Daladala Dar, Mwanza zaomba kusitisha huduma kuanzia kesho

Dar es Salaam. Saa chache baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (Latra) kutangaza kuongeza muda wa wiki mbili zaidi wa kupokea maoni kuhusu mapitio ya nauli, Umoja wa Wasafirishaji Abiria Dar es Salaam na Mwanza umeomba kusitisha kutoa huduma.

Kwa mujibu wa wasafirishaji hao, sababu kuomba kusitisha huduma hizo jijini Dar es Salaam na Mwanza zimetokana na kujiendesha kihasara tangu ongezeko gharama za mafuta lililoanza Aprili Mosi, 2026 lililotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura).

Kauli ya wadau hao imetolewa leo Jumatano Aprili 8, 2026 na viongozi wa umoja huo jijini Dar es Salaam wakati wakiwasilisha maoni ya taasisi hizo ya namna inavyojiendesha tangu kupanda kwa bei za mafuta katika mkutano wa wadau wa usafirishaji ulioandaliwa na Latra.

Mwenyekiti wa Umoja huo Mkoa wa Dar es Salaam (Uwadar), Jafar Kismat amesema baadhi ya mikoa kama ya Mbeya na Arusha, Kilimanjaro kuna nyakati daladala ziligoma kutoa huduma sambamba na kuongeza nauli kinyemela na hakuna hatua zilizochukuliwa hata hivyo, Uwadar haitaki kufika huko, lakini Latra iwaangilie.

“Lengo letu si kugoma kwa sababu ni mwiko, sasa tukigoma tunamgomea nani? Lakini mkurugenzi (Latra) hapa tulipofikia tulitarajia leo utasema… lakini unatuambia hadi siku 14 ingawa sheria inataka hivyo, ila watu wameshindwa kutoa huduma.

“Hii wiki moja ambayo unaona daladala ni kwa sababu sikukuu, sasa wenzangu wameniambia kama utaratibu ndio huu hakuna nyongeza yoyote, sisi hatugomi ila tutawaomba kusitisha kwa muda huduma hadi mtakaporekebisha,” amesema Kismat.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wasafirishaji Abiria Mkoa wa Mwanza, Yusuph Lupilia amelalamikia kitendo cha usafiri wa bajaji kufanya kazi sawa na daladala katika vituo vyote jijini humo.

Lupilia ameitaka Latra kuongeza bei ya nauli ili daladala zijiendeshe akipendekeza kuanzia kilomita sifuri hadi kilomita 10 iwe Sh800 kutoka Sh 600.

“Wasafirishaji nchi nzima wanakutegemea wewe (Mkurugenzi wa Latra), mimi nasema ukweli, sina konakona mkikataa kuongeza nauli kesho Mwanza gari hazitoki… tuone nguvu sasa ya Serikali na wamiliki,” amesema Lupilia.

Mapema leo asubuhi Mkurugenzi wa Latra, Dk Habibu Suluo alitangaza kuongeza wiki mbili ili kutoa fursa kwa wadau kuwasilisha maoni kuhusu mapitio ya nauli ongezeko baada upandaji wa bei za mafuta ulioanza Aprili Mosi, 2026.

Katika mchango wake, Kismat amesema haiwezekani daladala ikaweka mafuta ya Sh4,000 kisha ikaendelea kumtoza nauli ileile mwananchi jambo ambalo ni hasara.

“Tulitegemea mkurugenzi ungesema kutokana na hali hii ungetuongezea kidogo wakati taratibu zingine zikiendelea. Lakini kama utaratibu ndio huu wa mafuta Sh3,800 mkurugenzi utanisamehe kesho unaweza kuona daladala hazipo usiseme ni mimi hapana,” ameeleza Kismat.

Kismat amesisitiza ombi lao la kusitisha huduma likubaliwe na Latra hadi pale taasisi hiyo itakapofanya uchanganuzi vizuri.

“Mkurugenzi tunakuomba utuone neno lolote pamoja na sheria hairuhusu, lakini hata mama (Rais Samia Suluhu Hassan) anajua. Tuambie neno litakalotufurahisha hata tuongeze Sh100. Kama hakuna kifutio kidogo kesho daladala huzioni,” amesisitiza.