Mtengwa aonyesha njaa ya mafanikio TRA United

BAADA ya beki wa kulia wa TRA United, Isaack Mtengwa kupewa dakika 80 za kucheza dhidi ya Singida Black Stars, amesema hiyo inazidi kumpa ukomavu.

Aprili 4, 2026, TRA United ikiwa nyumbani iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 ilipoikaribisha Singida Black Stars kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara na beki huyo alianza kikosi cha kwanza.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mtengwa alisema kupewa nafasi na Kocha Etienne Ndayiragije ni jambo kubwa kama kijana akiahidi kuipambania nafasi hiyo.

“Kwangu hii ni nafasi kubwa sana, kila ninapopewa dakika za kucheza najifunza zaidi na kunifanya nikue, namshukuru kocha Ndayiragije,” alisema Mtengwa na kuongeza.

“Nitaendelea kupambana ili kuhakikisha napata zaidi nafasi na kuisaidia timu kufikia malengo yake.”

Aliongeza bado ana malengo makubwa ndani ya timu hiyo, ikiwemo kuhakikisha anakuwa miongoni mwa wachezaji wanaoaminika zaidi na benchi la ufundi.

“Najua sio rahisi kwangu lakini ukomavu wa mechi ngumu kama hizo nikiendelea kupata nafasi ipo siku nitaaminika na benchi la ufundi.”

Mtengwa yupo TRA kwa mkopo akiwa ni mchezaji wa Yanga na amewahi kucheza kwa mkopo wa msimu mmoja Wakiso Giants ya Uganda.

Msimu huu akiwa TRA United, Mtengwa amecheza mechi nne dhidi ya Singida Black Stars kwa dakika (80), Dodoma Jiji (dakika 82), Simba (dakika 12) na moja ya Kombe la FA akicheza dakika 78 dhidi ya Rhino Rangers.

Nafasi anayocheza Mtengwa ndani ya TRA United yupo Mzambia, John Lazarus ambaye amekuwa akianza mara kwa mara kikosini hapo akicheza mechi 13 kati ya 17 ilizocheza timu hiyo iliyopo nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.