Haya hapa maeneo muhimu kukuza sekta ya fedha

Dar es Salaam. Serikali imeainisha maeneo nane ya kipaumbele ndani ya sekta ya fedha ambayo yakitumika ipasavyo kwa ushirikiano na sekta binafsi yanaweza kuharakisha ukuaji wa uchumi.

Maeneo hayo ni pamoja na ufadhili wa tabianchi, mabadiliko ya tabianchi, huduma za kifedha za Kiislamu, udhibiti wa mali za kidijitali, upatikanaji wa mitaji kwa biashara changa na ndogo, elimu ya fedha, ulinzi wa watumiaji wa huduma za kifedha, pamoja na kupunguza hatari katika utoaji wa mikopo.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Fedha, Khamis Mussa wakati wa Jukwaa la Pili la Sekta ya Fedha 2026, lililofanyika chini ya kaulimbiu: “Ubunifu na Sekta ya Fedha Inayowajibika kwa Maendeleo Endelevu na Shirikishi ya Kijamii na Kiuchumi.”

Jukwaa hilo pia lilishuhudia uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Bima Jumuishi (NIIS) na Mkakati wa Utafiti, Ubunifu na Maendeleo.

Mussa amesema mabadiliko ya tabianchi na ufadhili wa miradi ya tabianchi yamekuwa vipaumbele vya kimataifa, huku kukiwa na msukumo mkubwa wa kufadhili miradi inayokabiliana na changamoto za mazingira.

Amesema licha ya Tanzania kuwa tayari imeweka mifumo inayolingana na ufadhili huo, bado kuna fursa na changamoto zinazohitaji juhudi za pamoja na mkakati madhubuti zaidi.

“Kuna fursa kubwa katika ufadhili wa kijani (green financing) hivyo ni umuhimu Tanzania kujipanga kunufaika nazo,” amesema.

Pia ameaema Tanzania imeendelea kushuhudia kuongezeka kwa uhitaji wa huduma fedha zisizo na riba, hususan huduma za kifedha za Kiislamu kama benki za Kiislamu, bima ya takaful na hati fungani za sukuk.

Amesema huduma hizo zinatoa mbadala wa benki za kawaida kwa kutumia mfumo wa kugawana hatari badala ya riba.

“Kufuatia mahitaji yake tayari tumeona kuna maendeleo kupitia bidhaa za takaful na masoko ya mitaji yanayozingatia Sharia lakini kuna haja ya kupanua huduma hizo na kuimarisha mifumo ya kisheria,” amesema.

Kuhusu maendeleo ya teknolojia ya kifedha, amesema matumizi ya sarafu za kidijitali kama Bitcoin na majukwaa ya kifedha mtandaoni yameongezeka, hali inayohitaji kuimarishwa kwa sheria na kanuni wakati ambao serikali inaandaa sheria mpya kudhibiti mali za kidijitali.

Kuhusu Upatikanaji wa mitaji kwa vijana na wanawake wanaoanzisha biashara ulitajwa pia kuwa na changamoto kubwa huku akisema ipo haja ya kuimarisha mifumo ya mitaji binafsi ili kusaidia kukuza biashara hizo.

Alitumia nafadi hiyo kusisitiza umuhimu wa elimu ya fedha na ujumuishwaji wa kifedha, akibainisha kuwa bado kuna pengo kubwa la uelewa miongoni mwa wananchi.

“Ni muhimu kuboresha elimu ya fedha, kukuza ujasiriamali na kubuni bidhaa za kifedha zinazolenga watu wa kipato cha chini ili kupunguza utegemezi wa mikopo isiyo rasmi yenye masharti magumu,” amesema.

Mussa amesema utekelezaji mzuri wa maeneo haya utaimarisha sekta ya fedha na kusaidia maendeleo endelevu ya uchumi kulingana na Dira ya Maendeleo 2050.

Aliwataka wadau kuimarisha usimamizi wa huduma mpya za kifedha za kidijitali ili kulinda watumiaji na kuongeza juhudi za kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa vijana, wanawake na biashara changa, pamoja na kuimarisha elimu ya fedha.

Kwa upande wake, Kamishna wa Mamlaka ya Udhibiti wa Bima Tanzania (TIRA), Bahayo Saquare amesema mamlaka hiyo imekamilisha mikakati miwili muhimu ya kuimarisha sekta ya bima.

Ameeleza kuwa mkakati wa kwanza unalenga kupanua huduma za bima kwa wananchi wanaojishughulisha na ufugaji na madini huku wa pili ukihamasisha bima zinazochangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Utekelezaji wa mikakati hiyo utaongeza upatikanaji wa huduma za bima, hasa kwa biashara, miundombinu na magari, na kufanya huduma hizo kuwa bora na bunifu zaidi,” amesema.

Hatua hiyo inatarajiwa kuharakisha maendeleo ya sekta ya fedha, kukuza uchumi na kuongeza mchango wa sekta ya bima katika Pato la Taifa kutoka asilimia 22 hadi 30