Mjadala wa mafuta wakolea, yashuka soko la dunia

Dar/Dodoma. Wakati mjadala wa kupanda kwa bei za mafuta ukiendelea kushika kasi nchini, Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza kupunguza msururu wa magari katika misafara yake, ikiwa ni hatua ya kukabili matumizi ya nishati hiyo.

Katika utekelezaji wa hatua hiyo, Rais Samia amesema wakuu wa idara mbalimbali wanaoongozana naye katika misafara wakiwa na magari yao, wote watakuwa wanapanda kwenye basi moja.

Mbali na uamuzi huo, wadau wa mafuta kutoka sekta mbalimbali wametoa mapendekezo mengine mbadala ya kuikabili hali hiyo, likiwemo la kuanzisha vituo vya uhifadhi wa gesi asilia katika mikoa yote nchini.

Wengine, wamependekeza Serikali iangalie namna ya kupunguza kodi na tozo kwenye bidhaa ya mafuta na kuweka ruzuku ili bei ya nishati hiyo ipungue.

Wakati wadau wakitoa mapendekezo hayo, bei hizo za mafuta zimesababisha mtikisiko katika sekta ya usafirishaji, wamiliki daladala wakitishia kugoma kutoa huduma wakidai, nauli wanazotoza ni ndogo ukilinganisha na gharama za uendeshaji, hasa kutokana na ongezeko la bei za mafuta.

Hata hivyo, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), ikiongeza wiki mbili zaidi za kupokea maoni kutoka kwa wadau wa usafirishaji kuhusu mapitio ya nauli baada ya kupanda kwa bei ya nishati hiyo.

Bei ya mafuta imepanda nchini na duniani kwa ujumla, baada ya kuzuka kwa vita Mashariki ya Kati, vinavyohusisha mataifa ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, vilivyoathiri mnyororo wa ugavi wa nishati hiyo.

Kutokana na vita hivyo, Iran ilifunga mlango wa Bahari wa Hormuz, unaotumika kupitisha takriban asilimia 20 ya mafuta yanayosafirishwa kwenye mataifa mbalimbali duniani.

Licha ya yote hayo, kuna matumaini ya kushuka kwa bei ya nishati hiyo baada ya ahadi ya kufunguliwa kwa mlango wa Hormuz, kunakosababishwa na makubaliano ya kusitishwa mapigano kwa wiki mbili.

Wadau wa sekta ya usafirishaji wakifuatilia mjadala wa ongezeko la bei ya mafuta ya petroli na dizeli wakati wa mkutano ulioitishwa na Mamlaka ya usimamizi wa usafiri wa aridhini LATRA jijini Dar es Salaam jana . Picha na  Said  Powa

Misafara ya Rais kupungua

Jana, akihutubia Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, baada ya kuwaapisha viongozi aliowateua, Rais Samia amesema anatambua serikalini kuna matumizi makubwa ya mafuta kwa kuwa kuna magari mengi na safari ni nyingi.

Amewataka maofisa ndani ya Serikali kuanzia sasa kupunguza matumizi ya mafuta, akisisitiza hilo litaanzia katika ofisi yake kwa kupunguza magari ya maofisa anaofuatana nao kwenye misafara yake, ambao kwa sasa watapanda basi moja.

“Msafara utakuwa gari yangu, escort yangu ya polisi na gari ya akiba nyuma, waliobakia wote nawaingiza kwenye basi tupunguze matumizi ya mafuta,” amesema.

Amewataka watumishi wengine kwenye ofisi zao wahakikishe wanapunguza matumizi ya nishati hiyo.

Katika hotuba yake hiyo, amesema kinachoendelea Mashariki ya Kati ndicho kilicholeta athari kwa ulimwengu wote na wiki iliyopita alitumiwa bei za mafuta katika mataifa mbalimbali duniani.

