Mafuta, mbolea na athari ya Iran: Jinsi migogoro ya kimataifa inavyoathiri maisha

Kwa mtazamo wa kwanza, machafuko ya Mashariki ya Kati au vita baridi kati ya mataifa makubwa yanaonekana kama habari za mbali, za kigeni ambazo hazina uhusiano na maisha yetu ya kila siku hapa nyumbani.

Tunazisoma kwenye simu, tunazisikia kwenye redio na kisha tunaendelea na shughuli zetu lakini ukweli ni kwamba, mvutano wowote unaoibuka katika eneo la Ghuba ya Uajemi au njia za kimkakati za kimataifa, huwa na athari ya moja kwa moja kwenye mifuko yetu.

Gharama ya mafuta na mbolea bidhaa mbili muhimu kwa uchumi wetu hutegemea sana usawa wa kisiasa duniani na kwa sasa, sababu ya Iran inakuwa tishio kubwa ambalo haliwezi kupuuzwa.

Kwanza, hebu tuangalie suala la mafuta. Taifa letu ni mwagizaji mkubwa wa mafuta yaliyosafishwa, ingawa sote tunakumbuka matumaini yaliyokuwapo ya kuwa na kinara cha kusafishia mafuta.

Wakati mivutano inapoongezeka katika Mlango wa Hormuz ambako Iran imetishia mara kwa mara kukwamisha usafirishaji wa meli za mafuta, bei za mafuta ghafi duniani hupanda kwa kasi.

Na kwa kuwa soko letu la ndani linategemea uagizaji kutoka nje, mshtuko huo wa bei huwasili hapa kwa muda mfupi sana.

Hatuwezi kujitenga na mfumo huo, msukosuko wowote unaoanza Bandari Abbas au Dubai, unaishia kwenye pampu za mafuta zetu.

Hili sio suala la ushirikina, bali ni uhalisi wa uchumi wa utandawazi unaofanya kila nchi iliyounganishika kuwa dhaifu mbele ya migogoro.

Athari ya pili na pengine yenye madhara zaidi kwa maendeleo yetu ni ile ya mbolea, Iran imekuwa muuzaji muhimu wa mbolea aina ya urea na bidhaa nyingine za petro kemikali kwa soko la kimataifa.

Wakati vikwazo vya kiuchumi vinapozidishwa dhidi ya Tehran au wakati mvutano wa kivita unapoingilia usafirishaji katika Bahari ya Shamu na Bahari Nyekundu, ugavi wa mbolea hukatika.

Matokeo yake ni bei ya mbolea kushamiri mitaani na kulazimisha wakulima wetu ambao tayari wanakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na gharama ya pembejeo kununua kwa bei ya juu au kukosa kabisa.

Wakulima wanaposhindwa kutumia mbolea, uzalishaji wa chakula hupungua na hatimaye tunarudi pale tulipoanza bei ya chakula inapanda na njaa ya kipato inawasumbua Watanzania wengi.

Katika muktadha huu, ni muhimu kwa serikali na wadau wauchumi kufanya uamuzi makini. Hatuwezi kudhibiti migogoro ya kigeni lakini tunaweza kujenga nguvu ya kustahimili mshtuko.

Hii inamaanisha kuwa lazima tuharakishe utafutaji wa vyanzo mbadala vya nishati na mbolea, tunahitaji kuangalia upya uwezekano wa kuongeza matumizi ya mbolea za asili zinazopatikana ndani ya nchi, kuwekeza zaidi katika kilimo cha kisasa kinachotumia pembejeo za ndani na pia kuimarisha uhusiano na wauzaji mbadala wasioathirika kirahisi na mvutano wa kijiografia.

Zaidi ya hayo, ni wakati muafaka wa kuongeza uwekezaji katika sekta ya nishati jadidifu kama vile jua na upepo ili kupunguza utegemezi wetu wa mafuta yanayoingizwa kutoka maeneo yenye misukosuko.

Hatimaye, dunia ya leo imekuwa kijiji kimoja, hakuna nchi iliyojitenga, migogoro inayoonekana kuwa ya mbali kama ile inayohusisha Iran na mataifa ya Magharibi au mvutano katika njia za bahari ina uwezo wa kubadilisha maisha ya mwananchi wa kawaida hapa Tanzania.

Hatuna budi kuacha mtazamo wakujiona kuwa watazamaji tu, bali tujenge mikakati ya kitaifainayotutayarisha kwa gharama za juu zinazoletwa na hali hii.

Sera zetu za kiuchumi, hasa katika sekta ya kilimo na nishati lazima ziwe na lengo la kujitosheleza na kupunguza udhaifu wetu kwa mishtuko ya nje. Vinginevyo, tutaendelea kuwa tegemezi, tukilipa gharama kubwa ya migogoro tuliyo nayo niaya kuiepuka.