Julio: Mechi na Geita ni vita ya watu wazima

Kocha wa Mashujaa FC ya mkoani Kigoma, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, amesema mchezo wa kesho Ijumaa dhidi ya Geita Gold katika mashindano ya CRDB Federation Cup hatua ya 16 bora, itakuwa vita ya watu wazima kulingana na ushindani uliopo baina ya timu hizo pindi zinapokutana.

Julio amesema anatambua ugumu wa mchezo huo kutokana na uwezo mkubwa wa Zuber Katwila ambaye ni kocha wa Geita Gold, huku pia akimtaja kuwa miongoni mwa walimu wa soka wenye uzoefu katika kuziongoza timu za Ligi ya Championship.

Julio ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Aprili 9, 2026 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya CRDB mkoani Geita, kuelekea mchezo wa 16 bora utakaozikutanisha Geita Gold na Mashujaa kwenye Uwanja wa Shule ya Wasichana Nyankumbu mkoani Geita.

“Ukiangalia Geita Gold kwenye Championship, ukikutana nayo utakuja kufedheheka mtu mzima, kwahiyo tunaingia kucheza na watu wazima wenzetu ambao walikuwa kwenye Ligi Kuu, sio mechi ya kitoto lakini tumejipanga kupambana kama ambavyo wenzetu wamejipanga ili mwenye bahati na aliyejipanga vizuri aweze kusonga mbele,” amesema Julio.

Pia Julio amekiri mashindano hayo kuwa magumu, hata hivyo amesema kikosi chake kimejipanga kupata ushindi kwakuwa ndoto yao ni kucheza mashindano ya kimataifa msimu ujao huku katika Ligi Kuu wakijipanga kumaliza nafasi nne za juu ambapo hivi sasa wapo nafasi ya 11 na alama 20.

“Sisi Mashujaa tunahitaji nafasi hiyo kushiriki kimataifa ukizingatia mwenendo wetu ambao mwanzo ulitaka kuonekana mbaya lakini sasa kuna nafuu fulani,” amesema.

Kwa upande wake Kocha wa Geita Gold, Zuberi Katwila, amebainisha kuwa kulingana na uzito wa ushindani walionao kwenye Ligi ya Championship katika kupanda ligi kuu pamoja na mashindano hayo ya FA, wamejipanga kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi huku akitarajia kuwatumia wachezaji waliokuwa hawapati nafasi ya kucheza.

Katwila amesema wachezaji waliokuwa hawapati nafasi anawaamini kwakuwa ndiyo walioifikisha timu katika hatua ya 16 bora, hivyo anaamini wana uwezo wa kuifikisha katika hatua ya nane bora ya mashindano hayo.

“Ni ‘rotation’ ambayo tulikuwa tunaifanya toka awali, wanaocheza Championship ni wengine na watakaocheza FA ni wengine, mechi zetu zote za FA wanatumika hao ambao ni wachezaji wetu lakini katika Championship wanakuwa kidogo wanakosa nafasi, hii ni mtoano ambayo lazima utumie wachezaji ambao watakuwa na nguvu ya kutosha kupambana na mchezo,” amesema Katwila.

Naye Mtenje Albano wa Geita Gold na Daniel Lyanga wa Mashujaa, wamewahakikishia mashabiki kuonyesha soka safi katika mchezo huo ambao Mlezi wa Geita Gold ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita, Yefred Myenzi, amelipia tiketi zote za mchezo huo kuwarahisishia mashabiki kuingia bure.