Fahamu Wasifu wa Wajumbe wa Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uchaguzi

Mwenyekiti wa tume hiyo ni Mohamed Chande Othman.

Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Kabla na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 imeendelea kupewa muda zaidi ili kukamilisha kazi yake, baada ya kuomba nyongeza ya siku 21.

Hii ni nyongeza ya pili kufuatia ile ya awali ya siku 42, baada ya muda wa kwanza wa siku 90 kuisha. Kwa sasa, tume hiyo inatarajiwa kukamilisha kazi yake kabla ya Aprili 24, 2026.

Katika mjadala wa umma, wengi wamekuwa wakitaka kufahamu nani ni nani ndani ya tume hiyo yenye jukumu kubwa la kuchunguza tukio lililotikisa taifa.

Wajumbe wake wanatajwa kuwa watu wenye uzoefu mkubwa ndani na nje ya nchi katika nyanja za sheria, diplomasia, usalama na uongozi wa umma.

Mwenyekiti wa tume hiyo ni Mohamed Chande Othman, mwanasheria mwenye historia ndefu katika utumishi wa mahakama. Amewahi kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania (2010–2017), Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu. Pia amewahi kushiriki kazi za kimataifa kama mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa katika uchunguzi wa haki za binadamu nchini Lebanon na Sudan, pamoja na kushiriki katika tathmini na uboreshaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Mjumbe mwingine ni Stergomena Lawrence Tax, mwanadiplomasia na mtaalamu wa masuala ya utangamano wa kikanda. Ana uzoefu wa zaidi ya miaka 30 katika uongozi wa sera za amani, usalama, diplomasia na maendeleo ya kiuchumi, jambo linaloonekana kuongeza uzito wa kiufundi katika kazi ya tume.

Pia yumo Ibrahim Hamis Juma, ambaye aliwahi kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania kuanzia 2017 hadi 2025. Akiwa katika nafasi hiyo, alisimamia maboresho makubwa ya mfumo wa utoaji haki nchini na amewahi pia kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya sekta ya sheria, ikiwemo uenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria.

Katika kundi la wanadiplomasia wakongwe yumo Ombeni Yohana Sefue, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Tanzania, Balozi katika Umoja wa Mataifa, Marekani na Kanada, pamoja na kushiriki katika nyadhifa mbalimbali za ushauri wa viongozi wa kitaifa. Uzoefu wake wa utawala na uandishi wa sera unatajwa kuwa muhimu katika kazi ya uchunguzi na upatanishi.

Kwa upande wa usalama, yumo Said Ally Mwema, ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP). Akiwa kazini, alihusika na maboresho ya polisi jamii na mapambano dhidi ya uhalifu wa kimataifa, ugaidi na biashara haramu, pamoja na kushiriki katika shughuli za Interpol.

Mjumbe mwingine ni Paul Meela, Balozi na Luteni Jenerali mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Amewahi kushiriki katika operesheni za kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa, ikiwemo kuwa kamanda wa majeshi Darfur, Sudan, na kushiriki katika juhudi za upatanishi katika migogoro ya kikanda.

Pia yumo David Joseph Kapya, mwanadiplomasia mwenye uzoefu mkubwa katika usuluhishi wa migogoro barani Afrika, akihudumu katika timu mbalimbali za amani na diplomasia katika maeneo kama DRC, Sudan, Burundi na Zimbabwe, chini ya viongozi wa kitaifa na kikanda.

Katika tume hiyo pia yumo Radhia Naima Msuya, mwanadiplomasia mwandamizi aliyewahi kuwa Balozi katika nchi mbalimbali ikiwemo Afrika Kusini, Namibia, Botswana na Lesotho, pamoja na kuhudumu katika taasisi za kikanda kama SADC. Uzoefu wake wa kimataifa umetambuliwa hata kwa tuzo za kimataifa.

Mwisho ni George Madafa, afisa mwandamizi mstaafu wa diplomasia ambaye pia aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia.

Kwa ujumla, tume hii inaundwa na watu wenye taaluma na uzoefu mpana katika sheria, usalama, diplomasia na utawala wa umma. Watazamaji wengi wanaamini kuwa mchanganyiko huu wa wataalamu unaweza kusaidia kuhakikisha uchunguzi wa kina, wa haki na unaozingatia weledi, huku ukilenga kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha amani na utulivu wa taifa.