Historia ya mauaji ya kimbari Rwanda isipotoshwe

Kigali. Rais wa Shirika la Manusura wa Mauaji ya Kimbari (Ibuka), Dk Gakwenzire Philbert, amesema kumbukumbu ya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi yaliyotokea mwaka 1994 nchini Rwanda inapaswa kuendelea kuwa msingi wa kujenga taifa lenye umoja, haki na uwajibikaji kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Akizungumza jana na Mwananchi kando ya mkutano wa maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 32 ya mauaji hayo, yanayoendelea katika Ukumbi wa International Conference on Genocide Prevention nchini humo, Dk Philbert alisisitiza umuhimu wa kulinda ukweli wa historia na kupinga vikali juhudi zozote za kupotosha au kukanusha mauaji ya kimbari.

Maadhimisho hayo, yaliyoanza kufanyika jana Aprili 7, 2026, yatadumu kwa siku 100.

“Kumbukumbu si chaguo, ni wajibu. Ni msingi wa heshima kwa waliopoteza maisha na kinga dhidi ya kurudia kwa historia hii chungu,” alisema.

Alionya pia kuwa itikadi ya chuki na ubaguzi bado inaendelea kujitokeza katika mifumo mbalimbali, hasa kupitia mitandao ya kijamii, hivyo alitoa wito kwa vijana kuwa mstari wa mbele katika kuipinga.

“Vijana wanapaswa kuwa walinzi wa ukweli. Kupitia elimu na maadili, wana jukumu la kuhakikisha historia haipotoshwi wala kusahaulika,” aliongeza.

Aidha, alisisitiza haja ya kuendelea kuwasaidia manusura wa mauaji ya kimbari, akieleza kuwa ustawi wao ni sehemu ya haki na uponyaji wa taifa lao la Rwanda.

Awali, akizungumza katika hotuba yake aliyoitoa mbele ya Jeannette, mke wa Rais Paul Kagame wa Rwanda, Dk Philbert alielekeza ujumbe kwa jumuiya ya kimataifa, akitaka hatua madhubuti zaidi zichukuliwe ili kuzuia na kupambana na mauaji ya kimbari pamoja na uhalifu dhidi ya ubinadamu duniani.

“Ulimwengu unapaswa kujifunza kutoka Rwanda. Kutochukua hatua kwa wakati kuna gharama kubwa kwa ubinadamu,” alisema.

Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika chini ya wito wa kuendelea kuenzi kumbukumbu, huku Rwanda ikiimarisha mshikamano na maendeleo ya kijamii baada ya historia ya mwaka 1994.

Akizungumza katika mkutano huo, Jeannette Kagame alisema kumbukumbu ya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi ni nguzo muhimu katika kujenga utu kwa Wanyarwanda, sambamba na kuimarisha mustakabali wa kizazi cha sasa na kijacho.

Alisisitiza kuwa maadhimisho ya kumbukumbu si tu kuhusu kuenzi waliopoteza maisha, bali pia ni nafasi ya kujifunza na kuchukua hatua zaidi za kuimarisha umoja na mshikamano kwa wananchi wote wa Rwanda, bila kujali ukabila, dini wala utamaduni, bali wasalie kuwa wamoja mara zote.

“Kumbukumbu hutufundisha ubinadamu. Hutukumbusha wajibu wetu wa kulinda maisha na kupinga chuki katika aina zake zote,” alisema mke huyo wa Rais Kagame.

Alisema jamii inapaswa kujenga utamaduni wa huruma, mshikamano na uwajibikaji ili kuhakikisha kuwa historia ya mwaka 1994 haijirudia tena.

“Ni jukumu letu sote, hasa viongozi na vijana, kusimama dhidi ya itikadi ya chuki na kuhakikisha ukweli unadumishwa,” alisisitiza.

Pia, Jeannette alisema ustawi wa Taifa la Rwanda ni ustawi wa Wanyarwanda wenyewe, sambamba na heshima wanayopewa na kuthaminiwa na mataifa mengine ndani ya Afrika na duniani kwa ujumla.

Maadhimisho ya mwaka huu yanaendelea kwa siku 100 za kumbukumbu, ambapo Rwanda na dunia kwa ujumla wanatafakari juu ya historia, haki na wajibu wa kuhakikisha kauli mbiu ya “Never Again” inakuwa kwa vitendo.