MAZOEZI ya viungo, michezo na elimu ya afya vilitawala uzinduzi wa programu ya Wellness Day ya Benki ya CRDB, hatua inayolenga kuimarisha utimamu wa mwili na akili kwa wafanyakazi wake ili kuongeza ufanisi kazini.
Uzinduzi huo ulifanyika kwenye Uwanja wa Michezo Nyamagana jijini Mwanza, ambapo wafanyakazi walishiriki mazoezi mbalimbali ya mwili, michezo tofauti pamoja na vipimo vya afya, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo kuweka mizani kati ya kazi na maisha binafsi.
Kupitia Wellness Day ambayo imekuwa ikiadhimishwa tangu mwaka 2021, wafanyakazi hupata mafunzo na semina zinazohusu siha ya mwili, lishe bora na ustawi wa akili, mambo yanayochukuliwa kuwa msingi wa utendaji bora kazini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Kati wa benki hiyo, Bonaventure Paul, alisema afya njema ya mfanyakazi ina mchango mkubwa katika ubora wa huduma kwa wateja.
“Tunawajali sana wateja wetu, lakini hatuwezi kufanikisha hilo bila kuwa na wafanyakazi wenye afya bora. Kupitia Wellness Day, tunatoa fursa ya kufanya mazoezi, kupata ushauri wa lishe na kushughulikia changamoto za kiafya zinazoweza kupunguza ufanisi kazini,” alisema Bonaventure.
Aliongeza, programu hiyo itatekelezwa katika kanda zote nane za benki hiyo pamoja na matawi ya nje ya nchi ili kuhakikisha wafanyakazi wote wanapata fursa ya kushiriki na kunufaika na mpango huo.
Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Mahusiano Mahala pa Kazi wa benki hiyo, Timoth Fasha, alisema wataalamu wa afya wanaoshiriki katika programu hiyo hutoa elimu kuhusu umuhimu wa usingizi wa kutosha, mazoezi ya mwili, lishe bora na afya ya akili.
Alibainisha kuwa, kutokana na majukumu mengi ya kikazi, baadhi ya wafanyakazi hushindwa kupata muda wa kufanya mazoezi au kupumzika ipasavyo, hali inayoweza kusababisha msongo wa mawazo na kupungua kwa ufanisi.
Kupitia programu hiyo, wafanyakazi wanapata nafasi ya kushiriki michezo, kufanya mazoezi ya viungo na kukutana na madaktari pamoja na washauri nasaha wanaotoa elimu kuhusu afya ya akili, mahusiano, lishe na mtindo bora wa maisha.