Singida Black Stars yatafuta kocha mpya DR Congo

SINGIDA Black Stars imehamishia rada zake DR Congo katika harakati za kumsaka kocha mpya wa kukinoa kikosi hicho, huku ikianza na jina la Papi Kimoto wa Union Maniema kabla ya kuelekeza nguvu kwa Guy Bukasa wa FC Saint Eloi Lupopo.

Taarifa kutoka ndani ya mabosi wa juu wa Singida zinaeleza kuwa, awali walikuwa wakimfuatilia Kimoto kwa muda mrefu wakivutiwa na uwezo wake, lakini mazungumzo yao yaligonga mwamba kutokana na kutofautiana katika baadhi ya vipengele vya kimkataba.

Klabu hiyo inasaka kocha mpya kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo kufuatia matokeo yasiyoridhisha katika kipindi cha hivi karibuni ambapo Aprili 5 mwaka huu ulitangaza kulivunja benchi la ufundi muda mchache baada ya kupoteza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya TRA United kwa mabao 2-0.

Mwanaspoti ilimpata mmoja wa viongozi wa Singida ambapo alisema: “Tunadhani Congo Kuna makocha wazuri, Kimoto tulikuwa tunamuangalia kwa muda mrefu lakini kwenye mazungumzo tumeshindwa kukubaliana, kuna mambo ambayo tumeona tuheshimu uamuzi wake.

“Kwa sasa tunaendelea kupambana na Bukasa, ni kocha mzuri na kijana, kama ulivyoona msimu huu alivyoiimarisha Lupopo na inacheza mpira mzuri.

“Bado hatujakubaliana ingawa yupo tayari kuja, anataka aje mwisho wa msimu lakini sisi tulikuwa tunapendekeza aje sasa ili aisome timu na afanye usajili kuelekea msimu ujao.

“Anataka pia aje na benchi lake zima, sasa mapendekezo ya wakubwa wa juu ni kwamba tuchanganye, baadhi aje nao na wengine watoke hapa, kwa hiyo mazungumzo bado yanaendelea kati yetu na Bukasa.” alisema Kiongozi huyo.

Bado Singida haijatangaza benchi lake la mpito huku Leo ikijiandaa na mechi dhidi ya KMC utakaochezwa katika uwanja Airtel ulioko Singida Majira ya Saa 10:00 Jioni.