Joseph Jr: Haikuwa rahisi kufika Celta Vigo

BAADA ya Mtanzania, Joseph Junior Michael Joseph kupata nafasi ya kusajiliwa Celta Vigo ya Hispania katika kikosi cha vijana chini ya miaka 19 (Juvenil B), amesema haikuwa rahisi kufika hapo.

Mchezaji huyo chipukizi anayefahamika zaidi kama JJ aliyezaliwa mwaka 2008, amepata nafasi katika kikosi hicho baada ya takribani miaka mitatu ya maendeleo ya kisoka kupitia mpango wa A Canteira Experience, programu iliyoundwa kukuza na kuwaingiza wachezaji vijana katika falsafa ya klabu hiyo.

Akizungumza na vyombo vya habari vya klabu hiyo, Joseph alieleza safari ya kutoka Tanzania kwenda Hispania ilikuwa na changamoto pia ilimjenga kwa kiwango kikubwa.

“Matarajio yalikuwa makubwa nilipowasili Vigo kupitia mradi huu, lakini nilipojiunga rasmi na klabu, yalikuwa makubwa zaidi ya nilivyodhani,” amesema.

“Kadri muda ulivyopita, niliweza kuzoea kutokana na msaada nilioupata kutoka kwa watu wanaonizunguka. Uzoefu huu umebadilisha mtazamo wangu kwa sababu nahisi nimekua katika nyanja nyingi za maisha yangu.”

Kupandishwa kwake hadi timu ya U19 B, kunaonyesha dira ya muda mrefu ya programu hiyo katika kubaini vipaji vya kimataifa, kuwasaidia kuzoea utamaduni mpya wa soka na hatimaye kuwapatia njia ya kuingia katika mifumo ya ushindani Ulaya.

Mbali na soka, A Canteira Experience inaweka mkazo mkubwa katika maendeleo ya jumla ya mshiriki. Wachezaji huunganisha mazoezi na elimu rasmi, ikiwemo masomo ya sekondari na programu za kimataifa za elimu zinazotolewa Vigo na maeneo ya jirani. Pia, kujifunza lugha na kuzoea utamaduni ni sehemu muhimu zinazowasaidia wachezaji kuendana na maisha ya Hispania.

Tangu kuanzishwa kwake, mpango huo umevutia takribani wachezaji 400 kutoka zaidi ya nchi 50, zikiwemo Brazil, Ujerumani, Japan, Marekani pamoja na mataifa kadhaa ya Afrika. Hata hivyo, safari ya Joseph yanaonekana wazi kama mfano halisi wa matokeo chanya ya programu hiyo.

Joseph anayecheza nafasi ya beki wa kati, safari yake kisoka ilianzia Tanzania katika akademi ya Magnet Youth Sports na usajili wake Celta Vigo kupitia timu ya vijana (Juvenil B), ulikamilika mapema mwaka huu.