JUMATANO hii kuna mechi mbili za kuweka heshima katika Ligi Kuu Bara ambapo mapema saa 8:00 mchana, Singida Black Stars itaikaribisha KMC, kisha saa 10:15 jioni, Pamba Jiji dhidi ya Yanga.
Mechi ya pili ambayo vinara wa Ligi Kuu Bara na bingwa mtetezi wa ligi hiyo, Yanga itakuwa uwanjani CCM Kirumba jijini Mwanza kucheza dhidi ya Pamba Jiji ambayo imegoma kupoteza nyumbani msimu huu.
Mtanange huo unatarajiwa kuwa na upinzani mkali kutokana na aina ya matokeo ya Pamba Jiji msimu huu hasa inapokuwa nyumbani kufuatia kutopoteza mechi kama ilivyo kwa Yanga, Azam na Mashujaa, pia inachangiwa na unyonge wa wenyeji mbele ya Wanajangwani.
Yanga kwa sasa imeshusha presha baada ya kushinda mchezo uliopita ilipoichapa Tanzania Prisons mabao 3-0, ikitoka kuandamwa na sare tatu mfululizo zilizowatingisha mabingwa hao.
Yanga bado ipo juu ya msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiongoza kwa tofauti ya pointi sita ambapo kama itaibuka na ushindi dhidi ya Pamba Jiji, itazidi kujitanua kileleni ikiikimbia Simba iliyopo nafasi ya pili, lakini mabingwa hao wakiwa wamecheza mechi nyingi zaidi.
Historia inatukumbusha kwamba, Pamba Jiji haijawahi kuwa ngumu mbele ya Yanga tangu irejee Ligi Kuu ambapo imepoteza mechi zote tatu zilizopita ikifungwa jumla ya mabao 10-0.
Kwa msimu huu, timu hizo zilipokutana duru la kwanza, Yanga ikiwa nyumbani iliibuka na ushindi wa mabao 3-0, huku pia msimu uliopita zilipocheza CCM Kirumba, wenyeji Pamba Jiji walilala kwa mabao 3-0 na msimu huo ugenini ikafungwa tena 4-0.
Kibarua alichonacho Pamba Jiji si rahisi kwani inatambua kwamba Yanga haijapoteza mchezo wowote kwenye ligi msimu huu ikiungana na Azam kwenye rekodi hiyo, lakini pia imefunga mabao mengi zaidi yakiwa 35, huku ukuta wao ukiwa na ubora ukiruhusu matatu tu.
Yanga itaendelea kumkosa kipa wake namba moja, Djigui Diarra ambaye anatumikia adhabu ya kukosa mechi tatu lakini bado lango lao liko salama chini ya Aboutwalib Mshery ambaye hajaruhusu bao lolote msimu huu akiwa golini.
Habari njema kwa Yanga ni kwamba washambuliaji wake wawili, Prince Dube na Laurindo Aurelio ‘Depu’ wanaweza kurejea baada ya kuanza mazoezi na wenzao ambapo wawili hao ndio vinara wa ufungaji kikosini hapo kila mmoja akifunga mabao sita.
Pamba Jiji msimu huu katika uwanja wa nyumbani, imecheza mechi tisa na kushinda tano, huku nne ni sare zikiwamo mbili za mwisho dhidi ya Azam (2-2) na Simba (1-1), rekodi ambayo imeifanya kuwa tishio kwa wageni wao.
Pamba Jiji itawategemea mastaa wake wawili washambuliaji Mathew Tegis aliyefunga mabao manne akiwa ndiye mfungaji kinara kikosini hapo akifuatiwa na Peter Lwasa mwenye mabao matatu ambao watakuwa mbele ya ukuta wa Yanga kupambana kuupenya.
Kocha wa Pamba Jiji, Francis Baraza akizungumzia mchezo huo, alionyesha kujiamini kwa mastaa wake akisema wamekuwa wakimfanyia kazi yake kwa urahisi kutokana na uzoefu wao kwenye Ligi ya Tanzania na kwamba wanataka kushinda mechi hiyo.
“Ukiangalia kwenye ligi timu yetu ina wachezaji wazoefu wanaoijua Ligi ya Tanzania, najivunia sana ubora wao, wamekuwa wakinifanyia kazi yangu iwe rahisi, naamini tunakwenda kupata matokeo mazuri kesho (leo),” alisema kocha huyo.
Kwa upande wa Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves alisema mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na rekodi ya wapinzani wao wakiwa nyumbani lakini amefurahishwa na hali ya Uwanja wa CCM Kirumba akisema utawaruhusu kucheza soka safi.
“Tunakwenda kukutana na timu nzuri ambayo wote mmeona imekuwa ikifanya vizuri sana ikiwa nyumbani, lakini tuna timu nzuri ambayo tunataka kuendelea kushinda kwenye michezo yetu,” alisema.
Ukiachana na mchezo huo, kutakuwa na mechi nyingine ambapo zitakutana timu mbili ambazo zimetimua mabenchi yao ya ufundi.
Singida Black Stars ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Airtel mkoani Singida, itaikaribisha KMC ambazo timu zote mbili zimeachana na makocha wao baada ya kupoteza michezo ya mwisho ikiwa ugenini.
Singida itakuwa chini ya Muhibu Kanu ambaye ana taaluma ya ukocha, ina kazi ya kurudisha hali ya ushindi mbele ya waburuza mkia, KMC yenye hali mbaya zaidi kwani baada ya kucheza mechi 17, imekusanya pointi nane.
Kwa upande wa Singida, ina changamoto katika kikosi chake kwani licha ya kufunga mabao mengi, pia imeruhusu idadi sawa ambayo ni 19, kitu ambacho safu ya ulinzi ina kazi ya ziada ya kufanya kuhakikisha inalinda lango vizuri kwa lengo la kulinda pia ushindi.
Pointi 25 ilizonazo Singida katika mechi 17 ilizocheza, zinailazimu timu hiyo kushinda leo ili kujiimarisha zaidi kwani ikipoteza kuna hatari ya kuja kushushwa na TRA United yenye pointi 23 ikishinda kiporo chake.