Sababu tume ya Oktoba 29 kuongezewa muda

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Kuchunguza Matukio ya Oktoba 29, Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande, ameeleza sababu za kuomba nyongeza ya muda, akisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha ripoti ya tume inakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa, huku ikijibu matarajio makubwa ya Watanzania na jumuiya ya kimataifa.

Sambamba na hilo, Jaji Chande amekanusha kuwa nyongeza ya muda inalenga kuathiri maudhui ya ripoti, akisisitiza kuwa tume ndiyo yenye mamlaka kamili ya kuandaa na kuwasilisha ripoti yake.

“Sisi ndio tunaandika ripoti. Hakuna mtu wa kuhariri au kuingilia kazi yetu,” amesema.

Mwenyekiti huyo amewaeleza wanahabari kuwa tangu kuanza kwa tume hiyo, kumekuwepo na taarifa za upotoshaji, zikiwemo zinazowatisha watoa ushahidi, lakini amesisitiza kuwa watu wengi wamejitokeza kutoa ushahidi kwa hiari. “Tume ni huru kwa asilimia 100. Ushahidi mwingi umetolewa kwa hiari, na idadi yake ni kubwa,” amesema.

Kauli ya Jaji Chande imekuja muda mfupi baada ya tume hiyo kuongezewa muda hadi Aprili 24, 2026, kukamilisha kazi yake.

Hii ni mara ya pili kwa tume hiyo kupewa nyongeza ya muda, baada ya awali kuongezewa siku 42 ili kuendelea na uchunguzi wa matukio yaliyotokea kabla na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29.

Uamuzi wa kuongeza siku 42 ulilenga kutoa nafasi na muda kwa tume hiyo kukamilisha kukusanya zaidi taarifa, maoni, na ushahidi kutoka kwa wananchi. Sababu nyingine iliyotajwa ni kutoa fursa ya kutosha kwa kila mwenye taarifa, ushahidi au maoni, aliyepo nchini au nje ya nchi, kuwasiliana na tume.

Tume hiyo iliundwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuanza kazi Novemba 20, mwaka jana, ikapewa siku 90 ambazo zilimalizika Februari 20, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Aprili 8, 2026, Jaji Chande amesema kitaalamu tume yake ni ya uchunguzi na si ya upelelezi, akisisitiza kuwa asili ya kazi hiyo imeifanya kuwa pana zaidi kadri ushahidi unavyoendelea kupokelewa kutoka kwa wananchi.

“Kazi yetu inaongozwa na ushahidi unaotolewa na wananchi. Hatuwezi kuwazuia watu kuleta ushahidi, wala kuupuuza pale unapowasilishwa. Tunapaswa kuupokea na kuufanyia uchambuzi wa kina,” amesema.

Amesema mtiririko wa ushahidi umekuwa mkubwa hasa katika siku za mwisho kabla ya kuongezewa muda, jambo lililolazimu tume kuomba muda zaidi, ili kuhakikisha hakuna ushahidi muhimu unaoachwa nje ya uchambuzi.

Jaji Chande amewataka Watanzania kutumia muda huo wa nyongeza kuwasilisha ushahidi zaidi, akisisitiza kuwa ushiriki wao ni muhimu katika kufanikisha kazi ya tume hiyo.

“Tunatambua matarajio makubwa ya Watanzania na jumuiya ya kimataifa. Hivyo, ni muhimu kuhakikisha kila ushahidi unaopatikana unachambuliwa kwa weledi ili kupata ukweli kamili,” amesema.

Kilichosababisha muda kuongezwa

Katika mkutano huo, Jaji Chande amezitaja sababu kuu nne za kuongezwa kwa muda kuwa ni uzito na ukubwa wa kazi, kina cha uchambuzi unaohitajika, wingi wa ushahidi unaoendelea kupokelewa, pamoja na hitaji la kufanya uchambuzi wa kisayansi wa baadhi ya vielelezo.

Amesema baadhi ya ushahidi, ikiwemo picha zilizopigwa kwa satelaiti na kusambazwa mitandaoni, zinahitaji kuthibitishwa na wataalamu ili kubaini uhalisia wake kabla ya kujumuishwa katika ripoti ya mwisho.

