Petroli, dizeli yapanda kwa Sh500 Z’bar, mafuta ya ndege yashuka

Unguja. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura) imetangaza bei mpya za mafuta, ambapo lita moja ya petroli na dizeli imeongezeka kwa wastani wa Sh500.
Wakati bei hizo zikipanda, mafuta ya ndege yameshuka kwa asilimia 0.21 kutoka Sh2,368 hadi kufikia Sh2,363.

Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Zura, Omar Ali Yussuf, usiku wa jana, Jumatano, Aprili 8, 2026, bei hizo zinaanza kutumika leo Alhamisi, Aprili 9.

Katika bei hizo, petroli imeongezeka kwa Sh558 ikilinganishwa na Sh2,942 ya Machi; dizeli imeongezeka kwa Sh548 ikilinganishwa na Sh2,952; na mafuta ya taa yameongezeka kwa Sh600 ikilinganishwa na Sh2,900.

“Mamlaka inapanga bei kulingana na mwenendo wa mabadiliko ya bei za mafuta duniani, gharama za uingizaji, kodi na tozo za Serikali, gharama za mabadiliko ya fedha za kigeni na usafirishaji,” amesema Yussuf.

Kupanda kwa gharama za mafuta kunatokana na vita inayoendelea Mashariki ya Kati kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran. Hata hivyo, mataifa hayo kwa sasa yamesitisha vita hivyo kwa wiki mbili kwa ajili ya mazungumzo.

Hata hivyo, akizungumza hivi karibuni, Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Nadir Abdulatif, alisema kuna mafuta yanayoweza kutosha kwa miezi mitatu.

Alisema iwapo ikipita miezi mitatu bado hali ya vita itaendelea kuwa vilevile, bei inaweza kupanda kidogo, lakini haitakuwa ya kuumiza wananchi kwani Serikali tayari imejipanga kuhakikisha inatoa nafuu kwa wananchi kuhusu gharama hizo.