Mbinu ya Trump Yafichuka Vitisho Kwanza, Amani Baadaye kwa Iran

Global Publishers
April 9, 2026
0 Comments

Hatua ya Donald Trump kutangaza kusitisha mapigano kwa muda dhidi ya Iran imezua mjadala mkubwa duniani, huku wengi wakishangazwa na mabadiliko yake ya ghafla kutoka vitisho vizito hadi wito wa amani ndani ya muda mfupi.

Hata hivyo, wachambuzi Jeffrey Sonnenfeld na Steven Tian wanasema hatua hiyo haikuwa ya kushangaza, bali ni mwendelezo wa mtindo wa kawaida wa Trump katika siasa na diplomasia.

Kupitia makala yao iliyochapishwa na Time, wanaeleza kuwa Trump hutumia mbinu ya kuanza mazungumzo kwa vitisho vikubwa ili kuongeza presha, kisha hubadilika na kuingia kwenye mazungumzo ya amani.

Katika mgogoro wa Iran, Trump alitishia mashambulizi makubwa dhidi ya miundombinu muhimu ya nchi hiyo, ikiwa ni pamoja na vituo vya umeme na madaraja. Lakini kabla hata ya vitisho hivyo kutekelezwa, alitangaza kusitisha mapigano kwa muda wa wiki mbili.

Kwa mujibu wa wachambuzi hao, huu ni mkakati wa “kuongeza mvutano ili kuupunguza baadaye” (escalate to de-escalate), ambao humpa Trump nafasi kubwa ya kujadiliana na kupata anachotaka.

Athari za uamuzi huo zilionekana mara moja katika masoko ya dunia, ambapo bei ya mafuta ilishuka kwa kasi huku soko la hisa la Marekani likipanda, ishara kuwa wawekezaji walipokea habari hiyo kwa matumaini.

Licha ya ukosoaji kutoka kwa baadhi ya viongozi na wachambuzi wa kimataifa, mtindo huu unaonekana kuwa sehemu ya “saini” ya Trump katika uongozi wake kuanza kwa nguvu, kisha kumalizia kwa mazungumzo.