Safari ya wanaanga wa NASA; Rekodi, sayansi na historia

Dar es Salaam. Wanaanga wanne kutoka Shirika la Anga la Marekani (NASA) wameanza kurejea duniani baada ya kukamilisha safari ya kihistoria ya kuuzunguka mwezi, na kufanikiwa kufika mbali zaidi na Dunia kuliko binadamu yeyote kuwahi kufika.

Safari hiyo ya siku 10, iliyoanza Aprili mosi, 2026, iliyopewa jina ‘Artemis II’, imehusisha wanaanga Reid Wiseman, Victor Glover, Christina Koch kutoka nchini Marekani na Mkanada Jeremy Hansen, ambao wamekuwa ndani ya chombo cha anga za juu cha Orion.

Kwa mujibu wa ratiba, chombo hicho kinatarajiwa kutua baharini katika Bahari ya Pasifiki karibu na pwani ya magharibi ya Marekani, Ijumaa saa 20:07 kwa saa za Marekani (01:07 asubuhi Jumamosi kwa saa za Afrika Mashariki).

Katika safari hiyo, Orion ilifikia umbali wa kilomita 406,771 kutoka usawa wa Dunia, hatua iliyovunja rekodi ya umbali mrefu zaidi kuwahi kufikiwa na binadamu angani.

Wanaanga hao hawakutua mwezini, lakini walifanya mzunguko maalumu kuuzunguka kabla ya kurejea, hatua muhimu inayotarajiwa kufungua njia kwa safari za baadaye za kutua mwezini kwa mara ya kwanza tangu enzi za misheni za Apollo.

Wanaanga wa NASA walifika mwezini kwa mara ya kwanza Julai 20, 1969 kupitia mpango wa Apollo 11, ambapo Neil Armstrong alikuwa mtu wa kwanza kutembea kwenye uso wa mwezi, akifuatiwa na Buzz Aldrin, huku Michael Collins akibaki akizunguka mwezi ndani ya chombo cha Apollo 11.

Baada ya Apollo 11, kulikuwa na safari nyingine tano za mafanikio za Apollo zilizotuma wanaanga wengine mwezini hadi mwaka 1972, na kwa jumla wanaanga 12 walitembea juu ya uso wa mwezi.

Safari hiyo ilikumbwa na changamoto kadhaa tangu mwanzo, zikiwemo hitilafu za mifumo ya usalama wa roketi na betri ya mfumo wa dharura kabla ya kurushwa. Hata hivyo, matatizo hayo yalitatuliwa na kuruhusu uzinduzi kufanyika kwa mafanikio.

Wakiwa angani, wanaanga walikumbana pia na changamoto ndogo, ikiwemo hitilafu ya mawasiliano kwa muda mfupi na tatizo la choo ndani ya chombo, ambalo lilirekebishwa.

Mwanaanga Christina Koch alituma ujumbe wenye hisia kali kutoka ndani ya chombo cha Orion uliogusa mioyo ya watu duniani kote. Baada ya kurejesha mawasiliano baada ya kupita upande wa mbali wa mwezi, alisema:

“Ni jambo la kufurahisha kuwasiliana tena na Dunia. Kwa Asia, Afrika na mabara mengine, tunawaona kutoka huku. Mnaweza kuangalia juu na kuuona mwezi wakati huu, nasi tunawaona pia.

“Tulipoelekeza safari yetu mwezini, nilisema hatuachi Dunia… tunaenda kuhamasisha, lakini mwisho wa yote, daima tutaichagua Dunia, daima tutachaguana sisi kwa sisi.”

Maneno hayo yalitolewa katika moja ya nyakati muhimu zaidi ya misheni hiyo, wakati wanaanga walipokamilisha mzunguko wao wa kihistoria kuuzunguka mwezi. Ujumbe wake unaonesha uhusiano wa kina kati ya utafiti wa anga na mahali tunapotoka.

Licha ya hayo, ujumbe huo umefanikiwa kufikia malengo yake muhimu, ikiwemo kupima mifumo ya chombo cha Orion kama vile uendeshaji, nishati, mawasiliano na maisha ya binadamu angani.

Matukio ya kipekee angani

Ikiwa angani, timu hiyo ilishuhudia tukio la kupatwa kwa jua na kupata picha za kipekee za upande wa mbali wa mwezi, eneo ambalo halionekani kirahisi kutoka duniani.

Katika ishara ya kumbukumbu binafsi, wanaanga walipendekeza jina la “Carroll” kwa moja ya mashimo ya mwezi, kumuenzi marehemu mke wa kamanda Wiseman.

Ujumbe wa Artemis II ni sehemu ya mpango mpana wa Artemis Program unaolenga kumrudisha binadamu mwezini ifikapo mwaka 2028 na baadaye kujenga makazi ya kudumu kwa ajili ya safari za anga za mbali zaidi, ikiwemo kuelekea sayari ya Mars.

Mbali na mafanikio ya kisayansi, safari hiyo imevutia mamilioni ya watu duniani kupitia picha na video zilizokuwa zikitumwa moja kwa moja, huku ujumbe wa mshikamano wa binadamu ukitolewa na mwanaanga Glover aliposema: “Kutoka huku juu, Dunia inaonekana kama kitu kimoja; sote ni binadamu.”

Safari ya kwenda mwezini si ya moja kwa moja kama wengi wanavyodhani. Kwa misheni ya Artemis II, chombo hulazimika kwanza kuzunguka Dunia kabla ya kuelekea mwezini, hatua inayochochewa na sababu za kisayansi na kiusalama.

Baada ya kurushwa, chombo huingia katika obiti ya karibu ya Dunia. Katika hatua hii, wahandisi hufanya ukaguzi wa mifumo yote ili kuhakikisha kila kitu kinafanya kazi ipasavyo. Pia, huzingatia mwelekeo sahihi wa safari kulingana na nafasi ya mwezi.

Hatua muhimu inayofuata ni kuwashwa kwa injini kwa nguvu zaidi katika kile kinachoitwa ‘Trans Lunar Injection’. Hapa ndipo chombo hupata kasi ya kutosha kujinasua kutoka kwenye mvuto wa Dunia na kuanza safari ya kuelekea mwezini. Roketi kama Space Launch System zimeundwa kutoa nguvu hii kubwa.

Tofauti na safari ya kwenda, kurudi kutoka mwezini ni rahisi zaidi kwani hutegemea mvuto wa Dunia. Chombo hutumia nguvu ndogo kuondoka kwenye obiti ya mwezi, kisha huvutwa na mvuto hadi kurejea duniani.

Changamoto kubwa huwa wakati wa kuingia tena angani, ambapo joto kali hutokea kutokana na kasi kubwa, hivyo vifaa vya kuzuia joto ni muhimu kulinda wanaanga.

Kwa ujumla, safari ya mwezini inahitaji mipango makini, huku kurudi kukitegemea zaidi nguvu za asili.

Safari hiyo imeelezwa kuwa ni alama ya matumaini na uwezo wa binadamu kufanya mambo makubwa licha ya changamoto zinazoikabili dunia kwa sasa.