WPL mzunguko wa 13 mechi sita kupigwa leo

APRILI 8, 2026, mzunguko wa 13 wa Ligi Kuu Soka Wanawake Tanzania Bara (WPL) utaendelea kwa mechi sita zitakazopigwa zikitarajiwa kuwa na ushindani wa aina yake kutokana na timu zinazowania nafasi ya ubingwa na zile zinazopambana kujinasua mkiani.

Yanga Princess iliyopo nafasi ya pili na pointi 33, itashuka dimbani kusaka pointi tatu dhidi ya Tausi FC iliyopo nafasi ya saba, Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Nyamagana jijini Mwanza, Bilo Queens iliyopo mkiani na pointi nne, itaikaribisha JKT Queens iliyopo nafasi ya tatu na pointi 29 katika mechi inayotarajiwa kuwa na ushindani mkali. JKT Queens inaingia ikiwa na uzoefu mkubwa, huku wenyeji wakisaka ushindi.

Fountain Gate itakipiga dhidi ya Geita Queens iliyopo nafasi ya 10 Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara, huku Mashujaa Queens dhidi ya Ruangwa Queens itachezwa Uwanja wa TFF Kigamboni, Dar es Salaam.

Mechi nyingine ya kukata na shoka ni kati ya Ceasiaa Queens na itakuwa nyumbani kuikaribisha Alliance Girls kwenye Uwanja wa Samora, Iringa. Bunda Queens watakipiga dhidi ya Simba Queens iliyopo kileleni na pointi 34.

Akizungumzia mechi dhidi ya Bunda, kiungo wa Simba Queens, Vivian Corazone, alisema: “Kila tukikutana na Bunda wanatupa changamoto, lakini tunaamini tumejipanga vizuri kuhakikisha tunafanya vizuri japokuwa sio rahisi kuchukua pointi tatu.”

Kocha wa Ceasiaa, Ezekiel Chobanka, alisema anakutana na timu ambayo aliwahi kuifundisha, jambo linaloifanya mechi hiyo kuwa na presha ya aina yake.