SAME UTALII FESTIVAL YACHOCHEA UCHUMI WA WANANCHI

Na Mwandishi Wetu SAME

WANANCHI wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, wamewaomba viongozi wa wilaya hiyo kuhakikisha Tamasha la Utalii la Same Festival linafanyika kila mwaka ili kuendelea kukuza uchumi wao na kuboresha maisha ya wananchi wa kawaida.

Ombi hilo limetolewa leo na wakinamama lishe wakati wa joggin ya kuhamasisha tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika Aprili 10 hadi 12 mwaka huu, ikiwa ni msimu wa tatu tangu kuanzishwa kwake.

Akizungumza katika joggin hiyo, mama lishe katika stendi ya mabasi wilayani Same, Anna Mzava, alisema kuwa tamasha hilo limekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza kipato chao kutokana na ongezeko la wateja kutoka maeneo mbalimbali wanaofika kushiriki.

“Tunaiomba serikali kuhakikisha tamasha hili linakuwa endelevu kwani linatusaidia sana sisi wananchi wa chini. Biashara zetu zinachangamka na tunapata kipato kikubwa zaidi. Kwa mfano, siku za kawaida napika mchele kilo tatu lakini wakati wa tamasha napika hadi kilo kumi na zote zinaisha,” alisema Anna.

Kwa upande wake, Jumanne Idd alisema kuwa tamasha hilo limekuwa chachu ya kuitangaza wilaya ya Same kitaifa, hasa vivutio vya utalii pamoja na vyakula vya asili vya kabila la Wapare.

Alisema kuwa kupitia tukio hilo, shughuli za kibiashara huongezeka kwa kiasi kikubwa, hali inayowezesha wananchi wengi kupata kipato na kunufaika kiuchumi.

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Same, Yusto Mapande, alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha tamasha hilo linaendelea kufanyika kila mwaka kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo wilayani humo.

Mapande aliongeza kuwa halmashauri itaendelea kubuni na kuibua vivutio vipya vya utalii ili kuvifanya vijulikane zaidi na hivyo kuinua uchumi wa wananchi.

“Faida kubwa tunayoitarajia ni kiuchumi. Pale watu wengi wanapokusanyika, kunakuwa na uhitaji wa huduma mbalimbali ambazo wananchi wetu wanazitoa na kulipwa, hivyo kuongeza kipato chao,” alisema Mapande.

Tamasha la Same Festival linatarajiwa kuendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza utalii, biashara na utamaduni wa eneo hilo huku likitoa fursa kwa wananchi kujikwamua kiuchumi.