Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema kuna kila sababu kuendelea kumkumbuka na kumuezi hayati Abeid Amani Karume kutokana na ujasiri wake kufanikisha kuongoza Mapinduzi ambayo aliondoa kiza kilichokuwa kimetanda katika kisiwa hicho.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Aprili 8, 2026 katika hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla katika kongamano la nane la kumbukizi la hayati Karume katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Karume Zanzibar.
Karume aliuawa Aprili 7, 1972 kwa kupigwa risasi na mlinzi wake katika jengo la Makao Makuu ya Chama cha Afro Shiraz Kisiwandui Mjini Zanzibar ambapo kwa sasa ndio Makao makuu CCM, na kaburi lake lipo nje Kaskazini mwa ofisi hizo.
Katika kumuenzi kwa vitendo, Dk Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuimarisha huduma bora za kijamii kwa wananchi, kuhamasisha uwekezaji na kuongeza fursa za ajira kama ilivyokuwa dhamira yake ya kukataa dhuluma.
“Alipofanya Mapinduzi, alisema yameleta uhuru na kumtoa Mwafrika kwenye dharau za mkoloni,” amesema,
Amesema maneno haya yanaonesha dhamira yake ya dhati kwa ukombozi kwa wananchi kuleta heshima, ustawi na kujenga umoja.
Amesema kongamano hilo linalowaleta pamoja makundi mbalimbali kupata fikra na maono yake, wanatakiwa kuyaendeleza na kuyatangaza ili yaendelee kuwajenga na kuongeza tija zaidi kwa jamii na wawe mabalozi wazuri kueneza fikra na falsafa za Mzee Karume kwa vitendo katika jamii na mahala pa kazi.
Akizungumzia kuhusu kauli mbiu isemayo “Maono ya Sheikh Abeid Amani Karume katika kudumisha utaifa na uchumi endelevu” amesema, inapaswa kutafakariwa kutumika kwa vitendo fikra katika kuongeza kasi ya maendeleo katika uchumi wa Zanzibar na kudumisha amani na mshikamano.
Amesema Mzee Karume hakutaka kumuona mtu akidhulumiwa kwa sababu ya hali yake, dini yake.
“Imani kuwa tumejifunza utamaduni wa kuhudumiana, kupendana na kuishi kwa usawa na viongozi kuendelea kusimamia vyema jukumu la kuleta maendeleo kwa kushirikiana na wananchi.”
“Ni muhimu kukumbuka Karume alikuwa mwana jumuiya wakati wote alisisitiza umoja wa kitaifa na ndio maana leo tunajivunia taifa la Tanzania ambalo ilitokana na waasisi hao kuunganisha mataifa yetu Aprili 26 mwaka 1964,” amesema.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo ni wajibu kuendeleza Mapinduzi na Muungano wa kihistoria kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya chuo hicho, Stephen Wasira amesema lengo kubwa ya mapinduzi ilikuwa ni kuleta maendeleo ya kiuchumi na kuwepo utawala wa kisheria.
“Mapinduzi yalileta mabadiliko ambayo yalitaka haki sawa, yaligawa heka tatu za ardhi haki ya uchumi na upendeleo ya sheria, kwa hiyo tunapomkumbuka tunakumbuka mafanikio ya kuleta umoja Zanzibar kwa sasa hakuna ubaguzi,” amesema
Amesema takribani asilimia 60 wanaohitimu katika chuo hicho ni wanawake lakini kabla ya hapo wanawake hawakupewa fursa kwa hiyo tukisema mapinduzi daima mbele ndio hayo, ukiyaacha yatakuwa mapinduzi nyuma,” amesema Wasira
Wasira ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, amesema chuo hicho kiliamua kufanya kongamano kila mwaka kutoa elimu kwa vijana ili kutambua kazi kubwa iliyofanywa na waasisi wa mataifa hayo.
“Kama hatusemi vijana wanaweza kudhani jinsi walivyo ndivyo walivyokuwa kumbe kuna watu walipigania haki hizo lakini wanatakiwa kutambua kwamba Zanzibar wakati wa ukoloni hakukuwa na haki na huduma zilitolewa kwa ubaguzi mkubwa,” amesema
Kwa mujibu wa Wasira, Zanzibar haki ilikuwa ngumu kuipata, ilitolewa kwa rangi, ukabila au asili ya mtu “Kama asili yako haikumpendeza mtawala basi wewe huwezi kupata haki, kama itampendeza basi utapata.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Haruna Mapesa amesema chuo kinatoa mafunzo katika sayansi ya jamii, uongozi maadili na utawala bora, tafiti ushauri katika taasisi za umma na binafsi ikiwa ni sehemu ya kuenzi waasisi wa Mapinduzi na Uhuru.
Amesema chuo kinaendelea kuwa kitovu cha utoaji maarifa, ufumbuzi na umoja wa kitaifa.
“Chuo ambacho kimeendelea kuwa kitovu cha maarifa kuwapika viongozi katika nyanja mbalimbali,” amesema.
Amesema chuo kimejiwekea utaratibu wa kufanya makongamano kwa viongozi na waasisi wa mataifa hayo kujikumbusha fikra na falsafa na jinsi zinavyoweza kuchangia maendeleo na uchumi.
“Aprili 5, 2028 kongamano la kwanza lilifanyika na la leo ni la nane likiwa na kauli mbiu ya maono ya Sheikh Abeid Amani Karume katika kudumisha utaifa na uchumi endelevu,” amesema.
Katika kongamano hilo ziliwasilishwa mada mbili; Mchango wa uzalendo katika kudumisha umoja wa kitaifa na nafasi ya elimu ya sayansi na teknolojia katika ukuaji wa uchumi wa buluu.
