Unguja. Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) imewasisitiza wafanyabiashara kutumia mfumo maalumu wa Usimamizi wa Mali (PMS) ili kupata taarifa sahihi ya biashara zao hasa mahoteli ya kulala wageni.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 8, 2026, Kaimu Waziri wa Wizara hiyo, Mudrick Ramadhan Soraga, amesema licha kuwapo mfumo huo lakini baadhi wamekuwa wakikwepa na kuisababishia Serikali hasara kwa kutopata kodi inayostahili.
Amewataka kujisajili kwenye mfumo kabla ya Aprili 24, 2026 na iwapo ukipita muda huo watazuiliwa leseni zao.
“Sekta ya hoteli ina mchango mkubwa katika pato la taifa, hivyo ni lazima kuwe na mfumo madhubuti wa ukusanyaji wa kodi unaozingatia uwazi na usawa na hilo lazima litekelezwe kwa wamiliki wa mahoteli na wafanyabiashara wote”, alisema Soraga.
Soraga ambaye pia ni Waziri Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu amesema mfumo huu unasaidia kuweka usalama na kuwawajibisha watakaokwenda kinyume na utaratibu.
Amebainisha kuwa Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuboresha ukusanyaji wa kodi, ikiwa ni pamoja na matumizi ya mifumo ya kielektroniki itakayorahisisha ufuatiliaji wa mapato ya hoteli.
“Hoteli zote zinapaswa kusajiliwa na kutumia mashine za kielektroniki za kutolea risiti ili kuhakikisha kila mapato yanarekodiwa ipasavyo na kodi stahiki inalipwa kwa wakati,” alisema.
Waziri Soroga amebainisha kuwa awali Serikali ilikuwa na kilio kikubwa cha kupoteza fedha na taarifa halisi za uingiaji wa wageni, ikiwa ni pamoja na siku wanazokaa watalii nchini sambamba na gharama za matumizi yao.
Soraga amefahamisha kuwa, utalii ni chanzo mojawapo kinachochangia asilimia 30 pato la taifa, lakini mapato hayo hayana uhalisia kwa sababu watu wanakwepa kulipakodi.
“Watoa huduma wote wa mahoteli tunataka wajisajili kwani mfumo huu pia utatusaidia kutathmini fedha za gawio la Serikali ambazo awali kulikuwa na mianya,” alisema.
Ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wadau pamoja na kurahisisha taratibu ili kuwavutia wawekezaji zaidi kuendelea kuwekeza nchini hasa katika sekta hiyo ya hoteli.
Naye, Biubwa Omar, kutoka Jumuiya ya Wawekezaji wa Utalii Zanzibar (ZATI), amesema ikiwa Serikali imeamua kuweka mfumo huo ni lazima kuwe na usimamizi mzuri wa mfumo huo ili kuhakikisha kila mmoja anawajibika na serikali inapata mapato yake.
Hivyo, aliwataka watoa huduma kuhakikisha wanashirikiana na serikali ili kuona mfumo huo unafanikiwa na serikali inapata mapato yake kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa wananchi.
