisiwandui, Zanzibar Aprili 7, 2026.
Akitoa mawaidha katika dua hiyo kwa niaba ya masheikh wenzake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maelewano Tanzania Sheikh Alhad Mussa Salum amesema Aliyekuwa Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema wanakila sababu ya kumuombea dua kwasababu alitenda mema mengi kwa wananchi.
Sheikh Alhad ambaye ni Sheikh Mkuu mstaafu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alisema wana kila sababu ya kuamini Mzee Karume anakwemda peponi hata kama alifanya kosa la namna gani lakini kwa dua anazoombewa na matendo aliyowatendea watu hakuna sababu kutoamini kwamba atakuwa peponi.
“Sheikh Karume hasauliki na hawezi kusahaulika kwasababu aliyotafanya mazuri ni mengi na tunaendelea kuona alama zake,” amesema.
“Kuna watu wamekufa lakini mioyo yao haijafa na kuna watu wanaishi lakini mbele za watu ni kama wafu, maana hawana jambo ukiwauliza wamesaidia nini jamii hawana, wewe ni sawa na mfu tu lakini kuna watu hawatasahaulika, mmoja ni Mzee Karume,” amesema.
Naye mzee wa kisiwani humo, Abdulhamid Msangama amesema walipata fursa na matunda ya Mzee Karume ambapo aliacha alama na sasa wanaendelea kunufaika nayo.
“Mzee Karume alikuwa na ofisi yake ya OKM iliyokuwa ikisimamia hali za wananchi usawa kwa wote bila kujali matabaka yake,” amesema.
Alisema yeye (Karume) ndiye alianzisha uchumi wa buluu, alikuwa mwanamichezo na wakati anafariki dunia alikuwa akicheza bao ofisini.
“Kwa Wazanzibari alichokifanya hawezi kusahaulika kwasababu waliwaunganisha Wazanzibar na kuwafanya wawe kitu kimoja na kuwafanya waoane hivyo ameacha alama kubwa,” amesema.
Ujumbe wa Samia, Dk Mwinyi
Katika ujumbe wake aliouweka kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, Rais Samia amesema: “Naungana na Watanzania wote kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Mwasisi wa Muungano.”
“Tutaendelea kumkumbuka na kumuenzi Mzee wetu Karume kwa uzalendo, ujasiri, uthubutu na mchango wake mkubwa katika kudumisha amani, umoja, mshikamano na maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Heri ya Kumbukizi ya Siku ya Karume!”
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiweka Shada la Maua katika Kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Hayati Abeid Amani Karume mara baada ya Dua iliyofanyika katika Afisi Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui Zanzibar leo Aprili 7, 2026, katika Siku ya Kumbukumbu ya (Karume Day).
Naye Rais Mwinyi kwenye akaunti zake za kijamii ameandika: “Leo tunaadhimisha Siku ya Kumbukizi ya Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar na kiongozi shupavu aliyelijenga taifa letu.”
“Tunaendelea kuuenzi mchango wake kwa kudumisha amani, mshikamano na kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya maendeleo ya Zanzibar na taifa kwa ujumla. Mwenyezi Mungu amrehemu Hayati Sheikh Abeid Amani Karume na kumpa pepo ya milele.”
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdulla Asnuu Makame amesema Karume baada ya Mapinduzi alilenga kuleta maisha bora kwa watanzania.
Amesema viongozi wote waliofuata ni kupitia kwenye nyayo zake aktengeneza dhamira ya kuwa na umoja katika Jumuiya ya Afrika.
“Ili kuihuisha ndoto yake ni kuendeleza umoja wa Afrika aliutaka na tuwasihi wenzetu kupambani umoja wetu kama Afrika.
“Hawa walioko nje ya Afrika wanatuangalia kama Afrika, wakitaka kutunyonya watawesa kutunyonya tena, kwa hiyo lazima tukae kwa umoja na kimkakati kusonga mbele,” amesema
Naye Haji Hassan Haji, mkazi wa Jangombe, amesema ipo haja viongozi kufuata matakwa ya Karume kwani hakubagua mtu, alipenda kushirikisha wananchi hata kama ni wa hali ya chini na changamoto alizifanyia kazi bila kujali mtu yupo vipi.
“Karume alikuwa mtu wa watu alitatua changamoto za watu awe mkubwa kwa mdogo, alileta elimu bure, afya watu walitibiwa bure akawapa na wananchi makazi bure kwahiyo aliguswa na maisha ya wananchi wanyonge,” amesema.
Naye Balozi Ali Karume ambaye ni mtoto wa Karume, amesema muasisi huyo wa taifa ndio alileta uhuru wa kweli katika taifa la Zanzibar baada ya kupigana na walipata fursa ya kuchagua mkuu wa nchi na mkuu wa serikali kwa mara ya kwanza kwani kabla ya mapinduzi aliachiwa Sultan atawale.
“Mzee Karume alitusaidia sana kwamba tunakuwa na demokrasia mpya, unamchagua Rais wako ndio kiongozi mkuu na unachagua wabunge wawakilishi alieneza hilo” amesema.
Amesema Wazanzibari daima wataendelea kumkumbuka kuleta maendeleo ambayo viongozi waliofuatia licha ya kujitahidi kufanya lakini hawakufikia kiwango chake tena ikizingatiwa alitawala kwa kipindi cha miaka michache kuliko awamu zingine zote zilizofuatia.
Baadhi ya viongozi wengine wakuu waliohudhuria ni Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba, Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na viongozi wengine wa vyombo vya ulinzi na usalama wakiongozwa na Mkuu wa Jeshi la Ulinzi Generali Jacob Mkunda.

