Global Publishers
April 7, 2026
0 Comments
Chama cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kimeishauri serikali kuangalia uwezekano wa kutoa ruzuku kwa mafuta ili kupunguza makali ya gharama kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, wakati akizungumza na vyombo vya habari leo Aprili 7, 2026 jijini Dodoma.
Kihongosi amesema CCM, kama chama kinachosimamia serikali, kimeona umuhimu wa hatua hiyo ili kupunguza mzigo wa maisha kwa wananchi unaotokana na kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia.
Ameeleza kuwa mapendekezo hayo yanatokana na uzoefu wa mwaka 2022, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alichukua hatua ya kutoa ruzuku ya mafuta, jambo lililosaidia kudhibiti ongezeko la bei na kulinda uchumi wa wananchi kwa kiasi fulani.
“Tunashauri serikali iangalie namna bora ya kurejesha mfumo wa ruzuku ili kupunguza makali ya bei za mafuta, kwa kuzingatia hali ya sasa ya kiuchumi,” amesema Kihongosi.
Amesisitiza kuwa hatua hiyo inaweza kuwa moja ya njia muhimu za kukabiliana na changamoto za gharama za maisha, huku akibainisha kuwa CCM itaendelea kutoa ushauri kwa serikali kwa lengo la kuboresha ustawi wa wananchi.
Kauli hiyo inakuja wakati wananchi wengi wakikumbwa na ongezeko la gharama za maisha, hususan katika sekta ya usafiri na bidhaa zinazotegemea mafuta, hali inayochochea mjadala mpana kuhusu hatua za haraka za kupunguza athari hizo.