“Tunapokea ushahidi wa aina mbalimbali. Kuna ushahidi wa picha na taarifa zinazohitaji uchambuzi wa kitaalamu. Hatuwezi kuuchukua moja kwa moja bila kuupitia kwa kina,” amesema Jaji Chande.

Aidha, amebainisha kuwa tume inalenga kufikia wananchi wengi zaidi ili kupata mtazamo mpana wa matukio hayo, sambamba na kuhakikisha ripoti yake inatafsiriwa kwa Kiswahili na Kiingereza ili ieleweke kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Awali, tume ilipanga kutembelea mikoa sita iliyoathiriwa zaidi na ghasia, lakini baada ya kuanza kazi ilibaini umuhimu wa kupanua wigo, hivyo kufikia mikoa 11 na wilaya 22.

Amesema hatua hiyo imelenga kupata picha kamili ya matukio kwa kuzungumza na wananchi katika maeneo yaliyoathiriwa na yale ambayo hayakuathiriwa.

“Kazi ya tume inaongozwa na ushahidi. Ndiyo maana hatuwezi kuacha ushahidi wowote unaotufikia. Tunaamini muda tuliopata utatosha kukamilisha kazi hii kwa ubora,” amesema Jaji Chande.

Ameongeza kuwa ushahidi ambao hautawasilishwa mbele ya tume hautazingatiwa, akihimiza wananchi wenye taarifa kujitokeza kwa hiari.

Jaji Chande amesema matarajio ya tume ni kuhakikisha ripoti yake itawafanya waathirika wa matukio ya Oktoba 29 kujihisi wametendewa haki na kusikilizwa.

“Tunataka ripoti itakayowafanya waathirika wajione wamo ndani yake. Lengo ni kusaidia Taifa kusonga mbele kwa mshikamano na uelewano,” amesema.

Kuhusu uhuru wa tume, amesema umejengwa katika sheria iliyoianzisha pamoja na viapo vya wajumbe wake, akisisitiza kuwa hakuna mtu au chombo kinachoiagiza nini cha kufanya.

Amesema baada ya kupokea hadidu za rejea, tume iliandaa kanuni zake, ikiwemo kuruhusu ushahidi kutolewa kwa hiari bila kulazimishwa.

Akitolea mfano, amesema Tanzania imewahi kuwa na tume huru kama ile ya Jaji Kipenka Musa iliyochunguza mauaji ya wafanyabiashara wa madini wa Mahenge, mkoani Morogoro, pamoja na tume ya sakata la Ihefu aliyowahi kuiongoza.

Amesema tofauti na baadhi ya tume za kimataifa, tume hiyo imepata ushirikiano mkubwa kutoka serikalini na wadau mbalimbali, hali inayorahisisha utekelezaji wa majukumu yake.

Ametolea mfano baadhi ya nchi ambako tume za uchunguzi hukumbana na changamoto za mazingira ya kazi, ikiwemo ukosefu wa ushirikiano kutoka mamlaka husika.

Akizungumzia ushiriki wa makundi mbalimbali, amesema tume imepokea maoni kutoka kwa vijana wa kizazi cha Gen Z, waendesha bodaboda, wanafunzi wa vyuo vikuu, wamachinga, na mama lishe kupitia jumuiya zao.

Kuhusu suala la maridhiano, amesema tume ilitembelea pia maeneo ambayo hayakuathiriwa na ghasia, ikiwemo Zanzibar, ili kujifunza uzoefu wa namna ya kujenga amani na mshikamano. “Tulikwenda Zanzibar kujifunza kwa sababu wenzetu wana uzoefu wa maridhiano. Inawezekana mapendekezo yetu yakajumuisha masuala ya maridhiano,” amesema.

Ameutaja pia Mkoa wa Kilimanjaro kuwa miongoni mwa maeneo yaliyotembelewa, licha ya kutokumbwa na ghasia, ili kuelewa sababu za utulivu wake.