Dodoma. Mwanga kwa vijana wanaomaliza vyuo vikuu na kuhitaji mikopo lakini hawana dhamana, hii inaweza kuwa neema kwao baada ya Serikali kuahidi kupeleka sheria bungeni ya kutambua vyeti kama dhamana.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ameliambia Bunge kuwa, wakati wowote sheria ya kutaka vyeti vya kuhitimu taaluma za vyuo, itapelekwa bungeni ili iwe sehemu ya dhamana.
Hoja hiyo huenda ikawa ni mwarobaini wa kilio cha muda mrefu ambacho mara kadhaa kiliwasilishwa na aliyekuwa Mbunge wa Kahama (CCM), Jumanne Kishimba.
Mara nyingi Kishimba alilalamika utaratibu unaotumiwa na Serikali wa kukataa kuwapa mkopo vijana waliohitimu masomo yao wakiwa na vyeti wakati wao walilipa fedha nyingi za ada na matokeo yake wakatunukiwa vyeti.
Dk Mwigulu ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Aprili 9, 2026 wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu ambapo alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Timida Fyandomo ambaye swali lake limehoji Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia vijana kuwekeza na kuwaungainisha kwenye kampuni kubwa za ndani na nje ya nchi.
Waziri Mkuu amesema mpango wa kutaka vijana watumie vyeti kama dhamana uko katika hatua nzuri na wakati ukifika watapeleka bungeni ili kuitungia sheria ya dhamana inayohamishika.
Amesema hali ilivyo sasa, wasomi wengi wamelundikana bila kazi na kwa baadhi ya maeneo wamekuwa ni mzigo kwa wastaafu ambao waliwasomesha.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Serikali imefungua madirisha mbalimbali kwa ajili ya kuwawezesha vijana ikiwemo Sh200 bilioni ambazo zimetengwa kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Waziri Mkuu amesema ndani ya ilani ya uchaguzi ya CCM, zaidi ya ajira milioni nane zitatolewa katika kipindi cha utekelezaji.