Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani Tanzania, imefuta sehemu ya mwenendo wa shauri la madai ya kashfa na tuzo ya Sh6 bilioni aliyokuwa ameipata waziri wa zamani wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Benard Membe.
Badala yake, majaji watatu, Ferdinand Wambali, Lucia Kairo na Dk Deo Nangela, wameamuru jalada la kesi hiyo lirudishwe Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ili shauri hilo lisikilizwe upya kuanzia pale mashahidi walipoanza kutoa ushahidi.
Hayo yamo katika hukumu waliyoitoa Aprili 2, 2026 na kuwekwa katika tovuti ya mahakama Aprili 8, 2026, wakati wakitoa hukumu ya rufaa iliyokatwa na mrufani, Cyprian Musiba na mhariri wa gazeti la Tanzanite linalomilikiwa na Musiba.
Rufaa hiyo iliihusisha kampuni ya CZ Information and Media Consultant Ltd ambao ni wachapishaji wa gazeti la Tanzanite ambalo Membe aliyefariki dunia Mei 12,2023, aliwashtaki wadaiwa akiomba limlipe fidia ya Sh10.1 bilioni.
Membe alifungua shauri hilo akidai kati ya Oktoba 2018 na Mei 2019 katika mfululizo wa matoleo yake, wadaiwa walichapisha taarifa za kashfa dhidi yake kwamba ni mdanganyifu wa uchaguzi na ni tishio la usalama wa Taifa.
Membe alidai gazeti hilo lilichapisha taarifa zaidi likidai yeye anatakatisha fedha kutoka nchini Libya na anajihusisha na biashara ya dawa za kulevya, madai ambayo alidai ni ya uongo na yalichafua heshima yake na kumletea usumbufu.
Ni kutokana na machapisho hayo, Membe alidai yalisababisha mradi wa thamani ya Sh4 bilioni aliokuwa nao usitishwe, akafukuzwa uanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kunyang’anywa pasi ya kidiplomasia na kuzuia kusafiri nje ya nchi.
Kesi hiyo ilisikilizwa upande mmoja (ex parte) baada ya Musiba na wenzake kutohudhuria kortini hivyo Mahakama ikatoa hukumu ya upande mmoja.
Katika hukumu iliyotolewa Oktoba 28, 2021 na Jaji Joacquine De-Mello, Membe aliibuka kidedea ambapo Mahakama iliwaamuru wadaiwa hao watatu kumlipa fidia ya Sh6 bilioni na wakazuiwa kuendelea kuchapisha taarifa za kashfa.
Musiba na wenzake walikata rufaa Mahakama ya Rufani Tanzania jijini Dar es Salaam dhidi ya mke wa Membe, Dorcas Membe ambaye amebeba mikoba ya mumewe baada ya kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi ya mwanasiasa huyo.
Katika rufaa hiyo wakata rufaa waliwakilishwa na wakili Sylvanus Mayenga wakati mjibu rufaa akiwakilishwa na mawakili Shundi Mrutu na Jonathan Mndeme.
Musiba waliwasilisha sababu moja ya rufaa ambayo ni Jaji alikosea kisheria kwa kutunga hukumu inayotokana na ushuhuda ambao hawakula kiapo kinyume na mahitaji ya Sheria ya Viapo na Tamko la Kisheria Sura ya 34.
Mashahidi hao ni Benard Membe mwenyewe aliyekuwa shahidi wa kwanza, Balozi mstaafu, Patric Isere aliyekuwa shahidi wa pili na shahidi wa tatu, Amri Mnkombolo.
Akijenga hoja, wakili Mayenga alieleza kuwa kumbukumbu za Mahakama, zinaonyesha Membe alitoa ushahidi bila kula kiapo na vilevile kwa shahidi wa pili ambapo inaonekana karani wa Mahakama aliwaongoza kula kiapo.
Lakini akasema hakuna kiapo kinachoweza kuapwa kabla ya kuchukua jina la shahidi, kazi, umri na dini yake na inaonekana karani aliwaongoza kula kiapo, lakini kumbukumbu hazionyeshi kama waliapa.
