BANK OF AFRICA TANZANIA YATOA MSAADA KWA VITUO VYA WATOTO WANAOISHI MAZINGIRA MAGUMU

BANK of Africa Tanzania imeendelea kutekeleza sera yake ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwa kutoa kiasi cha shilingi milioni 24 kwa vituo vinne vinavyolea watoto wanaoishi katika mazingira magumu, ikiwa ni juhudi za kuboresha maisha yao hususan katika mahitaji ya chakula na elimu hapa nchini.

Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Nandi Mwiyombella, alisema vituo vilivyonufaika na msaada huo ni Amani Foundation for Orphanage Centre (Zanzibar), UMRA Orphanage Centre (Dar es Salaam), Kijiji cha Furaha (Dar es Salaam) na Kalamu Education Foundation (Dar es Salaam).

Alisema kiasi hicho cha fedha kimegawanywa sawa, ambapo kila kituo kitapata shilingi milioni 6 kwa ajili ya chakula na vifaa vya shule ili kusaidia watoto hao kuendelea na masomo yao.

“Hiki kiasi si kikubwa wala kidogo, bali ni sehemu ya sera ya kusaidia jamii. Tunataka kuhakikisha watoto wanaoishi katika mazingira magumu wanapata mahitaji muhimu ya msingi,” alisema Mwiyombella.

Aliongeza kuwa benki hiyo inatoa wito kwa taasisi nyingine za kifedha nchini kuona umuhimu wa kusaidia makundi maalum katika jamii kama njia ya kupunguza umasikini na kuwawezesha watoto ambao ni taifa la kesho.

“Dhamira yetu kama benki ni kuthamini ukuaji wa pamoja na utu wa mwanadamu. Kwa kutoa msaada huu, tunalenga kuunga mkono juhudi za vituo hivi katika kuwalea na kuwaendeleza watoto hawa,” alisisitiza.

Aidha, alifafanua kuwa kabla ya kutoa msaada wowote, benki hushirikiana na jamii husika, ikiwemo halmashauri na uongozi wa vituo, ili kubaini mahitaji halisi yanayohitaji kipaumbele.

Kwa upande wake, Meneja Mradi wa Kalamu Education Foundation (KEF), Dkt. Saidy Ally Soudy, aliishukuru benki hiyo kwa msaada wa fedha na chakula, akisema utasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha ustawi wa watoto wanaolelewa katika kituo hicho.

“Kituo chetu kinawasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kina dhamira ya kuwasaidia kufikia ndoto zao kielimu. Msaada huu wa vifaa na chakula ni muhimu sana,” alisema Dkt. Soudy.

Naye Msimamizi wa Kijiji cha Furaha, Martha Massawe, alisema lengo la kituo hicho ni kuwasaidia watoto kupata elimu ya msingi na sekondari, huku akitoa shukrani kwa msaada huo uliosaidia pia ujenzi na upanuzi wa kituo hicho kilichoanzishwa mwaka 2002 katika eneo la Mbweni, Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Katibu wa UMRA Orphanage Centre, Hamza Ahmed, alisema msaada huo ni muhimu katika kuwasaidia watoto kujiandaa kwa maisha ya baadaye na kujitegemea.

“Tunawapongeza Bank of Africa Tanzania kwa msaada huu adhimu. Ni mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya watoto wetu,” alisema Ahmed.

Akizungumza kwa niaba ya watoto wenzake, Zuwena Abbas Ali kutoka Amani Foundation alitoa shukrani kwa benki hiyo kwa msaada walioupata, akisema unawasaidia katika maisha yao ya kila siku na masomo.

Mpango huo unaashiria dhamira ya kudumu ya Bank of Africa Tanzania katika uwajibikaji kwa jamii, huku ukilenga kuboresha maisha ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika maeneo ya Zanzibar na Dar es Salaam.

Ikizingatiwa kuwa vituo vya malezi hukumbwa na changamoto za mara kwa mara katika upatikanaji wa chakula na mahitaji ya msingi, benki hiyo ilitoa msaada huo ili kusaidia uendeshaji wa vituo hivyo na kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana kwa watoto.

Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Bank of AfricaTanzania, Nandi Mwiyombella (kulia), alikabidhi nyaraka za mradi kwa Sister Martha Massawe, Msimamizi wa Kijiji cha Furaha kilichopo Mbweni, Dar es Salaam. Makabidhiano hayo yamefuatia mchango wa kifedha uliotolewa na Benki kusaidia ununuzi wa vifaa vya ujenzi kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mpya ya kituo hicho. 

Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki hiyo, Nandi Mwiyombella (katikati) akipeana mkono na Meneja wa Kalamu Education Foundation (KEF),Dkt. Saidy Ally Soudy, baada ya kukabidhi msaada wa vyakula.

Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bank of Africa Tanzania, Nandi Mwiyombella (kulia), akitoa msaada wa mtungi wa gesi na vyakula kwa Katibu wa Kituo cha Yatima cha Umrah, Hamza Ahmed (kushoto), katika hafla ya kuimalisha ushirikiano na jamii, Dar es Salaam juzi.

Wafanyakazi wa Bank of Africa Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja viongozi wa Taasisi ya KEF.