Wagonjwa wa kigeni 3,018 watibiwa Tanzania, utalii tiba waimarishwa

Dodoma. Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Februari, 2026, jumla ya wagonjwa 3,018 ambao ni raia wa kigeni walipatiwa matibabu kwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika hospitali mbalimbali nchini.

Hospitali zilizotua huduma hizo ni ngazi ya rufaa za mikoa, kanda, hospitali maalumu na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo ilisaidia kuongeza mchango katika sekta ya afya katika upatikanaji wa vifaatiba vya kisasa ikiwemo PET/CT Scan, Angio Suite, Cathlab na CT Scan.

Takwimu hizo zimetolewa leo Jumatano Aprili 8, 2026 na Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Catherine Joachim.

Mbunge huyo ametaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuendeleza utalii tiba nchini ili kuboresha huduma za afya na kuongeza mchango wa sekta ya afya katika pato la Taifa.

Catherine pia amehoji namna gani ambavyo Serikali inaweza kushirikiana na hospitali binafsi kwenye mpango huo kwani sekta binafsi imepewa kipaumbele zaidi katika kukuza na kuchangia kwenye uchumi wa Taifa.

Naibu Waziri amesema katika kuendeleza utalii wa tiba nchini, Serikali inatekeleza mpango wa uboreshaji wa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi wenye vipaumbe kama miundombinu inayotakiwa kujengwa upya au kukarabati iliyochakaa.

“Kipaumbele kingine ni kuwajengea uwezo watumishi katika utoaji wa huduma kwa kuwaendeleza kitaaluma, kuanzisha huduma mpya za ubingwa bobezi, kuziwezesha hospitali zetu kupata ithibati za kimataifa na kuzitangaza huduma zinazotolewa na hospitali hizo nchi za nje,” amesema Dk Samizi.

Kuhusu kuzijengea uwezo hospitali binafsi, Naibu Waziri amesema mpango huo ni mkakati wa pamoja kwani Serikali inatambua umuhimu wa sekta binafsi katika kuchangia asilimia kubwa kwenye uchumi wa nchi.