Dar es Salaam. Kitendo cha Marekani na Iran kukubaliana kusitisha mapigano kwa muda wa wiki mbili kimeibua matumaini mapya, kikichochea kushuka kwa bei za mafuta duniani na kupunguza mvutano uliokuwa ukitishia kuzua vita kubwa Mashariki ya Kati.
Makubaliano hayo yaliyofikiwa Jumanne jioni yanajumuisha kufunguliwa kwa muda kwa njia muhimu ya usafirishaji wa nishati duniani, mlango wa bahari wa Hormuz, kufuatia juhudi za dakika za mwisho za kidiplomasia zilizoongozwa na Pakistan.
Tangazo hilo lilitolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump, chini ya saa mbili kabla ya muda wake wa mwisho wa saa 8:00 usiku (kwa saa za Mashariki ya Kati) wa kuanzisha mashambulizi dhidi ya miundombinu muhimu ya Iran, ikiwemo mitambo ya umeme na madaraja.
Awali, hali ilikuwa tete baada ya Trump kuandika katika mtandao wa Truth Social akionya kuwa “ustaarabu mzima ungeweza kutoweka usiku huo,” huku ndege za kivita za Marekani aina ya B-52 zikiripotiwa kuwa njiani kuelekea Iran kabla ya uamuzi wa kusitisha mashambulizi kutangazwa.
Mabadiliko hayo yalitokana na juhudi za Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, ambaye aliomba kusitishwa kwa mapigano kwa muda ili kutoa nafasi kwa mazungumzo ya kidiplomasia.
Kwa mujibu wa Trump, kusitishwa kwa mashambulizi kunategemea Iran kukubali kufungua kikamilifu na kwa usalama mlango wa Hormuz.
Baadaye, aliita siku hiyo “hatua kubwa kwa amani ya dunia,” akidai kuwa Iran imeanza kulegeza msimamo wake.
Hata hivyo, Iran, kupitia waziri wake wa mambo ya nje, Abbas Araghchi, ilithibitisha kukubaliana na makubaliano hayo, ikisema kuwa usafiri salama katika mlango huo utaratibiwa na vikosi vyake vya kijeshi kwa kipindi chote cha wiki mbili.
Israel yaunga mkono kwa tahadhari
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema nchi yake inaunga mkono makubaliano hayo, lakini akabainisha kuwa hayahusishi operesheni dhidi ya kundi la Hezbollah nchini Lebanon.
Hata hivyo, bado kuna mkanganyiko kuhusu upeo wa makubaliano hayo, baada ya Iran kutoa matoleo mawili tofauti ya mpango wa vipengele 10 unaotarajiwa kuwa msingi wa mazungumzo.
Tofauti hiyo imeibua maswali kuhusu msimamo halisi wa Tehran, hususan kuhusu mpango wake wa nyuklia.
Pakistan imealika pande zote mbili kufanya mazungumzo jijini Islamabad Ijumaa hii. Iran tayari imethibitisha kushiriki, huku Marekani ikiwa bado haijatoa msimamo wake rasmi.
Katika kipindi hicho cha wiki mbili, Trump amesema anaamini mazungumzo yanaweza kufanikisha makubaliano ya kudumu ya amani, akisisitiza kuwa pande zote zimepiga hatua kuelekea suluhu ya muda mrefu.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, amesema makubaliano hayo ni “nafasi muhimu ya kupumua” kwa dunia, huku akisisitiza umuhimu wa kuyageuza kuwa suluhisho la kudumu.
Mafuta yashuka, masoko yaimarika
Athari za tangazo hilo zilionekana haraka katika masoko ya nishati, ambapo bei ya mafuta ghafi aina ya Brent, kipimo cha kimataifa, ilishuka kwa karibu asilimia 15 hadi kufikia dola 93 (Sh239,307) kutoka dola 114 (Sh293,346) kwa pipa.
Hatua hiyo ilifuatia ahadi ya Iran kuruhusu tena usafirishaji wa mafuta kupitia mlango wa Hormuz chini ya usimamizi wa jeshi lake.
