Na Mwandishi Wetu.
MSIMAMIZI wa Bohari ya kuhifadhia Mafuta (DEPOT)ya MOIL ENERGIES Dkt. Sajad Habib Rai ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) kwa kuanzisha utaratibu wa kufanya kazi kwa Saa 24 katika maeneo ya bohari kwa lengo la kusaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wao huduma.
Aidha akizungumzia kuhusu upatikanaji wa mafuta katika Bohari hiyo, Dkt Sajad ambaye pia ni Meneja Mkuu wa Mansoor Industries, amesema wao kama MOIL ENERGIES wana akiba ya kutosha huku wakisubiri Meli zingine ambazo tayari zimetia nanga zishushe nishati hiyo
Akizungumza siku chache mara baada ya Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Juma Mwenda kutembelea ‘Depot’ hiyo iliyopo eneo la Kigamboni Jijini Dar es Salaam, Sajad ambaye ni Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo alisema kupitia utaratibu huo kwao ni fahari kwa kuwa unarahisisha kazi.
Amesema kutokana na kuongezwa huko kwa muda kwa watumishi wa TRA kuwepo katika maeneo ya kazi kama ambavyo Kamishna Mwenda amesema, shughuli zao zinakwenda kuongezeka ufanisi jambo analosema wamelipokea kwa mikono miwili.
“Kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Kamishina Mwenda kwa utendaji wake wa kazi, kwa sasa TRA imekuwa ikitupa ushirikiano mkubwa wafanyabiashara, kila siku tunaona hatua zaidi na zaidi hili kwetu linatusaidia kufanya kazi Kwa ufasaha” amesema Dkt Sajad
Aidha kuhusu utaratibu mpya wa uuzaji mafuta ya Dizel na Petroli uliowekwa hivi karibuni na TRA , amesema wao kama wafanyabiashara hawana shaka nao kwa kuwa umesaidia kuondoa changamoto ya uchepushaji mafuta na kuhakikisha kila mzigo unaotoka kwenye vituo hivyo unakwenda mahala ulipokusudiwa.
Awali akizungumza wakati wa ziara ya baada ya kutembelea Bohari hiyo na zingine za Uhifadhi wa Mafuta, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Mwenda amesema Mamlaka hiyo imejipanga kutoa huduma kwa Saa 24 katika Bohari za mafuta(Depot) huku akisisitiza uwepo wa udhibiti katika udanyanyifu kutoka kwa watoa huduma hiyo.
“Kama ambavyo Serikali imesema kuwa hakuna upungufu wa mafuta, TRA pia tunasisitiza kuna mafuta ya kutosha nchini kwa zaidi tunawaomba watoa kuzingatia taratibu za uuzaji wa mafuta hayo” amesema Mwenda
Aidha amewataka wauzaji wa mafuta hayo kuhakikisha wanashirikiana na Mamlaka hiyo ili kuwezesha huduma hiyo kutolewa kwa Saa 24 ili kurahisisha kazi ya usambazaji wa mafuta hayo.