“Kuna nchi ambazo tayari zimeshawapa watu wao ruhusa ya kufanya kazi nyumbani kusiwe na safari za magari kwenda ofisini na kurudi. Kuna nchi zimepunguza matumizi ya mafuta na wana upungufu wa mafuta.

“Leo tumeamka na neno la faraja, kwamba angalau pale Harmors ukiongea nao vizuri wale jamaa, vimeli vinapitapita kwa hiyo inatupa matumaini kwamba meli itapita. Na ile kuruhusu tu mali za Japan, Ufaransa kidogo nimeona bei ya mafuta imeshuka kidogo,” amesema.

Amesema hiyo inatoa matumaini lakini vivyo hivyo haijulikani wataamkaje, namna wanavyoamka na ndivyo bei ya nishati hiyo itakavyocheza pia.

Kwa kuwa upandaji wa bei ya mafuta unaambatana na kupanda kwa bei ya bidhaa, Rais Samia amewataka wafanyabiashara kuhakikisha bidhaa zilizonunuliwa kabla ya msukosuko huo, waangalie namna ya kuweka bei stahiki.

“Isitumike fursa ya kupanda kwa mafuta na kuweka bei za bidhaa kubwa kuliko zinavyopaswa kuwa. Wananchi, kuna bidhaa ambazo zinaingia kipindi hiki ambazo zimekumbana na msukosuko huu zitapanda bei,” amesema.

Amesema iwapo hali itaendelea kuwa tulivu kama ilivyotangazwa leo, huenda hata Tanzania bei ya mafuta ikashuka kwa tangazo la mwezi ujao, ukilinganisha na iliyopo sasa.

Katikakati ya hatua hizo, wamiliki wa daladala wametishia kuegesha magari kuanzia wakidai nauli wanazotoza haziendani na gharama za uendeshaji.

Vilevile, Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) kimeonekana kinaunga mkono kiaina msimamo wa wamiliki wa dalaladala, huku wakiwasilisha mahesabu kwa Mamlaka ya Udhibiri wa Usafiri Ardhini (Latra), yanayoonyesha namna wanavyopata hasara.

Katikakati ya sekeseke hilo, wamiliki hao wamesema kitisho cha mamlaka za Serikali kutishia kuzifutia leseni daladala au mabasi yatakayogoma si suluhisho la hali iliyopo; badala yale wamemtahadhalisha bosi wa Latra, Dk Habibu Suluo kuwa asipokuwa makini suala hilo linaweza kumwondoa kwenye nafasi yake.

Kwa mujibu wa wamiliki hao, bei ya mafuta imepanda lakini Latra, imewataka kuendelea kutoza nauli zilezile za zamani, jambo ambalo linawasababishia hasara.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wasafirishaji Abiria Mkoa wa Mwanza, Yusuph Lupilia amelalakikia kitendo cha usafiri wa bajaji kufanya kazi sawa na daladala katika vituo vyote.

Hayo yameelezwa wakati Latra ikikutana na wadau hao wa usafirishaji kilichohitimishwa kwa kutoa wiki mbili za kupokea maoni yao hadi Aprili 26, 2026.

Hata hivyo, Dk Suluo amesema taarifa za Aprili 8, mwaka huu zinaonyesha bei ya mafuta duniani imeshuka, hivyo baada ya mchakato wa kupokea maoni kukamilika, watapata picha ya hali inavyokwenda.

Amesema leo Alhamisi Aprili 9, 2026, kutakuwa na kikao cha juu cha Serikali kitakachofanyika jijini Dodoma, kitakachoangalia nini kifanyike ili huduma ziendelee.

“Leo hatuna majibu, tunawasikiliza, maana ninyi ndio mpo kwenye uwanja wa kazi ili biashara zenu zisife. Ni lazima tupokee maoni yenu na tuangalie mchakato utakuwa vipi, hususan kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri na wafanyakazi katika sekta hii,” amesema.

