KIPA wa Azam FC, Issa Fofana huenda akaondoka mwishoni mwa msimu huu kutokana na kile kinachodaiwa kutoridhishwa na nafasi yake ndani ya kikosi hicho.
Fofana alisajiliwa Azam msimu huu akitokea Al Hilal Omdurman ya Sudan ambako alikuwa na nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza. Mkataba wake Azam unamalizika Juni 30, 2027.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo zinadai kipa huyo anapitia wakati mgumu kwa kukosa muda wa kutosha wa kucheza.
Fofana alisajiliwa Azam FC kama chaguo la kwanza na mbadala wa Mohamed Mustafa, lakini mambo yamekuwa tofauti tangu Aishi Manula arudi kwenye ubora wake.
Licha ya ubora wake na uzoefu alionao, Fofana amejikuta akisugua benchi muda mwingi, jambo lililoibua maswali kutoka kwa wadau.
Inaelezwa kuwa wakala wake amefikisha malalamiko kwa uongozi wa klabu akieleza kutoridhishwa na namna mchezaji huyo anavyopewa nafasi chache.
“Ni kweli kabisa, Fofana anaamini anastahili kupewa nafasi kubwa zaidi kuliko anayopewa sasa,” kilisema chanzo cha Mwanaspoti.
“Kumbuka alikuwa kipa namba moja Al Hilal Omdurman, hivyo ni ngumu kwake kukaa benchi kwa muda mrefu namna hii na hali hii imefanya kutokuwa na raha.”
Wakati mambo yakiwa hivyo, taarifa zinaeleza mabosi wa Al Hilal Omdurman wameanza kufuatilia kwa karibu maendeleo ya kipa huyo.
Inaelezwa klabu hiyo ipo tayari kumrudisha nyota huyo endapo Azam itakuwa tayari kumuachia katika dirisha lijalo la usajili.
Msimu huu katika Ligi Kuu Bara, Azam ikiwa imecheza mechi 17, kipa huyo amedaka tatu mwanzoni mwa msimu dhidi ya Mbeya City, Azam ikiondoka na ushindi wa mabao 2-0, kisha dhidi ya JKT Tanzania na Namungo ambazo zote zilimalizika kwa sare ya 1-1. Ana clean sheet moja.
Hii ina maana kuwa amekosa zaidi ya asilimia 80 ya mechi za timu hiyo, jambo ambalo linaonekana kama pigo kwa kipa aliyekuwa na muendelezo mzuri wa mechi za Afrika.
Wakati Fofana akisugua benchi, ubora wa makipa wazawa ambao wameamua kuonyesha kuwa wanaweza kudumu vizuri nafasi hiyo, Zuber Foba na Aishi Manula umemfanya kipa huyo kuwa na wakati mgumu.
Azam kwa sasa inawatumia zaidi Manula na Foba, ambao wamekuwa wakipokezana kulilinda lango la timu hiyo.
Manula mwenye uzoefu wa miaka mingi kwenye ligi na timu ya taifa, amerejea kwenye kiwango chake bora na kumfanya Kocha Florent Ibenge ashindwe kumwacha nje. Hadi sasa Manula amecheza mechi nane kati ya 17 za Ligi Kuu Bara, moja pekee ameruhusu nyavu zake kutikiswa huku akiwa na clean sheet saba, takwimu nzuri kwa kipa ambaye alikaa nje muda mrefu akiuguza majeraha.
Kwa upande mwingine, Foba amekuwa akionyesha ukomavu kila anapopewa nafasi akicheza mechi sita za Ligi Kuu Bara na kupata clean sheet tano, naye ameruhusu bao mechi moja.