Dar es Salaam. Ili kuwafanya watoto wajiamini, wawe wadadisi wa mambo pamoja na kuwaandalia mazingira bora ya ajira baadaye, wazazi na walezi wametakiwa kuwekeza katika ujuzi mbalimbali walionao watoto hao.
Watoto wakiendelezwa kwenye maeneo kama sanaa ya muziki au michezo, watajenga kesho iliyo bora sambamba na kuwawekea msingi mzuri wanapokuwa darasani.
Akitoa rai hiyo Aprili 6, 2026 wakati wa tamasha la watoto wanaojifunza sanaa ya muziki mwanzilishi wa taasisi ya Koshumas ya ufundishaji wa vyombo vya muziki na uimbaji kwa watoto na vijana, Oscar Koshuma amesema elimu haiishii si tu darasani bali hata katika kuwekeza kwenye vipaji.
“Watoto na vijana wanavipawa mbalimbali vitakavyowawezesha kufanya mambo mengi ili kujiendeleza kadiri wanavyokua. Sasa hivi mtu akiwa na kipaji ni mtaji tosha kujiendeleza kwa kuwa kitampeleka mbali na asikae tu kuwaza kutegemea ajira,” amesema.
Koshuma amesema watoto hao wanaowafundisha kwa miezi mitatu sasa wameshaelewa kwa kuwa wanafanya hadi mitihani ya kutumia gitaa, kinanda, kuimba na vitu vyote vinavyohusiana na muziki.
Watoto wakionesha ujuzi wa sanaa ya muziki wanayoisoma katika taasisi ya Koshumas mbele ya wazazi wao Aprili 6, 2026 jijini Dar es Salaam.
“Watoto wanashika haraka sana masomo haya ukilinganisha na watu wazima. Kwa juma wanasoma mara mbili lakini wanaelewa na watafika mbali, kwani haiathiri masomo ya darasani,” amesema.
Amesema watoto wanavyofundishwa wanakuwa wanajiamini akitolea mfano kusimama mbele za watu kuimba au kupiga gitaa, hali hiyo inaweza kumsaidia hata katika mambo yake mengine.
Mzazi mmoja, Reen Mushi amesema mtoto wake anayejifunza kinanda imemsaidia kuweza kuwa mwangalifu hata katika mambo yake mengine ya shuleni na nyumbani.
“Wazazi wenye wasiwasi kwamba mtoto akifanya muziki au jambo lingine anaweza akakosa kufanya vizuri katika masomo ya darasani sio kweli kwani inamsaidia kuwa mzingatiaji,” amesema.
Mtoto Samwel Denis amesema kitendo cha yeye kujifunza ala za muziki kimemfanya kuwa na shauku ya kuzingatia mambo na umakini wa kujifunza zaidi.
“Sasa hivi najiamini, naweza kufanya jambo mbele za watu, pia, hata katika masomo ya hesabu naona inanisaidia kuwa makini,” amesema.
Mzazi mwingine, Joseph Sai amesema kama mzazi alitafakari baada ya shule, mtoto anaweza kufanya shughuli gani. Akaona amuangalie sehemu itakayomfanya ajifunze sanaa ya muziki anayoipenda hasa kupiga ngoma.
“Ameanza na miaka minne, sasa ana miaka 10, tunaamini itamsaidia hata katika maisha yake ya baadaye. Wazazi waamini katika Sanaa, pia, kama wanavyoamini katika maeneo mengine,” amesema.
Amesema sasa hivi kuna changamoto za ajira na watu wanaambiwa wajiajiri, kwa hiyo wazazi wasisite kuwatafutia watoto wao vitu vya ziada vya kujifunza na kujijenga.
Naye, mtoto wake, Aliera Sai amesema anapenda kujifunza vitu nje ya masomo ya darasani kwa kuwa vinamfanya awe mdadisi zaidi.