Mafuta yashuka bei soko la dunia

Washington. Masoko ya kimataifa yamepumua kwa afueni baada ya bei ya mafuta kushuka kwa kasi na hisa kupanda, kufuatia tangazo la kusitishwa kwa mapigano kwa masharti kati ya Marekani na Iran lililotolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump.

Katika hatua iliyokuja saa chache kabla ya muda wa mwisho wa mashambulizi ya kijeshi, Trump amekubali kuahirisha tishio lake la kuishambulia Iran, kwa masharti kwamba Tehran ikubali kusitisha mapigano kwa muda wa wiki mbili na kufungua njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani, ya mlango wa bahari wa Hormuz.

Athari za tangazo hilo zilionekana haraka katika masoko ya nishati, ambapo bei ya mafuta ghafi aina ya Brent, kipimo cha kimataifa, ilishuka kwa karibu asilimia 15 hadi kufikia dola  (Sh239,307) kutoka dola 114 (Sh293,346) kwa pipa.

Hatua hiyo ilifuatia ahadi ya Iran kuruhusu tena usafirishaji wa mafuta kupitia mlango wa Hormuz chini ya usimamizi wa jeshi lake.

Wakati huohuo, mafuta ghafi ya Marekani pia yalishuka kwa kiwango kikubwa, ishara kwamba wawekezaji walikuwa wakitarajia kurejea kwa mtiririko wa mafuta katika soko la dunia baada ya wiki kadhaa za taharuki.

Masoko ya hisa yaimarika duniani

Soko la hisa pia lilionyesha mwitikio chanya, huku masoko ya hisa ya Asia yakirekodi ongezeko kubwa.

Nchini Japan, soko la hisa la Nikkei 225 ilipanda kwa asilimia tano, huku Australia na Korea Kusini zikishuhudia ongezeko la zaidi ya asilimia mbili hadi karibu asilimia sita.

Masoko ya Hong Kong na China pia yalipanda, yakionyesha imani mpya ya wawekezaji.

Katika soko la dhamana, mavuno ya hati fungani za Marekani yalipungua, hali inayoashiria kupungua kwa hofu ya wawekezaji.

Katika hatua nyingine, bei ya dhahabu ilipanda kwa zaidi ya asilimia mbili, ikiendelea kubaki kuwa kimbilio la wawekezaji katika nyakati za sintofahamu.