Mapendekezo ya wanazuoni wa Kiislamu makali ya mafuta

Dar es Salaam. Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, wamependekeza Serikali ipunguze au kuondoa baadhi ya kodi na tozo katika nishati ya mafuta, ili kunusuru uchumi wa wananchi dhidi ya makali ya mfumuko wa bei unaochochewa na migogoro ya Mashariki ya Kati.

Mengine yaliyopendekezwa na jumuiya hiyo ni Serikali kuangalia upya bei za pembejeo za kilimo hususan mbolea, na inapowezekana kuanzisha au kuimarisha mfumo wa ruzuku, ili kupunguza gharama kwa wakulima na kudhibiti kupanda kwa bei za bidhaa sokoni.

Mapendekezo ya wanazuoni hao, yanakuja wakati ambao dunia inakabiliwa na ongezeko la bei ya mafuta kutokana na vita vya Marekani, Israel dhidi ya Iran, hali iliyosababisha uharibifu wa miundombinu ya uzalishaji mafuta na kuathiri bei ya nishati hiyo.

Hata hivyo, tayari Serikali imesema itachukua kila hatua za kubana matumizi katika wakati huu ambao bei za mafuta zimepanda maradufu, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kupunguza athari za hali hiyo kwa uchumi wa Taifa na wananchi wake.

Wanazuoni hao wametoa mapendekezo hayo jana, Jumanne Aprili 7, 2026 kupitia tamko waliloliita Haki, Ubinadamu na Wajibu Wetu katika Nyakati za Migogoro ya Dunia, lililotiwa saini na Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Sheikh Abdallah Ndauga.

Kupitia tamko hilo, Sheikh Ndauga amependekeza kwa Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza au kuondoa baadhi ya kodi na tozo zinazoathiri gharama za mafuta, kama ilivyofanywa na mataifa mengine.

“Kuangalia kwa makini bei ya mbolea na pembejeo za kilimo, na pale inapowezekana, kuanzisha au kuimarisha mfumo wa ruzuku,” amesema.

Amesema migogoro ya kimataifa haiishii kwenye ramani za kisiasa pekee bali huingia moja kwa moja katika maisha ya wananchi wa kawaida, kwa kuathiri uchumi, ustawi wa jamii na utulivu wa mataifa.

Amesema kupanda kwa bei ya mafuta kunasababisha mnyororo mpana wa athari unaogusa sekta zote, kuanzia usafirishaji, uzalishaji hadi bei za vyakula na huduma muhimu.

Aidha, amesisitiza katika hali hiyo, kuna haja ya kuweka mbele thamani ya maisha ya binadamu kuliko maslahi ya kisiasa au kiuchumi.

“Mara nyingi waathirika wakubwa wa migogoro ni raia wasiokuwa na hatia, wakiwemo wanawake, watoto na wazee. Kwa mtazamo huo, wito wetu ni kuendelezwa kwa misingi ya haki na ubinadamu bila upendeleo, wakipinga aina yoyote ya dhulma,” amesema.

Pia, ameonya kuhusu hatari ya migogoro ya kimataifa kuhamia ndani ya jamii kupitia mgawanyiko wa kidini, kikabila au kiitikadi, hali ambayo inaweza kuhatarisha mshikamano wa kitaifa.

Amesisitiza umuhimu wa tahadhari za mapema ili kuzuia athari hizo zisijitokeze nchini.

Amevihimiza vyombo vya habari kutimiza wajibu wa kutoa taarifa kwa uangalifu, vitumie lugha inayojenga uelewa badala ya kuchochea hofu au migawanyiko.

“Katika nyakati za changamoto, taarifa sahihi zinaweza kuwa chombo cha amani na utulivu badala ya chanzo cha taharuki,” amesema.

Ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kudumisha mshikamano, uvumilivu na maadili ya kitaifa, wakisisitiza kuwa nguvu ya Taifa ipo si tu katika sera na uchumi, bali pia katika umoja na mshikamano wa wananchi wake katika kukabiliana na changamoto za kimataifa.

Msimamo wa jumuiya hiyo, ameeleza ni kuhakikisha kunakuwepo amani, umoja, uvumilivu na kuheshimiana na kwamba wananchi wasiruhusu fitina za nje kuleta mgawanyiko, propaganda kuvuruga mshikamano, au migogoro ya wenyewe kwa wenyewe.