Iran yatoa onyo kulipiza kisasi, Israel ikiishambulia Lebanon

Israel imeishambulia Lebanon kwa mashambulizi makali zaidi kuwahi kushuhudiwa Jumatano iliyopita, na kusababisha vifo vya mamia ya watu huku Iran ikitoa onyo la kulipiza kisasi, ikiashiria kuwa haitakuwa busara kuendelea na mazungumzo ya kufikia makubaliano ya kudumu ya amani na Marekani.

Onyo hilo kutoka kwa mpatanishi mkuu wa Iran, Spika wa Bunge, Mohammed Bager Qalibaf, limeweka wazi hali tete inayoendelea katika eneo hilo kufuatia tangazo la usitishaji mapigano lililotolewa Jumanne na Rais wa Marekani, Donald Trump.

Pande hizo mbili zimewasilisha ajenda zinazokinzana kwa kiasi kikubwa kuhusu mazungumzo ya amani yanayotarajiwa kuanza Jumamosi ijayo, huku ikiwa bado haijulikani kama usitishaji huo wa mapigano wa wiki mbili utaendelea hadi wakati huo.

Qalibaf amesema Israel tayari imekiuka masharti kadhaa ya usitishaji huo kwa kuongeza mashambulizi dhidi ya kundi la wanamgambo la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran, huku Marekani nayo ikivunja makubaliano kwa kusisitiza Iran iachane na mpango wake wa nyuklia.

“Katika hali kama hii, usitishaji wa mapigano wa pande mbili au mazungumzo hayana mantiki,” amesema katika taarifa yake.

Israel na Marekani zote zimesema kuwa usitishaji huo wa mapigano wa wiki mbili hauhusu Lebanon, huku Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akisisitiza kuwa mashambulizi yataendelea.

“Nadhani Wairani walidhani usitishaji huo unaihusu Lebanon, lakini sivyo ilivyo,” amesema Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, ambaye ataongoza ujumbe wa Marekani katika mazungumzo hayo, akizungumza na waandishi wa habari mjini Budapest, Hungary.

Pande hizo pia zinaonekana kutofautiana kwa kiasi kikubwa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, ambao ni miongoni mwa sababu zilizotajwa na Trump kuanzisha vita.

Trump amesema Iran imekubali kusitisha urutubishaji wa uranium, ambayo inaweza kutumika kutengeneza silaha za nyuklia, huku Ikulu ya White House ikisema Iran imeonyesha utayari wa kukabidhi akiba yake iliyopo.

“Marekani, kwa kushirikiana na Iran, itachimba na kuondoa kabisa mavumbi yote ya nyuklia yaliyofichwa kwa kina,” Trump ameandika kwenye mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, Qalibaf amesema Iran inaruhusiwa kuendelea na urutubishaji wa uranium chini ya masharti ya usitishaji huo wa mapigano.

Ingawa Marekani na Iran zote zimetangaza ushindi katika vita vilivyodumu kwa wiki tano na kusababisha vifo vya maelfu ya watu, tofauti zao kuu bado hazijapatiwa ufumbuzi. Kila upande unaendelea kusimamia matakwa yake kinzani kuhusu makubaliano yatakayoweza kuathiri mustakabali wa Mashariki ya Kati kwa vizazi vijavyo.

Licha ya hali hiyo ya sintofahamu, masoko ya hisa duniani yalipanda, huku bei ya mafuta ikishuka kwa asilimia 14 hadi kufikia takriban dola 95 kwa pipa, baada ya kushuka hadi dola 90.40.

Hata hivyo, bei ya mafuta ghafi ya Brent bado iko juu kwa takriban dola 25 ikilinganishwa na kabla ya mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel kuanza.

Uwezo mpya wa Iran wa kukatiza usambazaji wa nishati katika Ghuba kupitia udhibiti wake wa Mlango Bahari wa Hormuz, licha ya uwekezaji mkubwa wa kijeshi wa Marekani katika eneo hilo kwa miongo kadhaa, unaonyesha namna mgogoro huo ulivyobadilisha mizani ya nguvu katika ukanda huo.

Netanyahu amesema Israel iko tayari kurejea vitani wakati wowote, akisisitiza kuwa kidole kiko kwenye kitufe cha kufyatulia risasi.

 Huduma ya ulinzi wa kiraia nchini Lebanon ilieleza kuwa watu 254 waliuawa katika mashambulizi ya Israel kote nchini humo juzi. Idadi kubwa ya vifo iliripotiwa katika mji mkuu, Beirut, ambapo watu 91 waliuawa. Wakazi wamesema baadhi ya mashambulizi hayo yalifanyika bila tahadhari za kawaida kwa raia kuondoka maeneo hatarishi.

Hezbollah, kundi la wanamgambo linaloungwa mkono na Iran nchini Lebanon, limesema mapema leo Aprili 9,2025  kuwa lilirusha makombora kuelekea kaskazini mwa Israel kujibu ukiukwaji wa usitishaji wa mapigano.

 Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amelaani kwa nguvu zote mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon, akisema kuwa hayakubagua, na kusisitiza kuwa Lebanon inapaswa kujumuishwa kikamilifu katika usitishaji wa mapigano.

Viongozi wa nchi 13 za Ulaya, Japan na Canada pia walitoa tamko la pamoja wakihimiza kusitishwa kwa haraka kwa mapigano ili kuepusha mgogoro mkubwa wa nishati duniani.