Mauzo ya Tanzania nje yaongezeka, wachumi wakitoa tahadhari

Dar es Salaam. Wataalamu wa uchumi wamesema huenda mauzo ya Tanzania katika masoko ya nje yakaathirika katika siku za usoni ikiwa uchumi wa nchi wanunuzi utasinyaa.

Kusinyaa kwa uchumi wao kutapunguza uwezo wao wa kununua bidhaa za Tanzania, kushusha kiwango cha mahitaji au kubadili aina ya bidhaa wanazohitaji.

Haya yanasemwa wakati ambao Tanzania imerekodi ongezeko la mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi yaliongezeka kwa asilimia 12.4, kufikia Sh47.82 trilioni   katika mwaka unaoishia Februari 2026 kutoka Sh42.55 trilioni kipindi kama hicho mwaka 2025.

Ripoti ya Tathmini ya hali ya uchumi ya Machi iliyotolewa na Benki kuu ya Tanzania (BoT) inataja ukuaji huo kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na ongezeko la mapato yatokanayo na utalii, yakionesha utendaji mzuri katika akaunti ya huduma, sambamba na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi hususan dhahabu.

Mauzo ya bidhaa nje ya nchi yaliongezeka kwa asilimia 15 na kufikia Sh28.26 trilioni katika mwaka unaoishia Februari 2026, kutoka Sh24.57 trilioni katika kipindi kama hicho mwaka 2025.

Ukuaji huo uliongozwa na dhahabu, ambayo ilichangia takribani asilimia 45.7 ya jumla ya mauzo ya bidhaa nje ya nchi, bidhaa zilizoongezwa thamani viwandani na tumbaku.

Mauzo ya dhahabu yaliongezeka kwa asilimia 35.8 hadi Sh12.91 trilioni kutoka Sh9.513 trilioni yakichochewa na bei nzuri katika soko la dunia.

Vilevile, bidhaa za viwandani zilionyesha ukuaji wa asilimia 26.1 kufikia Sh4.43 trilioni kutoka Sh3.51 trilioni, hali iliyoashiria mwelekeo mzuri wa kuelekea uzalishaji wenye thamani zaidi na kupunguza utegemezi wa bidhaa ghafi.

Mauzo ya mazao ya asili yaliongezeka kwa asilimia 14.5 na kufikia Sh4.418 trilioni katika mwaka unaoishia Februari 2026, yakichochewa na tumbaku, kahawa na pamba kufuatia kuimarika kwa bei katika soko la dunia.

Kwa Februari 2026 pekee, mauzo ya bidhaa nje ya nchi yalifikia Sh2.509 bilioni, ikilinganishwa na Sh1.846 bilioni katika mwezi kama huo mwaka 2025, kutokana na utendaji mzuri wa dhahabu na bidhaa za viwandani.

Katika mwaka unaoishia Februari 2026, mapato ya huduma yaliendelea kuongezeka kwa asilimia 8.8 na kufikia Sh19.55 trilioni, kutoka Sh1797 trilioni katika kipindi kama hicho mwaka 2025.

Ukuaji huu ulichangiwa zaidi na mapato ya utalii, yaliyoongezeka kufuatia idadi ya watalii wa kimataifa kuongezeka kwa asilimia 4.2 na kufikia wageni 2,255,006.

Akizungumzia suala hili, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha Iringa, Dk Isidori Minani anasema ongezeko hilo linashuhudiwa sasa kwa sababu biashara ilifanyika kabla ya machafuko hivyo si rahisi athari zake kuonekana katika ripoti hiyo.

“Lakini pia tutaathirika kwa kutegemea nini tunauza kwani tunapozalisha bidhaa gharama zake zinaweza kuongezeka, kama tunaagiza malighafi tutapata kwa gharama kubwa na kuzalisha kwa gharama kubwa hali itakayofanya tusizalishe kwa kiwango kikubwa hivyo bidhaa za kuuza nje zitapungua,” anasema.

Anasema kutokana hali hiyo kama kitu kilikuwa Sh2 milioni kitakuwa Sh2.5 milioni na kwa sababu kanuni ya biashara hutegemea mahitaji na usambazaji bei ikiwa kubwa uhitaji utapungua hasa uchumi wa nchi hizo ukiwa umesinyaa.

“Na hili linaweza kutugusa wote kwani fedha za nchi nyingi zinaweza kupoteza nguvu dhidi ya fedha za kigeni kwa sababu ya mfumuko wa bei, bei mafuta ikipanda maana yake bidhaa karibu zote zitapanda bei kwani zinahitaji kusafirishwa na nyingine zinatengenezwa kwa kutumia mafuta,” anasema.

Anasema bidhaa ikiongezeka bei kama wanaouza rejareja watanunua kwa bei kubwa na wao watauza kwa bei kubwa hali itakayofanya mfumuko wa bei kutokea.

