Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeshindwa kusikiliza ushahidi wa upande wa Jamhuri katika kesi ya kughushi vibali vya kumiliki silaha inayowakabili watu tisa wakiwemo maofisa sita wa Jeshi la Polisi, baada ya simu ya mleta vielelezo kutopatikana.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mkaguzi wa Polisi mwenye namba PF. 19931 Fredrick Malekela(45)mkazi wa Kilwaroad; E. 4627 Sajenti Kalemwa Kaunga(54) mkazi wa Chanika; E.7855 Sajenti Edger Mlogo(54)mkazi wa Kibamba; F.1126 Sajenti Robert Titus(47)mkazi wa Kisarawe na F.5092 Sajenti John Kaposwe(46) mkazi wa Kurasini na WP 10050 Julieth Moshib(30) mkazi wa Kisarawe.
Wengine ambao sio maofisa wa jeshi hilo ni Damson Mnyilenga (59) mkulima na mkazi wa Chanika; Simon Aloyce (60) mfanyabiashara na mkazi wa Mwanza pamoja na Venrand Liberio (29) mfanyabiashara na mkazi wa Tataba.
Kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa kwa siku tatu mfululizo kuanzia leo Jumatano Aprili 8, 2026 na tayari upande wa Jamhuri walikuwa na shahidi mmoja, ambaye alitakiwa kutoa ushahidi wake dhidi ya washtakiwa hao.
Wakili wa Serikali, Cathbert Mbiling’i, ameieleza Mahakama hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini anayesikiliza kesi hiyo.
“Kesi imeitwa kwa ajili ya usikilizwaji na ilipangwa kusikilizwa siku tatu mfululizo na leo upande wa Jamhuri tuna shahidi mmoja, lakini kwa asili ya ushahidi wake tunatakiwa tuwe na vielelezo.”
“Na mtu anayetunza vielelezo hivyo, simu yake haipatikani tumejaribu mara kadhaa kumtafuta hapatikani, hivyo kwa kuwa kesi hii imepangiwa siku tatu mfululizo, tunaiomba mahakama yako utupe ahirisho mpaka kesho ili tuweze kuendelea na usikilizwaji,” amedai Mbiling’i.
Mbiling’i baada ya kutoa taarifa hiyo, wakili wa utetezi, George Mwalai ameomba upande wa mashtaka wapeleke mashahidi zaidi ya mmoja ili ikitokea changamoto kama hiyo, kesi hiyo isikwame.
Kwa upande wake, wakili wa utetezi Nehemiah Nkoko na Kung’e Wabeya, hawakuwa na pingamizi ya kuahirisha kesi hiyo, ila walisisitiza Jamhuri kesho ipeleke mashahidi mahakamani hapo.
“Mheshimiwa hakimu, kuna mashahidi ambao hawahitaji kutoa kielelezo (nyaraka) hapa mahakamani, lakini kwa kuwa kesi hii imepangwa kwa siku tatu mfululizo, sina pingamizi, ila upande wa Jamhuri wajitahidi kesho kuleta mashahidi zaidi ya mmoja,” amedai Wakili Nkoko.
Hakimu Mhini baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, alielekeza upande wa Jamhuri kuhakikisha kuwa kesho wanapeleka mashahidi wa kutosha.
“Lengo la kupanga kesi hii isikilizwe siku tatu mfululizo ni kesi iende haraka ili haki ya watuhumiwa iweze kupatikana, hivyo upande wa Jamhuri mnapaswa kufuata utaratibu uliowekwa wa kuhakikisha kuwa siku hizi tatu tulizopanga zina kuwa na mashahidi na kesi inasikilizwa bila kiahirishwa,” amesema Hakimu Mhini na kuahirisha kesi hiyo hadi Aprili 9, 2026 saa 5:00 asubuhi itakapo anza kusikilizwa ushahidi.
Hata hivyo, washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana.
Machi 16, 2026, Jamhuri wakati ikiwasomea hoja za awali washtakiwa hao iliieleza Mahakama hiyo, kuwa inatarajia kuwa na mashahidi 43, akiwemo Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Faustine Mafwele.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 18451 ya mwaka 2025, yenye mashtaka 16 ya kughushi vibali vya kumiliki silaha.
Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa hayo, kinyume na kifungu namba 333 na 335A na kifungu 337 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.
Katika mashtaka yao, wanadaiwa kuwa vibali hivyo, vimetolewa kati ya Desemba 5, 2024 hadi Aprili 4, 2025
Katika shtaka la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa katika kipindi cha mwaka 2024, ndani ya Jiji la Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya walitengeneza nyaraka ya uongo ambayo ni kibali cha kumiliki silaha cha Desemba 5, 2024 chenye jina la Ahmed Ally, wakati wakijua kuwa sio kweli.
Shtaka la pili, hadi la 13, washtakiwa wanadaiwa katika kipindi cha mwaka 2024 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, walitengeneza vibali vya kumiliki silaha vyenye majina ya Ahmed Ahmed Sandrudin, Omary Abdallah, Robert Koka, Fathi Ally, Mohamed Salim, Suleman Mbewa, Mickdad Chakindo, Irfan Nafari, Gulam Abbas Najafi, Ismail Ismail na Salim Salim.
Shtaka la 14 hadi 16, washtakiwa hao wanadaiwa mwaka 2025 mkoani Dar es Salaam, kwa nia ya kulaghai walitengeneza nyaraka za uongo ambazo ni kibali cha kumiliki silaha chenye jina la Marwaan Habretsh, Maurice Kitiwe na Said Mohamed, wakati wakijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
