Mwanafunzi afariki dunia kwa kupigwa na radi Tabora

Tabora. Mtoto mmoja, Aishara Shingu (11), aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Ussoke iliyopo Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, amefariki dunia na watu wengine watano wakijeruhiwa baada ya kupigwa na radi.

Akizungumzia tukio hilo leo Aprili 9, 2026, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Tabora, Loshipay Laizer amesema watu hao walipigwa na radi wakiwa chini ya mti huko Ussoke wilayani Urambo.

Laizer amesema wakati mvua inanyesha, walikua shambani wanaendelea na shughuli zao, wakajificha chini ya mti ili kujikinga na mvua na hapo ndipo radi ilipowapiga na mtoto huyo akafariki dunia papo hapo.

“Wakiwa wamejificha chini ya mti ili mvua isiwanyeshee sana, ndipo radi ikawapiga na ndio huyu mtoto amepoteza maisha na wengine wamejeruhiwa na wanaendelea na matibabu,” amesema.

Amewataja majeruhi wa radi hiyo kuwa ni pamoja na Mamula Shingu (43), Marando Shingu (24), Danale Rungole (21), Pumbula Mango (29) na Tungu Masanja (41), na sasa wanaendelea na matibabu wilayani humo kufuatia majeraha yaliyosababishwa na radi.

“Hali zao sio mbaya na wanaendelea na matibabu na wengine wametibiwa tu na kuondoka ila wengine ilibidi kulazwa kutokana na ukubwa wa majeraha yao,” amesema.

Ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kukaa chini ya miti katika kipindi hiki ambapo wakati mvua zinaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini kwani miti mikubwa ina uwezekano mkubwa wa kuangukiwa na radi.

Katika tukio jingine, Laizer amesema wilayani Nzega, mwanaume mmoja ambaye majina yake bado hayajafahamika, amefariki dunia kwa kuzama kwenye dimbwi la maji ambapo alikuwa akitega samaki, ndipo akazama kwenye maji.

“Tumefika eneo la tukio tutakuta kweli amezama kwenye maji, tumeopoa mwili maana bahati mbaya alikuwa tayari ameshafariki dunia,” amesema.