Washambuliaji Yanga wapewa kazi nzito baada ya majeraha

BAADA ya kukaa nje kwa muda kutokana na majeraha, hivi sasa Prince Dube na Laurindo Aurelio ‘Depu’ wameanza mazoezi mepesi na wakati wowote watarejea uwanjani.

Lakini, kutokana na hilo, Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves amewapa kazi mpya kuifanya washambuliaji hao akitaka mmoja kati yao achukue tuzo ya mfungaji bora msimu huu Ligi Kuu Bara.

Dube ambaye alipata majeraha ya misuli ya paja na kukaa nje kwa takribani wiki tatu, amekosekana katika mechi tatu za Ligi Kuu Bara.

Kwa upande wa Depu ambaye naye alikuwa akiuguza majeraha ya nyama za paja, amekaa nje kwa kipindi cha takribani wiki tatu na kukosa mechi nne za ligi.

Akiwazungumzia mastaa hao, kocha Pedro alisema, wameonyesha dalili nzuri kwani wote wameshaanza mazoezi hivi karibuni, lakini Dube ndiye amejiunga kabisa na wenzake, huku Depu bado yuko kwenye programu maalum.

Alisema anaamini sana kwenye viwango vya washambuliaji hao na wamerejea muda mzuri ambao timu zimerejea kwa ajili ya mwendelezo wa mzunguko wa pili ambao unakamilisha mbio za ubingwa wa ligi msimu huu.

“Najua viwango vyao na wote wawili wana uwezo mkubwa, lakini wanaporejea kazi yao ni moja tu, nataka mmoja kati yao achukue tuzo ya mfungaji bora wa ligi na hilo linawezekana, sina mashaka nalo kabisa.

“Licha ya wawili hao kupata majeraha, wanatakiwa kukimbiza kufunga mabao kufidia mechi ambazo wamezikosa kwani si nyingi, Dube amerudi mazoezini na Depu yupo kwenye programu maalum ya mazoezi na kocha wa utimamu (fitness coach),” alisema Pedro.

Kocha huyo raia wa Ureno aliongeza kuwa: “Timu tuliyonayo na ubora walionao Depu na Dube vinatosha kabisa kuwasaidia kufikia malengo tuliyojiwekea msimu huu, ikiwemo na tuzo za maeneo tofauti tofauti ikiwemo ufungaji.”

Ndani ya Yanga, huu ni msimu wa pili kwa Dube ambaye aliwahi kuitumikia Azam FC, ambapo ule wa kwanza amefanikiwa kufunga mabao 13 katika ligi, huku msimu huu amefikisha mabao sita akiwa ndiye kinara wa ufungaji kikosini hapo sawa na Depu.

Kwa Depu naye si kitoto licha ya kwamba ametua Yanga usajili wa dirisha dogo la Januari 2026 akitokea Radomiak Radom ya Poland ambako alitumika nusu msimu na kuacha rekodi ya kufunga bao moja kabla ya kusajiliwa Jangwani na mpaka sasa ametikisa nyavu mara sita kwenye ligi.

Msimu uliopita, mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara alikuwa kiungo mshambuliaji wa Simba Jean Ahoua aliyefunga mabao 16.

Kwa sasa msimu huu, kinara wa ufungaji ni mshambuliaji wa Namungo, Fabrice Ngoy mwenye mabao manane ikiwa ni mawili zaidi ya Dube na Depu, huku Saleh Karabaka wa JKT TZ ana saba.