Na Janeth Raphael- MichuziTv -Dodoma
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, amesema kuwa changamoto ya kupanda kwa bei ya mafuta ni ya kidunia na si ya Tanzania pekee, hivyo haipaswi kuingizwa katika mjadala wa kisiasa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 7, 2026, katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi Kuu ya CCM jijini Dodoma, Kihongosi alisema nchi nyingi duniani, zikiwemo zile zenye uchumi mkubwa, zimeathirika na hali hiyo na zimepitia wakati mgumu kutokana na kupanda kwa bei za mafuta.
Alisisitiza kuwa katika kukabiliana na changamoto hiyo, ni muhimu kuwepo kwa ukweli na mshikamano wa kitaifa badala ya kubeba masuala ya kisiasa yanayoweza kupotosha wananchi.
Aidha, Kihongosi alimkosoa mmoja wa viongozi wa kisiasa kwa kutoa kauli kuhusu suala hilo bila kuwa na uelewa wa kutosha wa masuala ya uchumi. Alimtaka kujielimisha zaidi kabla ya kuzungumzia mambo nyeti yanayohusu maisha ya wananchi.
Katika hatua nyingine, alimzungumzia John Heche, akimtaka kutumia zaidi viongozi wenye uelewa wa masuala ya uchumi ndani ya chama chake, akiwemo Katibu Mwenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ili kuepuka upotoshaji wa taarifa kwa umma.
Kihongosi aliongeza kuwa Watanzania wanafahamu kuwa kupanda kwa bei ya mafuta ni changamoto ya kimataifa, na akasisitiza umuhimu wa nchi kuungana katika kutafuta suluhisho, kama ilivyofanyika wakati wa janga la COVID-19.
Alimalizia kwa kutoa wito wa kudumisha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi ili kuweza kukabiliana kwa pamoja na changamoto zinazolikabili taifa kwa sasa.
Kwa sasa, wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa kupanda kwa bei ya mafuta kunachangiwa na mambo mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya soko la kimataifa, migogoro ya kisiasa katika baadhi ya maeneo yanayozalisha mafuta, pamoja na ongezeko la mahitaji ya nishati duniani.
Hali hii imeendelea kuathiri gharama za maisha kwa wananchi katika nchi nyingi, ikiwemo Tanzania, hivyo kuhitaji mikakati madhubuti ya muda mfupi na mrefu ili kupunguza athari zake kwa uchumi wa taifa.