Dk Suluo amesema: “Nipeni haki niliyo nayo, leo siwezi kutoa kauli. Kwa bei ya mafuta haijapanda sana kwa mujibu wa viwango tulivyotumia kupanga nauli. Sina mamlaka ya kutangaza nauli, mtakwenda kunishtaki, niwaombe subira tu. Tuendelee kushirikiana kuongea bila mtu kuona anaonewa au kunyanyasika, mazingira ya Serikali ya awamu ya sita yanatupa faraja kuliko huko nyuma.”

Dk Suluo amesisitiza Latra haipo kwa ajili ya kuwarudisha nyuma bali kuwawekea mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao, akisisitiza uvumilivu katika kipindi hiki cha mpito.

Baada ya kikao hicho, wadau hao wa usafirishaji waliitisha kikao chao kingine ambacho hakikufahamika walijadili na kukubaliana nini, lakini mlemle ukumbini kabla ya kikao kufungwa, tayari walikwishaazimia kusitisha huduma.

Suala hilo la mafuta limewaibua Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ambapo kupitia kwa Mkurugenzi wake Mkuu, Dk Anna Henga ikipendekeza Serikali itanue na kuanzisha vituo vya uhifadhi wa gesi asilia katika mikoa yote nchini, ili kukabiliana na uhaba wa nishati ya mafuta.

Ametaka Serikali itoe taarifa rasmi ya ufafanuzi kuhusu ongezeko la bei ya mafuta, ikiwa nchi iliweka akiba ya mafuta ili kukabiliana na mtikisiko wa upatikanaji kwa takribani miezi mitatu, kama ilivyotolewa katika taarifa rasmi ya Serikali Februari 28, 2026.

Aidha, Serikali ipeleke mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria ya Fedha kwa hati ya dharura katika Kikao cha 4 cha Mkutano wa 13 wa Bunge kufuta kwa asilimia 50 ya tozo zote zilizowekwa kwenye kila lita ya mafuta ili kukabiliana na ugumu wa maisha kwa wananchi, kwa muda wa miezi sita.

LHRC imeitaka Serikali kuimarisha na kutekeleza mikakati ya kuongeza akiba ya taifa ya mafuta angalau kwa miaka miwili mfululizo.

Mapendekezo mengine, yametolewa na Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, walioitaka Serikali ipunguze au kuondoa baadhi ya kodi na tozo katika nishati ya mafuta.

Mengine yaliyopendekezwa na jumuiya hiyo ni Serikali kuangalia upya bei za pembejeo za kilimo hususan mbolea na inapowezekana kuanzisha au kuimarisha mfumo wa ruzuku, ili kupunguza gharama kwa wakulima na kudhibiti kupanda kwa bei za bidhaa sokoni.

Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Sheikh Abdallah Ndauga amesema migogoro ya kimataifa haiishii kwenye ramani za kisiasa pekee, bali huingia moja kwa moja katika maisha ya wananchi wa kawaida, kwa kuathiri uchumi, ustawi wa jamii na utulivu wa mataifa.

“Mara nyingi waathirika wakubwa wa migogoro ni raia wasiokuwa na hatia, wakiwemo wanawake, watoto na wazee. Kwa mtazamo huo, wito wetu ni kuendelezwa kwa misingi ya haki na ubinadamu bila upendeleo, wakipinga aina yoyote ya dhuluma,” amesema.

Wabunge walia na matumizi

Ndani ya Bunge, wabunge wametumia sehemu ya michango yako wakati wakijadili makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka 2026/27, kushauri ubanaji wa matumizi, wakiitaka Serikali wapunguze vikao visivyo vya lazima.

Mbunge wa Singida Magharibi (CCM), Elibariki Kingu, amesema mahali Taifa lilipofikia ni lazima Waziri Mkuu akubali kupunguza vikao visivyo vya lazima na kukata posho ili kiasi kitakachookolewa kielekezwe kwenye ruzuku ya mafuta.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kata matumizi lakini ondoa hata baadhi ya kodi, ukifanya hivyo utachukua pointi tano za nchi na Taifa litatabasamu, lakini umefika wakati turuhusu makampuni mengine kushindana kwenye biashara ya mafuta, si hao wanne waliopo sasa,” amesema Kingu.