Wakati huo huo, mafuta ghafi ya Marekani pia yalishuka kwa kiwango kikubwa, ishara kwamba wawekezaji walikuwa wakitarajia kurejea kwa mtiririko wa mafuta katika soko la dunia baada ya wiki kadhaa za taharuki.
Soko la hisa pia lilionyesha mwitikio chanya, huku masoko ya hisa ya Asia yakirekodi ongezeko kubwa.
Nchini Japan, soko la hisa la Nikkei 225 ilipanda kwa asilimia tano, huku Australia na Korea Kusini zikishuhudia ongezeko la zaidi ya asilimia mbili hadi karibu asilimia sita.
Masoko ya Hong Kong na China pia yalipanda, yakionyesha imani mpya ya wawekezaji.
Katika soko la dhamana, mavuno ya hati fungani za Marekani yalipungua, hali inayoashiria kupungua kwa hofu ya wawekezaji.
Wakati huo huo, bei ya dhahabu ilipanda kwa zaidi ya asilimia mbili, ikiendelea kubaki kuwa kimbilio la wawekezaji katika nyakati za sintofahamu.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limefanya mkutano wa dharura ambapo mataifa ya Russia na China yalipinga azimio lililolenga kufungua tena mlango wa Hormuz.
Katika kikao kilichofanyika Jumanne, Aprili 7, 2026, azimio hilo lililowasilishwa na Bahrain, ambaye pia ni rais wa sasa wa Baraza hilo, lilishindwa kupitishwa licha ya kuungwa mkono na mataifa 11 kati ya 15 wanachama wa Baraza la Usalama.
Mataifa yaliyounga mkono ni pamoja na Marekani, Uingereza na Ufaransa. Hata hivyo, kura za turufu za Russia na China zilitosha kulizuia azimio hilo, huku Pakistan na Colombia zikijizuia kupiga kura.
Awali, rasimu ya azimio hilo ilipendekeza matumizi ya “njia zote muhimu,” ikiwemo nguvu za kijeshi, ili kuhakikisha uhuru wa usafiri katika Mlango wa Hormuz.
Hata hivyo, ili kuepuka pingamizi, maandishi yalirekebishwa na kupunguza makali yake, yakiruhusu tu “njia za kujilinda” na “juhudi za pamoja za kujihami.”
Pamoja na mabadiliko hayo, Russia na China zilibaki na msimamo mkali.
Balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa, Vasily Nebenzya, alikosoa azimio hilo akilitaja kuwa “lenye upendeleo,” akidai halikutaja mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran kama chanzo cha mgogoro wa sasa.
Kwa upande wake, China ilieleza wasiwasi kuwa azimio hilo lingeweza kutumiwa kama mwamvuli wa kisheria kuhalalisha mashambulizi zaidi ya kijeshi katika eneo hilo, hivyo kuhatarisha uhuru wa mataifa.
Aidha, Russia ilisisitiza kuwa mgogoro huo ulianza kushika kasi baada ya operesheni ya kijeshi iliyoanzishwa mwishoni mwa Februari, na kwamba azimio lolote lilipaswa pia kulaani hatua hizo za awali.
Awali, kauli ya Trump ya kuanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya miundombinu ya Iran, ikiwemo mitambo ya umeme na madaraja, ilielezwa na wataalamu wa sheria za kimataifa kwamba ingechukuliwa kama uhalifu wa kivita.
Hata hivyo, katika mabadiliko ya ghafla, Trump alitangaza kupitia mitandao ya kijamii kuwa amekubali kusitisha mashambulizi hayo kwa masharti kwamba Iran ifungue “kwa ukamilifu, mara moja na kwa usalama” njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani ya mlango wa bahari wa Hormuz.
Hii si mara ya kwanza kwa Trump kubadili msimamo kuhusu vitisho kwa Iran, Machi 21, alitishia “kushambulia na kuangamiza” vituo vya umeme vya Iran endapo mlango Hormuz usingefunguliwa ndani ya saa 48.