Hali kama hiyo ilitokea kwa shahidi wa tatu hivyo hoja yake ni kuwa kisheria, hapakuwepo na kiapo halali kabla mashahidi hao kutoa ushahidi.
Akijibu hoja hizo, wakili Mrutu alikanusha madai hayo na kumtuhumu wakili Mayenga kwa kile alichokiita ‘misplaced arguments’ au hoja zisizo sahihi
Ni msimamo wake kuwa mashahidi wote watatu waliongozwa kula kiapo kabla hawajatoa ushahidi wao na kusema hoja ya waleta rufaa haina mashiko.
Katika hukumu yao, majaji hao walisema baada ya kusikiliza mabishano ya pande mbili, hoja wanayopaswa kuiamua ni kama kweli au sio kweli, mashahidi walikula kiapo kabla ya Mahakama kuanza kuchukua ushahidi wao.
Majaji hao walirejea kumbukumbu za mwenendo wa kesi siku wakitoa ushahidi zinaonyesha kile kilichorekodiwa na Mahakama hakikidhi vigezo vya kuitwa kiapo kwa kuwa hakuna maelezo ya kuthibitisha kuwa walikula kwanza kiapo.
“Kuhusu kesi iliyopo mbele yetu, rekodi ya rufaa inaonyesha kwamba, mashahidi waliongozwa kwa kiapo au uthibitisho kabla ya kujitambulisha wenyewe na maelezo yao yameandikwa,” walieleza majaji hao na kuongeza kusema:-
“Katika mazingira hayo, Mahakama imeachwa kubashiri kile hasa kilichotokea katika chumba cha mahakama kuhusu kuchukua kiapo/uthibitisho wa mashahidi.”
“Kanuni ya msingi ya Mahakama mfumo unazitaka mahakama kutoamua kesi kwa kubahatisha au kubahatisha juu ya kile kilichotokea au kwa kesi iliyopo, iwe ni utaratibu sahihi ulifuatwa wakati wa kuapa au kuthibitisha mashahidi.”
“Ni mtazamo wetu thabiti kwamba, nukuu zilizorekodiwa za mwenendo wa kesi zinaonyesha utaratibu ulikuwa na dosari mojawapo ni kutowaapisha kabisa mashahidi na mbili kwa kuwaapisha bila utangulizi na kurekodi maelezo yao.”
Majaji hao walikubaliana na hoja za wakili Mayenga kuwa kuapa au kuthibitisha shahidi kabla ya kuchukua ushahidi wake ni lazima kisheria mahitaji chini ya masharti ya kifungu cha 3 cha Sheria hiyo inayosimamia viapo.
“Katika maamuzi tuliyoyarejea, tulisisitiza msimamo wetu kwamba kushindwa kuzingatia mashahidi wa kiapo au uthibitisho ni mbaya na ushahidi ni ubatili na kwa sababu hiyo, ushahidi huo hauwezi kutumika kuamua haki ya wahusika.”
“Kwa njia hiyohiyo, ni uamuzi wetu kwamba, ushahidi wa shahidi namba 1,2 na 3 uliorekodiwa bila kuapishwa au kuthibitishwa unakuwa sio ushahidi kabisa.”
“Kwa hivyo, tunatumia mamlaka yetu chini ya kifungu cha 4 (2) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa Sura ya 141 kubatilisha hukumu ya Mahakama Kuu na kesi isikilizwe upya kuanzia mashahidi walipoanza kutoa ushahidi na kuendelea, yaani, Mei 4, 2021 na kuweka kando amri yake (tuzo) ,” walieleza majaji hao katika hukumu yao.
Majaji hao walisema vinginevyo iliyobaki sehemu ya kesi imesalia sawa na wakaagiza faili la kesi hiyo lipelekwe mahakama iliyosikiliza ili isikilizwe tena kuanzia pale mashahidi walipotoa ushahidi wao ambayo ni Mei 4,2021.
Kesi hiyo itasikilizwa upya wakati aliyekuwa shahidi wa kwanza, Membe mwenyewe akiwa ameshafariki dunia na ndiye alikuwa mlalamikaji.
