Dar es Salaam. Mashahidi 12 wa upande wa Jamhuri, wanatarajiwa kutoa ushahidi katika kesi ya wizi wa jenereta, inayomkabili Emmanuel Fredrick (26), maarufu Mramu na Emmanuel Chale (32).
Mashahidi hao wanatarajia kutoa ushahidi wao, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mkoa wa Dar es Salaam.
Mramu na Chale, wanakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la wizi wa jenereta moja lenye thamani ya Sh64.9 milioni, mali ya kampuni ya Yapi Merkenzi.
Wakili wa Serikali, Cathbert Mbiling’i ameieleza Mahakama hiyo, leo Jumatano Aprili 8, 2026 wakati akiwasomewa hoja za awali washtakiwa hao.
Wakili Mbiling’i ametaja idadi hiyo ya mashahidi, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, kabla ya kuwasomea hoja za awali, wakili Mbiling’i aliwasomea upya mashtaka yao.
Amedai katika shtaka la kwanza ni wizi na linawakabili washtakiwa wote.
Amesema washtakiwa wanadaiwa, Agosti 15, 2025 eneo la Goldstar, lililopo Wilaya ya Ilala, washtakiwa kwa pamoja waliiba jenereta moja aina ya Cater rangi ya njano yenye thamani ya Sh64.9 milioni, mali ya Kampuni ya Yapi Merkez.
Katika shtaka la pili ni kukutwa na mali ya wizi linalomkabili Mramu pekee yake, tukio analodaiwa kulitenda Agosti 18, 2025 eneo la Kona kwa Mbowe, lililopo Salasala wilaya ya Kinondoni, kinyume na sheria alikutwa akimiliki jenereta hiyo idhaniwayo kuwa ni mali ya wizi, mali ya Yapi Merkez.
“Uchunguzi ulifanyika ambao ulipekea washtakiwa kukamatwa na kuhojiwa Polisi na washtakiwa walikiri kuhusika na wizi huo na kukutwa na mali ya wizi.
“Uchunguzi zaidi ulifanyika kwa kuthibitisha mali ya wizi iliyokuwa imeibiwa na kupata ripoti ambayo ulionyesha thamani halisi ya jenereta lililoibiwa,” amedai.
Ameendelea kueleza baada ya upelelezi kukamilika, washtakiwa walikamatwa na kupelekwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.
Washtakiwa baada ya kusomewa hati ya mashtaka na maelezo yao, walikana mashtaka isipokuwa taarifa zao binafsi.
“Mheshimiwa hakimu, upande wa mashtaka tunatarajia kuwa na mashidi 12 na vielelezo vitano,” amedai wakili Mbiling’i.
Hakimu Mhini, baada ya kusikiliza maelezo hayo aliahirisha kesi hadi Aprili 21, 2026 itakapoanza kusikilizwa ushahidi na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.
