Watanzania wahimizwa kupikia nishati safi

Arusha. Wakati dunia inakabiliwa na changamoto kubwa ya mabadiliko ya tabianchi, matumizi ya nishati mbadala ya kupikia yanatajwa kuwa miongoni mwa suluhisho la kupunguza athari za uharibifu wa mazingira nchini huku jamii ikihimizwa kuachana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia.

Aidha ongezeko la joto duniani, ukataji miti hovyo na uchafuzi wa hewa vimeendelea kuhatarisha usalama wa binadamu.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Aprili 8,2026 na Meneja Programu ya Tanzania Clean Cooking (TCCP), Fredrick Tunutu, alipozungumza katika kiwanda cha teknolojia za kupikia ikiwemo majiko bunifu na nishati safi ya kupikia (kuni poa).

Amesema programu hiyo inayofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Sweden (Sida) na kutekelezwa na Shirika la AECF Tanzania inalenga kusaidia kampuni za nishati safi za kupikia kuwafikia wananchi wengi zaidi, kuwajengea uwezo na kupata ruzuku ili kuimarisha uzalishaji na usambazaji wa nishati safi.

Mwonekano wa kuni safi ya kupikia (kuni poa) zilizotengenezwa kwa kutumia mabaki ya mabaki ya miwa ya maranda ya mbao, lengo likiwa ni kupunguza matumizi ya nishati chafu ya kupikia na ambazo zinaleta athari kwa mazingira.

Amesema kutokana na ongezeko la joto duniani, ukataji miti hovyo, na uchafuzi wa hewa vimeendelea kuhatarisha afya za binadamu pamoja na mifumo ya ikolojia, hivyo jamii lazima iachane na matumizi ya nishati chafu na kuhamia kwenye nishati safi na endelevu.

“Tunaendelea kufanya kazi na kampuni 13 zinazojihusisha na teknolojia mbalimbali za nishati, ikiwemo gesi ya LPG. Hii ni sehemu ya juhudi za kufikia malengo ya serikali ya kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034,” amesema Tunutu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hanny G Investment Ltd, Hanny Mbaria, amesema kampuni yake imejikita katika uzalishaji wa kuni mbadala (kuni poa) pamoja na majiko sanifu ya kupikia.

Amesema nishati hiyo hutengenezwa kwa kutumia mchanganyiko wa mabaki ya miwa na maranda ya mbao, ambayo hupitia hatua mbalimbali za kitaalamu hadi kuwa kuni bora zinazofaa kwa matumizi ya majumbani na taasisi.

Ameongeza kuwa kwa sasa kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha tani 120 hadi 150 za nishati kwa siku, huku wakiajiri wafanyakazi zaidi ya 145 wakiwemo vijana ambao ndiyo asilimia kubwa pamoja na wanawake.

Mmoja wa wanufaika, Nomi Mollel amesema awali alikuwa mfanyakazi wa kawaida ila kwa sasa amekuwa msimamizi wa uzalishaji.

“Ajira hii imenisaidia kubadilisha maisha ya familia yangu. Sasa nina uwezo wa kujitegemea na kusaidia wengine,” amesema.

Kwa upande wake Martha Mwashinga, ambaye ni mwendeshaji wa mashine za kutengeneza majiko, amesema wanawake wana uwezo mkubwa iwapo watapewa nafasi.

“Nilianza kama msimamizi, lakini nilivutiwa na mashine, nikajifunza na sasa ninaendesha. Kazi hii imenipa heshima na kipato, ninaweza kuhudumia familia yangu.”