Droo FA Zanzibar yapangilia ratiba, mechi kuanza Aprili 13

BAADA ya Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), kufanya droo ya hatua ya 16 Bora ya Kombe la FA, imeweka wazi ratiba na Aprili 13 mwaka huu itaanza kwa kupigwa mechi mbili, huku ikitarajiwa kumalizika Aprili 16, 2026.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Aprili 13 mwaka huu, Kundemba itacheza dhidi ya Black Sailors kwenye Uwanja wa Mao A, huku Uhamiaji ikipambana dhidi ya Raskazone kwenye Uwanja wa Mao B.

Aprili 14, Inter Zanzibar itaumana na Mlandege kwenye Uwanja wa Mao A na New King itatoana jasho na bingwa mtetezi  KMKM kwenye Uwanja wa Mao B.

Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana kwenye mechi ya Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), KMKM ililala bao 1-0 mbele ya New King.  

Michezo miwili mingine itachezwa April 15, Mwembe Makumbi City itapambana na JKU kwenye Uwanja wa Mao A, huku Mafunzo na Polisi zikichuana kwenye Uwanja wa Mao B.

KVZ dhidi ya Zimamoto na Kipanga dhidi ya Malindi, zitakamilisha ratiba ya hatua hiyo Aprili 16 na mechi zote zitapigwa saa 10:00 jioni.

Mechi hizo zitachezwa kwa mfumo wa mtoano na hakutokuwa na muda wa nyongeza, endapo timu zitatoka sare kwenye dakika 90, mshindi atapatikana wa mikwaju ya penalti.