UN kuamua hatima ya Mahakama ya mauaji ya kimbari

Arusha. Hatima ya safari ya zaidi ya miaka 32 ya kutafuta haki kwa waathirika takriban milioni moja wa mauaji ya kimbari ya Rwanda inatarajiwa kujulikana Juni 2026, katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kinachotarajiwa kukutana jijini Arusha.

Baraza hilo litakutana kufanya uamuzi kuhusu mustakabali wa utaratibu wa mabaki ya Mahakama za Kimataifa za Jinai uliopo Arusha.

Litaanza kwa kujadili mwenendo wa kituo hicho ambacho kimekuwa kikifanya kazi kwa miaka 16, kikiwa na jukumu la kusimamia masuala yaliyosalia baada ya kufungwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Rwanda iliyodumu Arusha kwa miaka 15.

Katika mijadala hiyo, miongoni mwa uamuzi unaotarajiwa kutolewa ni kufunga kabisa kituo hicho au kuhamisha majukumu yake kwenda eneo lingine.

Naibu Katibu Mkuu Msaidizi na Msajili wa Mechanism ya Kimataifa ya Mabaki ya Mahakama za Makosa ya Jinai (IRMCT), Abubacarr Tambadou amesema uamuzi wa mwisho kuhusu iwapo kituo hicho kitaondoka kabisa Tanzania utafikiwa katika kikao hicho cha Juni 2026.

Tambadou ametoa kauli hiyo wakati wa maadhimisho ya miaka 32 ya mauaji ya halaiki ya Rwanda yaliyofanyika katika makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Arusha, yakihusisha pia wananchi wa Rwanda wanaoishi katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

“Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litatoa uamuzi wa mwisho katika kikao chake kijacho; hapo ndipo tutajua iwapo shughuli zitafungwa au majukumu kuhamishwa,” amesema Tambadou.

Ameongeza kuwa baada ya Baraza la Usalama kufikia uamuzi, ofisi ya IRMCT Arusha itatoa taarifa rasmi kueleza mwelekeo wa hatua zitakazochukuliwa.

Iwapo uamuzi huo utakuwa wa kufunga kituo hicho, utahitimisha enzi muhimu ya mchakato wa haki ulioanza zaidi ya miongo mitatu iliyopita kufuatia mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.

Kituo hicho kilichopo katika eneo la Kilima cha Lakilaki, kando ya barabara ya Arusha – Minjingu, kilianzishwa mwaka 2010 kuchukua majukumu ya ICTR iliyofungwa rasmi mwaka 2009.

Katika mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994, takriban watu milioni moja waliuawa, huku baadhi ya watuhumiwa waliokimbia bado wakiwa hawajakamatwa hadi sasa.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1995, ICTR iliwafungulia mashitaka watu 93 waliodhaniwa kuhusika na ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu.

Kati yao, watu 62 walihukumiwa, kesi 10 zilipelekwa katika mahakama za kitaifa huku watatu wakihamishiwa IRMCT mwaka 2010.

Aidha, watuhumiwa 10 waliachiwa huru katika kipindi cha uendeshaji wa mahakama hiyo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha.

Mamlaka za Rwanda zinasisitiza kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kuwafikisha baadhi ya wahusika mbele ya sheria, bado kuna watuhumiwa waliokimbia na wanaendelea kuishi kwa uhuru katika nchi mbalimbali barani Afrika, Ulaya na Amerika Kaskazini.

Katika hotuba yake ya maadhimisho hayo, Rais wa Rwanda, Paul Kagame alizitaka nchi hizo kushirikiana katika kurejesha watuhumiwa hao ili wafikishwe mbele ya haki.

Alisisitiza kuwa haki kwa waathirika bado haijakamilika iwapo wahusika wataendelea kukwepa uwajibikaji.

“Haki haiwezi kukamilika wakati waliohusika na mauaji ya kimbari bado wako huru wakijificha katika nchi nyingine. Hatutaruhusu yaliyotokea mwaka 1994 yajirudie tena,” alisema katika Kituo cha Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari Kigali, juzi.

Aliongeza kuwa mauaji ya kimbari huanza kwa kukataa ukweli, mgawanyiko na kutojali, pia alisisitiza kuwa nguvu ya Rwanda ipo katika uwezo wake wa kuinuka na kujijenga upya baada ya historia hiyo chungu mioyoni mwa wananchi wake.