“Ukitokea tatizo moja wapo ni kunyong’onyeza nguvu ya fedha ya ndani. Bahati mbaya kushuka kwa thamani ya fedha kwa nchi nyingi za Afrika zinaweza kupoteza nguvu kwa fedha za kigeni hali hii itaathiri mauzo ya nje, kwani watakaouziwa watakuwa wamepoteza uwezo wa kununua na tutauza kwa bei ndogo,” anasema.

Anasema moja ya jambo linaloweza kufanyika ili kupunguza makali haya ni serikali kuingilia kati kwa kuhakikisha inatoa ruzuku kwenye mafuta au kuondoa baadhi ya kodi ili mafuta yakipanda bei isiwe kwa kiwango kikubwa.

“Mafuta yakipanda bei kwa kiasi kikubwa itaathiri uzalishaji, mauzo, bei za bidhaa, thamani ya fedha na hata uwezo wa nchi kununua vitu nje utapungua kwani utahitaji fedha nyingi zaidi kupata kitu kimoja,” anasema na kuongeza.

“Kuongeza uzalishaji ingesaidia lakini si suala la muda mfupi ambalo matokeo yake yanaweza yasiwe chanya sana japokuwa ingekuwa njia nyingine ya kupunguza mfumuko wa bei.”

Kuhusu suala la mfumuko wa bei alilolizungumzia Dk Minani, BoT ilifafanua kuwa unatarajiwa kubaki ndani ya wigo wa asilimia 3 hadi 5 katika robo ya pili ya mwaka 2026 licha ya shinikizo linalotokana na kupanda kwa gharama za bidhaa za mafuta katika soko la dunia.

Hayo yalisema Aprili 2, 2026 na Naibu Gavana wa BoT anayeshughulikia Sera za Uchumi na Fedha, Dk Yamungu Kayandabila alipokuwa akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) baada ya kikao chake cha hivi karibuni.

Alisema ongezeko la gharama za nishati na usafirishaji linaendelea kuwa chanzo kikuu cha shinikizo la mfumuko wa bei, likichochewa na kupanda kwa bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia iliyotoka dola za Marekani 60 kwa pipa katika robo ya kwanza ya mwaka 2026 hadi zaidi ya dola 100 kwa pipa.

Alifafanua kuwa licha ya hali hiyo, mfumuko wa bei uliendelea kubaki katika kiwango cha chini ukiwa wastani wa asilimia 3.3 kwa Tanzania Bara katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, huku ukitarajiwa kuendelea kudhibitiwa ndani ya malengo yaliyowekwa.

“MPC inatarajia mfumuko wa bei kubaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5 katika robo ya pili ya mwaka 2026, bei nafuu za chakula pamoja na uthabiti wa thamani ya shilingi vinasaidia kupunguza kasi ya ongezeko la mfumuko wa bei,” alisema.

Akifafanua kwa nini mauzo ya Tanzania yanaweza yasiathiriwe sana na machafuko haya, mchambuzi wa Uchumi, Oscar Mkude anasema Tanzania haiuzi sana katika nchi zenye shida huku akitolea mfano wa dhahabu mnunuzi mkubwa kuwa Afrika Kusini na tumbaku kwenye nchi za Asia.

Anasema pia Tanzania inauza sana katika nchi nyingine za Afrika na China.

“Hatuna athari kubwa sana kutokana na vita, athari inaweza kuonekana kwa kushindwa kuuza kwa kiwango kikubwa ikiwa masoko yetu yataathirika kwa uchumi wao kusinyaa, hii itafanya mahitaji yao kupungua, kiwango kitakachokuwa kinahitajika hakitakuwa sawa na kilichokuwapo awali,” anasema.

Anasema changamoto nyingine inayoweza kuonekana ni kubadilika kwa wasambazaji kwani nchi hizo zinaweza kutafuta wazalishaji wengine hali inayoweza kuongeza ushindani kwa Tanzania.

“Katika bidhaa tunazouza sana soko linatabirika, tumbaku soko lake ni Asia na dhahabu ni Afrika Kusini labda bidhaa zile nyingine ndiyo zinaweza kuathiriwa kwa muda hasa kutokana na kuguswa kwa mnyororo wake wa uzalishaji,” anasema.

Kwa upande mwingine, katika mwaka unaoishia Februari 2026, uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje uliongezeka na kufikia Sh48.44 trilioni kutoka Sh44.41 trilioni mwaka 2025. Ongezeko hilo lilichangiwa hasa na mahitaji makubwa ya pembejeo za uzalishaji kama vile malighafi za viwandani, vifaa vya usafiri, mashine na huduma za usafirishaji.

Hata hivyo, uagizaji wa mafuta, uliokuwa unachangia asilimia 13.8 ya jumla ya uagizaji, ulipungua kwa asilimia 16.6 na kufikia Sh5.486 trilioni kutoka Sh6.577 trilioni, hali iliyotokana na kushuka kwa bei katika soko la dunia.