Siku chache baadaye, Machi 26, aliongeza muda kwa siku 10 akitaka hatua za haraka zichukuliwe kufungua tena njia hiyo ya kimkakati.
Kadri mvutano ulivyozidi kuongezeka mwishoni mwa Machi na mwanzoni mwa Aprili, Trump aliongeza ukali wa matamshi yake, akiahidi “kuangamiza kabisa” kituo kikuu cha mauzo ya nje ya mafuta cha Iran katika Kisiwa cha Kharg iwapo makubaliano ya amani yasingefikiwa.
Hata hivyo, kati ya Aprili 5 na 6, alionyesha dalili za kulegeza msimamo kwa muda, akitangaza kusitisha kwa siku 10 mashambulizi yaliyokuwa yakilenga miundombinu ya nishati hadi Aprili 6, 2026, akieleza kuwa kulikuwa na maendeleo katika mazungumzo yanayoendelea.
Katika hatua iliyoongeza mvutano, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) lilitangaza kuwa iwapo Marekani itavuka “mstari mwekundu,” majibu yake hayatabaki ndani ya mipaka ya kanda hiyo.
Kauli hiyo iliungwa mkono na viongozi wa Iran, huku ripoti zikieleza kuwa hadi watu milioni 14 wamejitolea “kujitoa mhanga” kulinda taifa lao.
Raia hao wameunda ngome za kibinadamu kulinda miundombinu muhimu kama mitambo ya umeme, hatua inayoonyesha jinsi hali ilivyo tete ndani ya nchi hiyo.
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amenukuliwa akisisitiza kuwa taifa hilo liko tayari kulinda mamlaka yake kwa gharama yoyote.
Kumuondoa Trump madarakani
Wimbi la wito wa kumuondoa madarakani Rais wa Marekani, Donald Trump, linaendelea kushika kasi baada ya kauli zake za hivi karibuni kutishia kushambulia Iran, hatua ambayo baadhi ya wabunge wa chama cha Democratic wanasema inaweza kuingia katika makosa ya kivita.
Mwakilishi wa Colorado, Diana DeGette, ameongoza wito huo akitaka Bunge la Marekani kuanza mchakato wa kumuondoa madarakani Rais huyo (impeachment), endapo Baraza la Mawaziri halitachukua hatua ya kumwondoa kupitia Marekebisho ya 25 ya Katiba ya Marekani.
DeGette alisema kauli za Trump, zikiwemo onyo kwamba “ustaarabu mzima unaweza kutoweka kwa usiku mmoja,” zinaashiria tishio la wazi la uhalifu wa kivita dhidi ya raia wa Iran.
Mwakilishi mwingine wa Democratic kutoka Colorado, Brittany Pettersen, alieleza kushtushwa na kauli hizo, akisema haiwezekani kwa Rais wa Marekani kutishia kuangamiza ustaarabu mzima. Kupitia msemaji wake, alithibitisha kuwa yuko tayari kuunga mkono hatua ya kumuondoa Trump madarakani.
Kwa upande wake, Jason Crow, alisisitiza kuwa wanajeshi wa Marekani wana wajibu wa kisheria kufuata amri halali pekee, akionya kuwa Rais anaweza kuwaweka katika mazingira magumu ya kuchagua kati ya kufuata amri zisizo halali au kuhatarisha taaluma zao.
“Rais anahatarisha usalama wa Wamarekani, wanajeshi wetu, washirika wetu na raia wasio na hatia,” alisema Crow, akiongeza kuwa hatua mbalimbali ikiwemo impeachment zinapaswa kuzingatiwa ili kudhibiti mamlaka ya rais.
Seneta wa Colorado, Michael Bennet, naye alimkosoa Trump akisema anachochea hali hatarishi ili kushughulikia mgogoro aliouchochea mwenyewe, akidai vita dhidi ya Iran vilianzishwa bila mkakati madhubuti.
