Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetangaza rasmi kuwa mchezo namba saba (7) wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/2026 kati ya TRA United FC na Simba SC utafanyika Aprili 9, 2026 katika Sheikh Amri Abeid Stadium, kuanzia saa 10:00 alasiri.
Mchezo huo ulikuwa uchezwe Machi 14, 2026 lakini uliahirishwa kufuatia mvua kubwa iliyonyesha jijini Arusha na kusababisha uwanja huo kushindwa kukidhi vigezo vya kisheria kwa mchezo kuchezwa.
Katika taarifa hiyo, TPLB imefafanua kuwa mashabiki wote waliokuwa wamenunua tiketi kwa ajili ya mchezo uliopangwa awali hawatapaswa kununua tiketi mpya. Tiketi hizo tayari zimerejeshwa kwenye kadi zao za N-CARD, na mashabiki hao watatakiwa kuwasilisha kadi hizo getini kwa ajili ya uhakiki siku ya mchezo.
Kwa mujibu wa bodi hiyo, tiketi zilizokuwa zimeuzwa kabla ya kuahirishwa kwa mchezo huo zilikuwa ni 95 za VVIP, 567 za VIP, na 3,215 za mzunguko.
Aidha, mashabiki ambao hawakupata nafasi ya kununua tiketi hapo awali wametakiwa kununua tiketi kupitia vituo rasmi vya N-CARD au mitandao ya simu. Bei za tiketi zimetajwa kuwa shilingi 50,000 kwa VVIP, shilingi 30,000 kwa VIP (Wing A na B), na shilingi 10,000 kwa mzunguko.
TPLB imehitimisha kwa kuwashukuru mashabiki wa soka nchini kwa ushirikiano wao mkubwa, ikiwemo kujitokeza kwa wingi viwanjani na kuendelea kuziunga mkono klabu zao.