Dar es Salaam. Tanzania imepata bahati kuwa nchi ya kwanza Afrika kuzindua mfumo mpya wa kidijitali wa DriverLinkAfrica, unaotumika kuajiri madereva wenye sifa kitaaluma na ubora unaotajwa utabadilisha sekta ya usafiri na usafirishaji.
Mfumo huo unaotumia aplikesheni maalumu ambayo kampuni zitajiunga kwa ajili ya kuajiri madereva waliojisajili utasaidia kupata madereva bora, wenye sifa zote hitajika, pia kudhibiti changamoto mbalimbali walizonazo baadhi ya madereva ikiwemo wizi, ulevi na kukosa uaminifu.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi leo Alhamisi 9, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Deep Search International inayomiliki mfumo huo wa kidijitali, Yusuf Washokera amesema mfumo utaongeza kipato cha madereva, kuwapeleka kimataifa pamoja na kurahisisha upatikanaji wao kwa kampuni za usafirishaji.
“Mfumo huu umezinduliwa Tanzania kwanza kisha Kenya, Uganda, Rwanda halafu nchi zote za Afrika, ambapo dereva mwenye sifa atapata ajira nje ya nchi ikiwemo Mashariki ya Kati.”
“Dereva atatuma wasifu wake kwenye jukwaa hili lenye kazi za udereva zaidi ya 72. Pia kampuni zitakuwa na akaunti kwa ajili ya kuajiri na kuwasimamia madereva,” amesema.
Imeelezwa hatua hiyo ni mwelekeo wa kidijitali katika sekta ya usafiri nchini ambapo faida zake, Washokera amesema utasaidia madereva kupata kazi ndani na nje huku nchi zote 54 za Afrika zikiwa zinaona wasifu wa madereva hao.
“Mfumo huu ndio utakuwa chanzo kikuu cha ajira kwa madereva na imekuwa heshima kubwa kuzinduliwa Tanzania kisha kwenda katika nchi zingine,” amesema,
Akieleza zaidi Washokera amesema zilifanyika tafiti kupitia mfumo huo na kubaini utapunguza wizi kwa kuwa kampuni zitakuwa zinawasimamia madereva kupitia kuwawekea alama ya orodha nyeusi ‘blacklist’ kwa wale wenye tabia za wizi, kutelekeza magari au ulevi.
Amesema kampuni za ndani na nje ya nchi zitakuwa zinaona sifa za madereva walioweka wasifu wao kwenye mfumo huo, huku dereva atakuwa na nafasi ya kuchagua yeye anataka kufanya kazi na kampuni gani.
Hata kampuni zisizo na uadilifu kwa madereva kama kutowalipa mishahara au unyanyasaji zitakuwa zimekosa sifa ya kuendelea kuwepo kwenye mfumo huo.
Akifafanua zaidi amesema mfumo umeunganishwa na taasisi za Serikali sekta ya usafirishaji, kampuni, wadau na vyama madereva na vya usafirishaji na mamlaka ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra).
Phillip Changala msimamizi wa shughuli za uendeshaji kampuni ya usafirishaji Mofat, amesema kitendo cha kuwapata madereva kidijitali tayari kinaheshishima kada hiyo.