Mbunge wa Mbinga Mjini (CCM) Jonas Mbunda ameitaka Serikali kuwekeza zaidi kwenye uzalishaji wa gesi na kupunguza gharama, ili watu wengi waone umuhimu wa kutumia gesi katika vyombo vya usafiri.

Mbunge wa Ukonga (ACT-Wazalendo), Bakari Shingo ameitaka Serikali kuweka mkazo ili bei ilipofikia isiongezeke, kwani ikipanda zaidi itapelekea maumivu Zaidi kwa wananchi.

Kwa upande wake Mbunge wa Biharamulo Magharibi (CCM), Ezra Chiwelesa ameihoji Serikali kwa nini aliyetoa taharuki kwa wananchi asijitokeze hadharani kueleza hali ikoje kuhusu mafuta.

“Ndiyo maana Rais alianzisha Wizara ya Mahusiano, fanyeni utaratibu wa kuona nani anaweza kuzungumza kipi na wakati upi, sasa kwenye hili kwa nini hakuachiwa Waziri wa Nishati au Naibu Waziri ndiyo waseme,” amehoji Chiwelesa.

Naye Mbunge wa Hai (CCM) Saashisha Mafuwe amesema kwa hali ilivyo ni lazima Serikali ikubali kuuza akiba ya dhahabu iliyopo ili fedha zitakazopatikana zikasaidie kupunguza makali ya mafuta.

Pamoja na maumivu hayo, kumejitokeza ahueni, baada ya Marekani na Iran kukubaliana kusitisha mapigano kwa muda wa wiki mbili, hatua iliyochochea kushuka kwa bei za mafuta duniani na kupunguza kwa muda mvutano Mashariki ya Kati.

Makubaliano hayo yaliyofikiwa Aprili 7 yanajumuisha kufunguliwa kwa muda kwa njia muhimu ya usafirishaji wa nishati duniani, Mlango wa Bahari wa Hormuz, kufuatia juhudi za dakika za mwisho za kidiplomasia zilizoongozwa na Pakistan.

Tangazo hilo lilitolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump, chini ya saa mbili kabla ya muda wake wa mwisho aliopanga kuanzisha mashambulizi dhidi ya miundombinu muhimu ya Iran, ikiwemo mitambo ya umeme na madaraja.

Kwa mujibu wa Trump, kusitishwa kwa mashambulizi kunategemea Iran kukubali kufungua kikamilifu na kwa usalama mlango wa Hormuz.

Baadaye, alisema siku hiyoni  hatua kubwa kwa amani ya dunia, akidai Iran imeanza kulegeza msimamo wake.

Iran kwa upande wake, kupitia waziri wake wa Mambo ya Nje, Abbas Araghchi ilithibitisha kuwepo makubaliano hayo, ikisema usafiri salama katika mlango huo utaratibiwa na vikosi vyake vya kijeshi kwa kipindi chote cha wiki mbili.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema anaunga mkono kwa tahadhari makubaliano mapya yaliyofikiwa, akibainisha kuwa hayahusishi operesheni dhidi ya Hezbollah nchini Lebanon.

Hata hivyo, mkanganyiko umejitokeza baada ya Iran kutoa matoleo mawili tofauti ya mpango wa vipengele 10, hali inayozua maswali kuhusu msimamo wake, hasa kwenye mpango wa nyuklia.

Pakistan imealika mazungumzo jijini Islamabad, ambapo Iran imethibitisha kushiriki huku Marekani ikiwa bado haijatoa msimamo rasmi.

Kufuatia makubaliano yaliyofikiwa, bei ya mafuta ghafi ilishuka kwa karibu asilimia 15 kufikia dola 93 kwa pipa baada ya Iran, hatua iliyochochea pia kupanda kwa masoko ya hisa barani Asia.